Wana Azaki kujadili uchaguzi Serikali za Mitaa, Uchaguzi Mkuu

Dar es Salaam. Washiriki zaidi ya 500 wanatarajiwa kuujadili uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 katika maadhimisho ya sita ya Asasi za Kiraia yanayotarajiwa kufanyika jijini Arusha Septemba 9 hadi 13, 2024.

Pia, washiriki hao wakiwemo wadau wakuu wa maendeleo wa asasi za kiraia pamoja na sekta binafsi, wataangalia na kuchambua dira nzima ya maendeleo Taifa ya mwaka 2050.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society (FCS), Justice Rutenge leo Agosti 23, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Rutenge amesema katika maadhimisho ya mwaka huu moja kati ya mambo yatakayoangaziwa ni pamoja na uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanywa 2025.

Amesema kutokana na mambo hayo muhimu ya kitaifa ambayo yanatarajiwa kufanyika siku za usoni kaulimbiu itakayoongoza maadhimisho ya mwaka huu itakuwa ni sauti, dira.

Anasema katika kipindi hicho ni muhimu sauti ya mwananchi kusikika hivyo hivyo wao kama Asasi wameamua kuchukua sauti za umma kwa lengo la kufikisha maoni yao kwa Serikali ambao ndio watekelezaji wakuu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi wa Civil International, Nesia Mahenge kuwa wiki hiyo inaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha ushirikishwaji bora na watendaji kutoka sekta mbalimbali hapa nchini.

“Tukio hili ni muhimu kwa wadau wa maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla, katika kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi, Serikali na wananchi,” amesema.

Related Posts