Samia aagiza huduma zirejeshwe Ngorongoro

Ngorongoro. Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kurejeshwa huduma za kijamii, kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na kuondolewa vikwazo vyote vilivyowekwa kwa wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro, ambao kwa siku tano wamekusanyika maeneo tofauti wakidai kupatiwa haki hizo.

Miongoni mwa madai ya wananchi hao ambao awali waliandamana ni kupinga kufutwa vitongoji 96, vijiji 25 na kata 11, amri ambayo kimsingi ilikuwa ikiwakosesha haki ya kupiga kura.

Madai mengine ni kuhusu huduma za elimu, afya na maji, pamoja na kuondolewa vikwazo vya kuingia na kutoka eneo hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi ameeleza hayo leo Agosti 23 alipozungumza na wananchi wa kata 11, katika eneo la Oloirobi lililopo Kata ya Ngorongoro. Wananchi hao wapo eneo hilo tangu Agosti 18, 2024.

Lukuvi aliambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Awadh Juma Haji.

Amesema wametumwa na Rais Samia kuzungumza nao na kutoa maagizo hayo ambayo ameelekeza mamlaka zote kuanzia mkuu wa mkoa hadi wilaya kuhakikisha yanatekelezwa.

Mbali ya hayo, Lukuvi amesema Rais amepanga kukutana na wawakilishi wa wananchi hao na kuwa utaratibu wa kukutana nao utaandaliwa ili wakawasilishe kero zao mbele yake.

Amesema Rais ana taarifa kuwa wananchi hao hawapati baadhi ya huduma zikiwamo za kuharibika kwa miundombinu kama vyoo vya shule, hali inayosababisha wanafunzi kujisaidia vichakani.

“Mkurugenzi wa Ngorongoro hawa wananchi wanapata huduma kwenye mamlaka hii lakini ziko baadhi ya huduma hazitolewi vizuri… baadhi ya shule vyoo vyake vimeharibika lakini ninyi hamshughulikii, kuna baadhi ya shule maji hayatoki, kuna shule zimeharibika lakini hamtengenezi,” amesema Lukuvi.

Amesema kuna viongozi ambao wanapata tabu kupita kwenye mageti, wakiwamo wenye magari binafsi ambao huzuiwa baada ya saa 10.30 jioni.

Kutokana na hilo, ametoa maelekezo wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro kuhakikisha usumbufu huo unaondolewa.

“Huduma za wanafunzi zitolewe kikamilifu, huduma hospitalini lazima zitolewe kikamilifu. Nataka Makonda uhakikishe kule kote ambako huduma zimesitishwa zirejeshwe ili wananchi hawa wasipate shida kupata huduma za kijamii,” amesema.

“Tunazo habari kuna baadhi ya wanafunzi wanajisaidia vichakani, kule shule ya sekondari ya wasichana kuna mashine imeharibika wanafunzi wanakwenda kilomita kadhaa kufuata maji kwenye kisima, nakupa siku saba ile mashine itengenezwe,” ameagiza.

Pia ametoa mwezi mmoja kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha hakuna vyoo kwenye shule yoyote ambavyo vimejaa.


Lukuvi afunguka ujumbe alioagizwa na Rais Samia Ngorongoro

Lukuvi amesema Rais amesikiliza na kusoma mabango yote waliyonayo wananchi hao na kuwa, alipata salamu kutoka kwa viongozi wao na kuwa jitihada zingine alizofanya ni kumtuma Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Arusha kuzungumza na wawakilishi wao.

Amesema Rais ametaka awahakikishe jamii ya Ngorongoro, kwamba pamoja na kwamba mahakama imetoa uamuzi jana (Agosti 22) wa kuzuia GN, yeye kama msimamizi wa Katiba na utawala bora, wakati uamuzi unatolewa alishawatuma na kuwa uamuzi huo umeimarisha nia ya Rais.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imezuia tamko la Serikali namba  673 la Agosti 2, 2024 la kufuta kata, vijiji na vitongoji, vikiwamo vya wilayani Ngorongoro, hadi amri ya Mahakama itakavyoelekeza vinginevyo.

Uamuzi huo ulitolewa Agosti 22 na Jaji Ayoub Mwenda, aliyesikiliza maombi madogo ya zuio hilo yaliyowasilishwa na mmoja wa wananchi wa Ngorongoro, Isaya Ole Posi, kupitia wakili Peter Njau.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mwenda aliridhia maombi hayo madogo na kukubali zuio la kusimama tamko hilo kupisha usikilizaji wa maombi ya msingi.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Arusha, wakili Njau amesema katika maombi hayo madogo namba 6953 ya mwaka 2024, wameyawasilisha mahakamani jana, kusikilizwa na kutolewa uamuzi huo.

Alisema maombi hayo madogo yalikuwa na hoja mbili, ya kwanza ni kuomba zuio hilo na ya pili ambayo ni kuu katika shauri hilo ni kuiomba mahakama itoe kibali cha mleta maombi  kufungua maombi ya marejeo ya amri hiyo kama ilikuwa halali au laa.

“Jaji ameridhia maombi yetu na ametuamuru tuwape nakala za maombi yetu upande wa Jamhuri (mjibu maombi) kwa hiyo amri ile ya tangazo la Serikali itasimama ili kupisha maombi mama kama amri ile ilikuwa halali au la,” alisema.

“Mteja wangu na wengine ambao ni wakazi wa Ngorongoro wanahisi aliyetoa amri ile hakuwa na mamlaka stahiki kuitoa na haikutolewa kihalali, hivyo kwenye maombi ya msingi mahakama itatazama hilo,” alisema.

Jaji Mwenda aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 26, 2024 mahakama itakaposikiliza maombi ya msingi ya Ole Posi.

Agosti 2, mwaka huu lilitolewa tangazo la Serikali chini ya kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za wilaya, likitoa tamko la kufuta vijiji, kata na vitongoji kutoka wilaya za Ngorongoro, Bahi, Chemba, Kasulu, Kakonko, Hai na Rombo.

Lukuvi alisema Rais Samia ameagiza shughuli za uchaguzi wa serikali za mitaa zinazoendeleaa maeneo mbalimbali nchini zifanyike Ngorongoro na maandalizi yafanyike bila hitilafu yoyote.

“Rais ametutuma tuje tuwasilishe kwamba, haki yenu ya kupiga kura katika uchaguzi huu uko palepale. Mkurugenzi ambaye ndiye anasimamia uchaguzi vituo vyote vilivyopangwa kwa maelekezo ya Rais vifunguliwe na vifanye kazi yake,” amesema

Amesema ili uchaguzi ufanyike ni lazima mipaka ijulikane na kuelekeza mamlaka zinazosimamia uchaguzi kuheshimu mipaka yote ya vijiji, vitongoji na kata iliyokuwepo awali.

“Kuna kata 11 hapa mbunge simamia kila diwani aende kwenye kata yake asimamie ujumbe na kueleza wananchi hakuna aliyezuiwa haki ya kupiga kura,” amesisitiza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ngorongoro, Murtallah Mbillu akizungumza na Mwananchi jana alisema maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 yanaendelea kama kawaida.

Mbillu alisema: “Baada ya zuio hilo, mimi kama mkurugenzi nimeanza kutekeleza yale yanayotekelezwa na wizara za kisekta, kwa sababu Mahakama imeamua na kusitisha.

“Mimi kama mkurugenzi wa Ngorongoro taratibu zingine kama maandalizi ya uchaguzi na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, zinaendelea kama kawaida.”

Kwa upande wake, Profesa Kabudi, amesema Watanzania wote wako sawa, akiwahakikishia wananchi hao watapata haki sawa na wa maeneo mengine.

“Nchi yetu imejengwa  kuwa Taifa moja, lenye upendo, amani na umoja, Rais Samia anasimamia misingi hiyo. Anaomba muwe na amani, utulivu na tutunze nchi yetu. Tuwe watu wa amani na upendo kama Watanzania wote,” amesema.


Profesa Kabudi atuliza wananchi Ngorongoro

“Ibara ya 8 ya Katiba yetu inasema wazi kabisa  mamlaka yote ya Serikali yanatoka kwa wananchi, na wananchi ndiyo ninyi mliokusanyika hapa. Ninyi ni wananchi wa Tanzania na ni sehemu ya wale wananchi wanaoleta mamlaka ya nchi. Katiba yetu inasema kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha inakuza ustawi wa wananchi,” aliongeza.

Waziri Kabudi alisema ibara hiyo inataka wananchi wapate haki za kushiriki shughuli za nchi yao na kuwa Rais amekuwa na falsafa ya R nne, ikiwemo maridhiano, hivyo amewaomba wananchi hao kuendelea kutunza amani na kuwa wavumilivu.

“Rais anasimamia utawala wa sheria, Serikali lazima isimamie utawala wa sheria ndiyo maana imepokea maamuzi ya Mahakama ya kusimamisha agizo lile,” amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema moja ya sifa yake ni kusimamia haki na ukweli, na amekula kiapo kuwa atakapokuwepo kwenye nafasi yoyote, hatashiriki kukandamiza haki za mtu na kuwa nafasi wanazopata ni za upendeleo wa Mungu.

“Rais naye anapenda haki ndiyo maana sikuwahi kuja huku Ngorongoro niliposikia kelele sipendi kwenda mahala bila majibu, hunibebi kama hakuna majibu na majibu yenyewe lazima yawe ya kweli kwa sababu nitadaiwa mbele ya Rais na Mungu,” amesema.

“Nisingependa niende mbele ya Mungu nikumbushwe habari ya Ngorongoro nilihusika kutenda udhalimu na kuumiza wananchi hilo sitakubali,” amesema.

“Ninayo matumaini makubwa yale yatakayosemwa mimi kwa mamlaka yangu iwe kwenye kijiji, kata au tarafa au wilaya au ngazi ya mkoa yoyote atakayechelewesha utekelezaji nitapiga nyundo,” amesema.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi hao, Mbunge wa Ngorongoro, Emanuel Ole Shangai amesema kwa kipindi cha miaka minne  hawajawahi kuona viongozi na leo Rais amewapeleka.

“Niwaombe muwe na imani kwa sababu Rais ni wa Watanzania wote na inawezekana kuna watu wake walio chini walimdanganya ndiyo maana yakatokea yaliyotokea,” amesema.

Related Posts