Dar es Salaam. Wazazi na walezi kutowajibika ipasavyo kwenye makuzi ya watoto kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu za wao kukosa misingi mizuri ya ustawi na kusababisha kushamiri vitendo vya ukatili katika jamii.
Mengine yametajwa kuwa ni kufanya matendo yasiyo na staha mbele ya watoto, ukali kupitiliza, kukosa elimu na kutotenga muda wa kuzungumza na watoto.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 23, 2024 na Mratibu wa Mafunzo Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Dk Christina Onyango katika semina iliyolenga kuwajengea uwezo askari wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Ilala kuelekea utekelezaji wa kampeni ya ‘Tuwaambie kabla hawajaharibikiwa’.
Kampeni hiyo imelenga kuwajengea uelewa wanafunzi kutoka msingi hadi chuo kikuu kuhusu masuala ya ukatili.
Dk Onyango amesema baadhi ya wazazi au walezi kwa kujua au kutojua wamekuwa wakifanya matendo yasiyo na maadili mbele ya watoto jambo linalochochea mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Ametoa mfano zinapotokea sherehe za kijamii kama vile harusi baadhi ya watu hasa wanawake hucheza kwa namna isiyo na staha kwenye madirisha ya magari huku watoto wakiwa wanashuhudia.
“Wakiendelea kucheza wengine hufikia hatua ya kuvua nguo, huu nao ni ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto. Wazazi tunapaswa kujitafakari,” amesema.
Amesema matendo ya namna hiyo hayana afya kwa ustawi wa mtoto, hivyo ni vyema wazazi kujitafakari kabla ya kutenda jambo hasa wanapokuwa karibu na watoto.
Amesema ukali kupitiliza kwa watoto huwafanya kuwa waoga hata kueleza changamoto wanazopitia.
Anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiona fahari kuogopwa na watoto kiasi cha kwamba anapoingia nyumbani watoto wanajificha.
“Wazazi wengi tumekuwa tukipata muda wa kuzungumza na watoto wetu huwa tunajikita zaidi kuangalia anaendeleaje katika upande wa taaluma, lakini tunajua ni changamoto zipi wanapitia? Tujitafakari,” amesema.
Amesema baadhi ya wazazi au walezi hawatengi muda wa kufuatilia mambo yanayohusu mtoto ikiwemo kujua anacheza wapi na nani.
Pia kufuatilia mambo anayoangalia kwenye a televisheni, mitandao ya kijamii na maeneo mengineyo.
“Kutoweka umakini katika hili kumefanya baadhi ya watoto kujikuta ni waathirika wa ukatili ukiwemo ule wa mitandaoni,” amesema.
Dk Onyango amesema ili kutokomeza vitendo vya kikatili na vile vya mmomonyoko wa maadili elimu inatakiwa kutolewa kwa watu wote katika jamii kuhusu masuala ya ukatili, chanzo na kinachopaswa kufanyika kuutokomeza.
“Kila mmoja katika nafasi yake ajue majukumu yake na aweze kuyatekeleza kwa ukamilifu, hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutokomeza vitendo hivyo,” anasema.
Akizungumza kampeni hiyo Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Gloria Urassa amesema inatarajiwa kufanyika kuanzia mwishoni mwa Agosti hadi Februali 2025.
Amesema imelenga kuongeza uelewa wa wanajamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia na itatolewa kwa wazazi, walezi, wanafunzi kutoka ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu.