Mapya yaibuka kesi ya ‘waliotumwa na afande’

Dodoma. Kesi ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti wa Yombo Dovya, Dar es Salaam imeahirishwa hadi Agosti 28, 2024 kupisha shauri la maombi ya marejeo lililofunguliwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma.

Maombi ya marejeo namba 23476/2024 yamefunguliwa leo, Ijumaa Agosti 23, 2024 na Leonard Mashabara na yametajwa faragha mbele ya Jaji Suleiman Hassan.

Wakili Emanuel Anthony, anayemwakilisha Mashabara akizungumza na Mwananchi amesema wanaiomba Mahakama ingalie kumbukumbu na mwenendo wa kesi ya jinai iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Zabibu Mpangule wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.

“Tunaomba Mahakama Kuu ijiridhishe na uhalali wa mawakili ambao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuwakilisha washtakiwa au kuwatetea ilhali TLS kupitia baraza uongozi lilitoa tamko  Agosti 5 kwamba wale watuhumiwa ni wahalifu,” amesema.

Amesema kupitia tamko hilo, TLS ilisema watashirikiana na vyombo vya haki jinai ambavyo ni polisi, waendesha mashtaka, Jeshi la Magereza na vyombo vya haki.

Wakili huyo amesema wanaiomba Mahakama itamke kama ni halali kwa mawakili hao kuendelea kuwatetea washtakiwa.

Wajibu maombi katika shauri hilo la marejeo ni TLS, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Wengine ni mawakili Godfrey Wasonga, Meshack Ngamando, Boniventura Njeru na Sadick Omary wanaowawakilisha washtakiwa katika kesi ya jina inayomuhusu binti mkazi wa Dovya.

Wamo pia, washtakiwa wa kesi hiyo ambao ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Wakili wa kujitegemea aliyeiwakilisha TLS, Ezekiel Mwakabeje amesema shauri hilo limetajwa; na Mahakama Kuu imewapa muda wajibu maombi kupeleka kiapo kinzani au kama wana pingamizi katika shauri hilo.

Amesema wamepewa muda wa hadi Jumatatu Agosti 26, 2024 kabla ya saa 3.30 asubuhi wawe wamewasilisha viapo hivyo kwa ajili ya kuangalia kama ni lini shauri litasikilizwa.

Akizungumzia kesi ya jinai dhidi ya Nyundo na wenzake ambayo pia inasikilizwa faragha, Ngamando amesema haikuendelea baada ya kufunguliwa kwa shauri hilo la maombi ya marejeo.

Maelezo ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, yaliungwa mkono na Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude ambaye amesema kesi hiyo ilishindwa kuendelea kutokana na kufunguliwa kwa maombi hayo Mahakama Kuu.

Related Posts