Mwanza. Wakati matukio ya wizi na kupotea kwa watoto yakishamiri nchini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia George Mlalo (21), mkazi wa Kisiwa cha Kamasi wilayani Ukerewe kwa tuhuma za wizi wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.
Mtuhumiwa ambaye ni mvuvi alikamatwa Agosti 16, mwaka huu saa moja usiku katika Kisiwa cha Ghana wilayani Ukerewe, Mkoa wa Mwanza kwa kosa la kumuiba mtoto, Precious Mathew, mkazi wa Kisesa wilayani Magu.
Akizungumza leo Agosti 23, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amedai kuwa, mtuhumiwa alimuiba mtoto huyo akieleza alimpenda hivyo alikwenda kuishi naye kwa kuwa yeye hana watoto.
Amesema mtoto huyo aliripotiwa kupotea Agosti 10, mwaka huu Kisesa wilayani Magu.
Amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa walimfanyia uchunguzi wa kitabibu mtoto na ikabainika yuko salama.
“Baada ya kumpata mtoto amefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na hali yake kwa jumla ilionekana kuwa ni nzuri, vipimo vimethibitishwa na daktari hajapata changamoto yoyote ya kiafya achilia mbali kwamba alikuwa ametenganishwa na mzazi wake, kwa hiyo maisha yanaendelea kama kawaida,” amesema.
Kamanda Mutafungwa amesema mtoto amekabidhiwa kwa mama yake, Irine Festo (22), mkazi wa Mabatini jijini Mwanza na kwamba anaendelea vizuri.
Amesema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
“Wakati tunamkamata tulimkuta akiwa na mtoto huyo, alikuwa akiishi naye kama mwanaye na alipohojiwa alidai aliamua kumuiba kwa sababu alimpenda,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda Mutafungwa amesema miongoni mwa sababu walizobaini katika uchunguzi wa matukio ya kupotea na wizi wa watoto ni wanandoa kutaka kuridhishana pale wanapokosa watoto, huku upotoshaji wa taarifa nao ukichangia.
“Sababu ninayoona kubwa kwenye matukio ya aina hiyo ni changamoto za uzazi katika familia. Unakuta kumejaa lawama kati ya wanandoa, mwanamke anaiba mtoto ili amdanganye mume wake kwamba alipata ujauzito na amejifungua, sasa familia ina mtoto ili ipate furaha, sababu za aina hiyo zimekuwa zikijitokeza katika matukio mengi,” amesema.
“Pia suala la watu kutia chumvi taarifa au kutoa ambazo hawana uhakika nazo mara nyingi kunakuwa na hisia nyingi na maneno mengi kuliko uhalisia. Tunaomba wananchi watoe taarifa matukio yanapotokea kama huna uhakika usiingie kupotosha jamii.”
Amesema jamii ijihadhari na taarifa zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii.