KAMA wewe ni shabiki wa soka, kaa tu sebuleni ukiwa na rimoti mkononi. Ndio, leo tena ni wikiendi ya bandika bandua ya kupata burudani ya soka. Kwa wale watakaotimba vibanda umiza, waage mapema kabisa kwa wenza wao ili wasilete utata.
Unajua kwanini? Kuanzia saa 8:30 mchana kuna ngoma moja ya Ligi Kuu ya England (EPL), inapigwa kati ya wenyeji Brighton dhidi ya Manchester United. Ikiisha mechi hiyo saa 11:00 zinapigwa nyingine tano za ligi hiyo maarufu, na zikiisha hizo tu, itabidi ubonyeze tena rimoti kuhamia kwenye mechi za CAF.
Ndio, kama hujui ni kwamba leo zinapigwa mechi kibao za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, lakini nne kati ya hizo zitaziwahusu wawakilishi wa Tanzania, Yanga, Azam, JKU na Uhamiaji kabla ya kesho Coastal Union kufunga hesabu, kujua ni timu zipi zitatinga raundi inayofuata kuungana na Simba.
Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho kwa msimu huu, imeanzia raundi ya pili ya michuano hiyo na inasubiri mshindi kati ya Al Ahli Tripoli na Uhamiaji ambazo zitarudiana usiku wa leo baada ya wiki iliyopita Walibya kushinda kwa mabao 2-0, ikicheza ugenini dhidi ya maafande hao wa Zanzibar.
Kati ya wawakilishi hao wanne wanashuka uwanjani leo, ni Yanga pekee ndio watakuwa nyumbani, lakini timu zilizosalia zote zitakuwa ugenini ikiwamo Azam FC itakayokuwa Kigali, Rwanda kurudiana na APR iliyowachapa kwa bao 1-0 wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Yanga yenyewe itarudiana na Vital’O ya Burundi iliyokubali kichapo cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam, ikiwa kama wenyeji na leo itakuwa na kazi ngumu kuwazuia mabingwa hao wa Tanzania wasiende raundi inayofuata, huku JKU iliyopigwa mabao 6-0 ns Pyramids itakuwa jijini Cairo kujitetea.
Yanga iliyoonyesha mziki mkubwa mbele ya Vital’O baada ya kutawala na kushinda vizuri licha ya matokeo hayo imejipanga kuhakikisha inaingia kwa kutafuta matokeo mengine bora wakati itakaposhuka Uwanja wa Azam kuanzia saa 1:00 usiku, mechi ya Ligi ya Mabingwa itakayoenda sambamba na ile ya Azam kule Kigali.
Kipigo ilichoishushia Vital’O, kimekuwa ni cha pili kwa ukubwa katika michuano hiyo ya Mabingwa baada ya kile ilichopewa JKU na Pyramids, japo katika Kombe la Shirikisho kuna mtu kapigwa 7-0 pale wenyeji Alize Fort ya Comoros ilipocharazwa nyumbani bao hizo na Black Bulls ya Msumbiji.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema bdo hajariodhika na kwamba amepanga anashusha kikosi kizito kitakachokwenda kutengeneza ushindi mwingine utakaoandikisha pengine rekodi mpya ya CAF.
Gamondi alisema bado Yanga haijafuzu licha ya kushinda vizuri katika mechi ya kwanza ambapo anaamini wapinzani wao watakuja tofauti kwenye mechi ya pili ya marudiano.
“Nilisema mara baada ya mechi ya kwanza kumalizika, bado hatujafuzu, kuna dakika 90 zingine ngumu zijazo, tumewaona wapinzani wetu na wao wametuona kila mmoja ataingia na hesabu tofauti,” alisema Gamondi na kuongeza;
“Tutakuwa na kikosi chetu kamili ambacho tunaamini kitakwenda kutupa tiketi ya kwenda kucheza hatua inayofuata kwa kupata ushindi, tunawaheshimu Vital’O ni timu inayoundwa na wachezaji vijana wenye vipaji vikubwa wanakosa uzoefu tu wa kutosha.”
Yanga hadi sasa ndio iliyofunga mabao mengi katika mechi za kimataifa kwa msimu huu kwa timu za Tanzania, kwani ilishinda 4-0 huku Azam ikishinda 1-0 na kila moja kuvuna fedha za ‘bao la mama’.
Ushindi huo uliipa Yanga Sh 20 milioni kutoka ile ahadi ya Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan aliyeziahidi timu zote kulipa kila bao moja katika mechi ya ushindi sh 5 milioni.
Wachezaji wa Yanga wamajipanga kusaka ushindi mkubwa zaidi kwenye mchezo wa leo ili kujikusanyia mamilioni hayo ambayo yanatoka nje ya bonasi ya klabu hiyo, kam,a itakavyokuwa kwa Azam iliyovuna Sh 5 Milioni kwa kuichapa APR inayorudiana nao kwenye Uwanja wa Amahoro, jijini Kigali.
Mchezo huo wa Yanga utaamuliwa na waamuzi kutoka Gambia, ambapo mwamuzi wa kati atakuwa Lamin Jamweh, akisaidiwa na Abdul Jawo na Nfally Jarju huku mwamuzi wa akiba akiwa Boubaccar Alhasan.
Lamin hii itakuwa mechi ya nne ya Ligi ya Mabingwa kuchezesha ambapo takwimu zinaonyesha ni mchezo mmoja tu kati ya tatu ambazo aliziongoza kuamua huku timu ya nyumbani ikakosa ushindi, kwenye mechi ya sare ya bila mabao kati ya Espérance Sportive de Tunis dhidi ya Asec Mimosas huku zingine wakishinda.
Yanga ni kama watakutana na mwamuzi huyo baridi aliyezaliwa miaka 35 iliyopita ambaye pia hana rekodi ya kuwa mtoaji wa kadi nyekundu mara kwa mara katika mechi zake akiwa na kadi nyekundu moja pekee.
Vital’O wao wanajua kwamba mziki wa Yanga ni mkubwa kwao lakini wamejipanga sawasawa kukomaa kuhakikisha wanafanya kitu tofauti. Wachezaji wa Vital’O juzi walijifungia na kocha wao kabla ya kwenda mazoezini wakijipanga kwa mikakati ya kuwazuia wenyeji wao hao.
Kocha wao Parris Sahabo ameweka wazi kuwa wala hawatakwenda na mpango wa kujilinda kuizuia Yanga na kwamba watakwenda na hesabu za kuwa makini kwenye kuta lakini pia kutafuta bao la mapema na mengie ya ushindi.
“Hata tukisema tutajilinda haitakuwa na faida kwetu, sisi mpango wetu ni kuhakikisha hatuongezi ugumu kwa kuruhusu Yanga kupata mabao, tutakuwa makini kwenye ulinzi lakini tutakuwa na akili ya kutafuta mabao,”alisema Parris. “Tunakubaliana na ubora wa Yanga ina wachezaji wakomavu kuliko vijana wetu lakini hii ni nafasi ya kuwashangaza watu kwa kufanya kitu tofauti na kufungua milango ya kujulikana na kujiuza.