Michango ya figo isigeuzwe biashara ya figo

Dar es Salaam, Kuna hadithi ya Warusi inayosimulia kisa cha kaka mjivuni aliyemtoboa macho mdogo wake aliyekuwa masikini. Walianza kwa mabishano ni kipi bora kati ya wema na uovu. Mjivuni akasema uovu ndiyo dili, na yule masikini akabisha na kusema wema ndiyo kila kitu.

Wakabeti kwamba atakayeshindwa anyang’anywe mali zake, lakini kwa kuwa masikini hakuwa na mali akakubali kuwa mkeka wake ukichanika basi atakuwa mtumwa wa kakaye.

Wakapanga kuwauliza wadau watatu ili kupata suluhu ya ubishi wao. Mfanyakazi wa ofisini akasema “Ah wapi! mimi nakaribia kustaafu baada ya kumaliza ujana wangu wote kazini.

Hapa nina tuzo tatu za Mfanyakazi Bora lakini sina hata kibanda cha nyasi. Wenzangu wezi wamefukuzwa lakini wana maghorofa. Kila nikipiga hesabu za vikokotoo naona kiza… hakyanani sitoboi mwaka huu!”. Kaka mjivuni akampa mdogo wake cheko la jino pembe.

Wakaachana naye na kuingia kwenye ajira ya sekta binafsi. Mfanyabiashara akasema “Nyie mnaongea nini? Kwa miaka thelathini sasa nafanya biashara halali.

Ebu niangalie namiliki risiti tu, lakini tazama wale wauza ngada wa juzi tu hapa wanavyonipigia misele na mandinga yao. Wema kitu gani bwana!” Mpaka hapo bwana mdogo alikuwa keshakosa penati mbili kati ya tatu. Akabwaga manyanga na kukabidhi ushindi.

Ngoma haikuishia hapo. Kama ujuavyo mtumwa hana mshahara, hivyo baada ya masikini yule kunyang’anywa kila kitu njaa ikamgonga. Akarudi kwa mjivuni na kumwomba angalau kibaba cha unga watoto wakale. Mkubwa akamwambia:

“Hapa ni ubaya ubwela… lete jicho nikupe gunia zima!” dogo akakubali kupoteza macho, meno na viungo vingine vya mwili kwa mabadilishano ya chakula na huduma zingine.

Hadithi iliendelea hadi huko mwishoni ambapo wema ulikuja kujidhihirisha kuwa bora kuliko uovu. Ilitokea miujiza ya kumporomosha mjivuni na kumkweza yule dogo kwani alikuwa sahihi. Miujiza hiyo iliweza kumrudisha dogo kuwa zaidi ya vile alivyokuwa hapo awali.

Utamu wa hadithi ni kumalizika kwa utamu, lakini sisi kwenye stori yetu tuondoke na jambo letu. Hayo mengine tutamalizia panapo majaliwa.

Hakuna jambo baya kama njaa. Unaweza kukataa na kusema ugonjwa ndiyo mbaya zaidi, lakini mgonjwa anasitiriwa aibu yake kwani hayo ni maumbile ya kibinadamu.

Hata matajiri huumwa, lakini hakuna mtu yeyote aliyeumbwa kuishi na njaa. Muumbaji aliwatayarishia chakula viumbe wake wote kwa namna yao, hata funza hupata maisha pale panapotokea uozo.

Hivyo njaa huwa ni jambo la aibu linaloashiria uvivu na kutojitambua.

Usemi wa “Adui yako mwombee njaa” unaakisi ukweli kwamba hata uwe shujaa wa aina gani, ukiwa na njaa unakuwa bwege tu.

Ukiitafsiri njaa kuwa umasikini utamwona vema mfanyakazi anayeulalamikia wema, mfanyabiashara mwaminifu aliyebaki kuwa kapuku na mwisho ndugu yetu aliyeuza macho kwa sababu ya magunia ya unga. Ulifika wakati ndugu yetu huyu aliona chakula kina thamani zaidi ya viungo vyake vya mwili. Hiyo ndiyo njaa.

Huko mitaani unaona watu wakipora simu na bodaboda, akinadada wakiuza miili yao, watoto wakicheza kamari na uchafu mwingine wa kujidhalilisha kwa sababu ya njaa.

Kadhalika watu wanashiriki ukatili wa kukata viungo vya miili ya wenzao kwa sababu hiyohiyo. Wengine wanabaka watoto baada ya kudanganywa kuwa wangetoboa kimaisha.  

Hivi karibuni Watanzania tumeingia kwenye ukurasa mwingine baada ya wataalamu wetu kwa ushirikiano na wataalamu wenzao wa nje kufanikiwa kupandikiza viungo vya mwili.

Zamani tuliposikia wazungu wakipandikiza mioyo na figo, tuliwasonya na kusema hiyo ni kufuru kwa Mwenyezi Mungu. Lakini kumbe kasoro ya ngoma utaiona ukiisikia kwa mbali. Hivi sasa tumeshaingia kuicheza tunashangilia kila mdundo.

Potelea mbali iwe kufuru au baraka. Lakini yale tuliyohisi yangeweza kuwatokea wenzetu ndiyo yanayoweza kututokea sisi tusipokuwa makini. Wahuni wapo kila kona kuanzia majumbani, mitaani, mahospitalini na hata makanisani. Kama baba anaweza kumnajisi bintiye au kumuua na kumkata viungo, na daktari anaiba damu inayochangiwa kwa wahitaji basi hatuko salama.

Nakumbuka kipindi kile mtu aliyechangia damu alichagua chungwa au bia baada ya kufanya hivyo. Tulishangaa idadi ya watu waliojitokeza. Baadaye iligundulika kuwa wengi walivutiwa na kile kishushio cha bia baada ya kutoa damu. Sasa kwa jinsi Watanzania walivyojikatia tamaa, kama mtawapa bakshishi yoyote baada ya kuchangia tutegemee uchangiaji kuvuka malengo baada ya muda mfupi sana. 

Lakini hatari kubwa ni kuzuka kwa biashara haramu ya viungo kama ini, moyo na figo. Hapa wimbi la utekaji watoto litaongezeka maradufu na kama nilivyosema wahuni wapo hadi mahospitalini. Hivyo hata kama kutakuwepo na masharti thabiti ya uchangiaji, wahuni wanaweza kuyafanya mambo yakawa mepesi na biashara haramu ikachukua mkondo.

Wasiwasi ndiyo akili ukiona madalali wa viungo vya mwili wanaanza kuibuka ujue huo ndiyo mwanzo wa mwisho. Lugha ya “Una vyumba vingapi” itabadilika kuwa “una figo ngapi?” halafu utashangazwa na jibu la dalali: “Ninazo sita”!!! Kuna mtu mwenye figo sita?

Related Posts