Mwanza. Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Tawi la Mwanza, kilichopo Kisesa wilayani Magu, Elias Mbise (20) amekamatwa akidaiwa kusambaza taarifa za uchochezi mitandaoni na kuhamasisha wenzake kuwafanyia vurugu askari wa Jeshi la Polisi na watumishi wengine wa umma.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kusambaza taarifa hizo katika kundi sogozi (WhatsApp) akiwashawishi watu mbalimbali katika kundi lake waungane, wanunue vibiriti na mafuta ya petroli ili kuwashambulia askari na kuharibu mali za umma.
Akitoa taarifa ya tukio hilo leo Agosti 23, 2024 mbele ya waandishi wa habari jijini Mwanza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo, mkazi wa Wita, Kata ya Kisesa wilayani Magu, alikamatwa Agosti 13, 2024, saa 3 usiku.
Amesema jeshi hilo ambalo moja ya majukumu yake ni kufanya doria kwenye mitandao, lilinasa jumbe zilizokuwa zikisambazwa na mtuhumiwa huyo, likafungua jalada la uchunguzi kumfuatilia na kumnasa ambapo anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Yeye anasema vijana wamechoka, hivyo anawahimiza wajitokeze na kuwa na mawazo chanya katika kupigania haki zao, uhamasishaji anaosema wajitokeze wakiwa na vibiriti na mafuta ya petroli kwa lengo la kuwashambulia askari ambao wataonekana wakiwa na sare.
“Na kwa tukio hili, niwaombe watu wote kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii kuliko kutengeneza meseji na kuzisambaza ambazo zinaweza kusababisha uchochezi au uvunjifu wa amani na Jeshi la Polisi tuko makini sana katika kuwafikia hao ili wachukuliwe hatua,” amesema Mutafungwa.
Katika tukio lingine, jeshi hilo linamshikilia Jackson Magoti (34), mkazi wa Michese Tanesco mkoani Dodoma kwa tuhuma za mauaji ya mfanyakazi wa nyumbani, Sainethi Kakululu (20) mkazi wa mtaa wa Ipuli, Mahina jijini Mwanza.
Mutafungwa amesema mtuhumiwa huyo alitiwa mbaroni Agosti 16, 2024 saa 5:30 asubuhi jijini Dodoma baada ya kufuatiliwa kwa muda mrefu kufuatia mauaji aliyoyatekeleza Agosti 5, 2024 saa 11:30 jioni nyumbani kwa Jackline Ngowi ambapo alimuua mfanyakazi huyo kwa kumkaba shingo.
“Mtuhumiwa alifanya hivyo ili kutimiza azma yake ya kuiba mali zilizokuwa ndani ya nyumba ya Jackline Ngowi, mtuhumiwa aliwahi kuajiriwa katika nyumba hiyo kama msimamizi wa bustani kwa hiyo alikuwa amezoea hayo mazingira.
“Baada ya tukio hilo la mauaji na kufanikiwa kuchukua baadhi ya vitu humo ndani, alitoweka kabla ya kukamatwa na askari wetu kule Dodoma. Baada ya kumkamata tumemkuta na vielelezo alivyopora vikiwemo simu, viatu na baadhi ya nguo za marehemu,” amesema Mutafungwa.
Kufuatia matukio hayo, kamanda huyo amewataka wananchi wa Mkoa wa Mwanza kutoa taarifa za waalifu na uhalifu haraka ili jeshi hilo lichukue hatua mara moja, huku wakiendelea kufanya msako katika visiwa, mialo na Ziwa Viktoria kwa ajili ya kudhibiti uhalifu wa ziwani.