Kasoro kibali cha DPP zairudisha kesi ya ugaidi kortini

Songea. Mahakama ya Rufani imeamuru kusikilizwa upya kesi ya ugaidi inayowakabili washitakiwa sita baada ya kubainika kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hakikuwa kimeidhinishwa awali na mahakama.

Desemba 16, 2022 Jaji Yose Mlyambina wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, aliwahukumu kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kwanza na miaka 30 kwa kosa la pili, wakawa wanatumikia miaka 30 kwa kuwa vifungo vilitumikiwa pamoja.

Hata hivyo, hawakuridhika na hukumu wakakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania, ambayo katika hukumu iliyotolewa Agosti 22, 2024 imeamriwa jalada la kesi hiyo lirejeshwe Mahakama Kuu kesi isikilizwe upya.

Warufani hao ni Seif Chombo maarufu Baba Fatina na mwanaye Abdallah Chombo, na Athman Chombo ambaye ni ndugu. Wengine ni Mohamed Kamala, Omary Mbonani na Rashid Ally.

Upande wa mashitaka ulidai kati ya Januari 1, 2014 na Julai 13, 2020 katika Kijiji cha Lukumbule na maeneo mbalimbali nchini Tanzania, washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa la ugaidi na walishiriki vikao vya kupanga ugaidi.

Katika kipindi hicho katika maeneo ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma na maeneo mbalimbali ya Tanzania, washitakiwa wanadaiwa kwa pamoja walikula njama ya kuanzisha harakati ya kuiondoa Serikali halali ya Tanzania.

Ilidaiwa lengo lilikuwa kuindoa Serikali halali ya kidemokrasia ya Tanzania na kuweka kile walichokiita katika maelezo yao ya onyo ya kukiri makosa hayo yaliyopokewa kortini kama kielelezo, Dola ya Kiislamu Tanzania.

Katika utetezi wao, licha ya kukubali kuwa wote wanafahamiana kwa vile ni wakazi wa Kijiji cha Lukumbule, warufani walikana kufanya makosa waliyotuhumiwa nayo na wala hawakuwahi kushiriki mafunzo ya ugaidi.

Mrufani wa kwanza, Seif Chombo, ingawa alikiri kuwa alikuwa akisali katika Msikiti wa Masjid Al-Malid, alikanusha kujihusisha na mazoezi ndani ya msikiti huo wala hakuwahi kusafiri kwenda Msumbiji kwa ajili ya vita ya Jihad.

Warufani wengine licha ya kukiri walikuwa wanaswali msikiti mmoja na Chombo, walikanusha kufanya mazoezi yoyote ndani ya msikiti huo, huku baadhi wakikana kuandika maelezo ya kukiri kutenda makosa isipokuwa walitaja majina yao tu.

Baada ya kuhukumiwa kifungo, warufani wakiwakilishwa na jopo la mawakili sita Kitara Mugwe, Eliseus Ndunguru (the Junior, Edson Mbogoro, Hillary Ndumbaru, Frank Kapinga na Dickson (the senior) walikata rufaa.

Warufani waliegemea sababu kuu nne za rufaa, ya kwanza ilitosha kushawishi jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, Rehema Kerefu na Omar Makungu, kubatilisha mwenendo na hukumu ya kesi hiyo.

Sababu hiyo ni kuwa jaji aliyesikiliza kesi hiyo, alikosea katika sheria na ukweli kwa kusikiliza kesi hiyo na kuwatia hatiani warufani kinyume cha matakwa ya sheria.

Akijenga hoja ya sababu hizo, wakili Ndunguru Junior alisema mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa kile kilichodaiwa kuwa ni kibali cha DPP cha Juni 7, 2022 hakikuwa kimeidhinishwa na mahakama.

Alieleza alipopewa kumbukumbu za mahakama na kuzipitia kujiridhisha kama nyaraka hizo zimetolewa na DPP, alibaini hazikuwapo mahali popote kwenye mwenendo wa shauri hilo na wala hazikuwa sehemu ya kumbukumbu za rufaa.

Majaji walisema wakili alifanya jitihada za kupitia jalada halisi la kesi hiyo na bado nyaraka hizo hazikuwamo, lakini siku chache baadaye kabla ya rufaa kusikilizwa, alijulishwa kuwa nyaraka hizo zimepatikana katika jalada la mahakama.

Alichokiona ni nyaraka hizo zilipigwa tu muhuri wa mahakama lakini hazikuwa zimeidhinishwa na kuthibitisha kuwa zilipokewa kwa utaratibu na mahakama iliyosikiliza shauri hilo na haieleweki ziliingiaje kwenye jalada la mahakama.

Akisisitiza kuhusu hoja hiyo, wakili huyo alinukuu kifungu cha 34(2) na 26(1) cha Sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa ambavyo vinasisitiza kuwa kibali cha DPP ni lazima kiidhinishwe na mahakama wakati wa usikilizwaji wa kesi.

Kutokana na dosari hizo, wakili huyo aliiomba mahakama kubatilisha mwenendo mzima wa shauri hilo, kufuta kutiwa hatiani kwa washitakiwa na adhabu, na washitakiwa wote waachiwe huru mara moja kutoka gerezani wanakoshikiliwa.

Katika rufaa hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na jopo la mawakili likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akisaidiwa na mawakili wenye cheo kama chake, Sabrina Joshi, Ofmedy Mtenga na Salim Msemo.

Wengine ni Valence Mayenga, Faraja George, Clara Charwe na Ignas Mwinuka ambao ni Mawakili Waandamizi wa Serikali.

Nchimbi aliijulisha mahakama kuwa wajibu maombi wanapinga rufaa hiyo ya warufani.

Kuhusu kibali cha DPP, wakili Joshi alikubali mapema kuwa ni kweli nyaraka hiyo haionekani katika mwenendo wa kesi hiyo lakini akasisitiza iliwasilisha kortini, ikapokewa na kuidhinishwa na Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa wakili huyo, hakuna tofauti kati ya kugongwa muhuri kwa nyaraka na kuiidhinisha nyaraka hiyo.

Alieleza kwa kuwa nyaraka hiyo ya DPP iligongwa muhuri wa mahakama, ni wazi kuwa iliidhinishwa na mahakama.

Katika hukumu ya rufaa hiyo, majaji walisema baada ya kusikiliza mabishano ya kisheria ya mawakili wa pande mbili, wameona hoja kuu ambayo mahakama inapaswa kuiamua ni kama kulikuwa na kibali cha DPP au la.

Majaji walisema hakuna ubishi kuwa mbele ya mahakama iliyosikiliza kesi hiyo, warufani kwa pamoja walishitakiwa kwa makosa mawili ambayo ni kosa la kula njama kutenda kosa la ugaidi, na kosa la pili ni kushiriki mikutano ya ugaidi.

Kulingana na kifungu cha 34(2) cha sheria ya uhujumu uchumi, kesi itasikilizwa tu baada ya DPP kutoa kibali na inasema hakuna mashitaka yatasikilizwa chini ya sheria hiyo, bali pale tu ambapo kutakuwapo na kibali hicho cha DPP.

Majaji hao walisema kwa maudhui ya kifungu hicho, ni wazi hakuna mtu atashitakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi na uhujumu uchumi bila kuwapo kwa kibali cha maandishi cha DPP kuruhusu usikilizwaji wake.

Wamesema katika kupitia kibali hicho, ingawa inaonyeshwa kwamba kilitolewa na DPP Juni 7, 2022 kumbukumbu za mahakama hazionyeshi kama kilipokewa na mahakama kwa kuwa hakikuidhinishwa licha ya kupigwa mhuri.

Wamesema wanatambua katika wasilisho, wakili Joshi alijenga hoja kuwa kupigwa mhuri kwa nyaraka kunaifanya iwe tayari imeidhinishwa na kusema wameshindwa kukubaliana naye kwa sababu mhuri unaweza kupigwa na yeyote.

Katika rufaa hiyo, majaji wamesema kwa kuwa kibali cha DPP hakikuidhinishwa na mahakama kuthibitisha kama kiliwasilishwa na kupokewa rasmi ili kukifanya sehemu ya kumbukumbu za mahakama, wanakubaliana na hoja za Ndunguru.

Kwa msingi huo, wakabatilisha mwenendo wote wa shauri hilo na kufuta amri ya kuwatia hatiani na adhabu waliyopewa warufani na ili kutenda haki na ionekane imetendeka wanaamuru kesi hiyo isikilizwe upya na kwa haraka.

Related Posts