WAKILI wa Mahakama Kuu, Tundu Lissu, ametaka ufuatiliaji wa haraka kwenye kesi iliyofunguliwa jijini Arusha na mwananchi mmoja, kupinga uhamisho wa wananchi wa Ngorongoro, mkoani Arusha.
Akiandikia mawakili wenzake kupitia mitandao ya kijami, Lissu ameeleza yafuatayo: Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).
Naomba kushauri yafuatayo kuhusu kesi iliyofunguliwa Arusha na masuala mengine muhimu:
- 1. Tupate nyaraka zote za shauri hilo ili tujadiliane mambo ya uhakika. Mawakili walioko Arusha wanaweza kutusaidia kwenye hili.
2. Nyaraka hizo zitatusaidia kujua sio tu nani aliyefungua kesi na wakili wake, bali pia tutajua hasa uamuzi wa Mahakama Kuu unasema nini.
3. Inawezekana kabisa serikali imeona kwamba uamuzi wa Waziri wa TAMISEMI umeongeza, badala ya kupunguza, hasira za wananchi wa Ngorongoro. Kujifungulia kesi na kushindwa mahakamani ni namna yao ya kurudi nyuma na kujipanga upya, sio kukubali yaishe.
4. Kama niko sahihi kwenye Na. 3, basi msimamo wa wananchi wa Ngorongoro uwe ni kuongeza moto wa mapambano kwa kuendelea na maandamano hadi madai yafuatayo yatimizwe:
(a) Rais Samia na serikali yake watoe tamko rasmi la kufuta uamuzi wa kuwahamisha wananchi wa Ngorongoro kutoka kwenye maeneo yao;
(b) Rais Samia na serikali warudishe fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya huduma za jamii zilizohamishiwa Wilaya ya Handeni;
(c) Rais Samia na serikali yake watoe tamko rasmi la kufuta amri ya Waziri wa TAMISEMI la kufuta Vijiji na Kata za Ngorongoro. Uamuzi wa Mahakama Kuu tunaousikia peke yake hautoshi na unaweza kukatiwa rufaa na serikali;
(d) Tume ya Uchaguzi ifute rasmi uamuzi wake wa kuwahamishia wapiga kura walioandikishwa Ngorongoro kwenda Msomera na Handeni kwa ujumla;
(e) Rais Samia na serikali yake waondoe vizingiti na vizuizi vyote kwa wananchi wa Ngorongoro kuingia na kutoka Ngorongoro kama raia huru, na kuondoa vizuizi vya kuingiza mahitaji muhimu kwa maisha yao;
(f) Rais Samia na serikali yake waondoe vizingiti na vizuizi vyote vilivyowekwa kwa mifugo ya wananchi kuingia katika maeneo muhimu ya malisho, maji au chumvi ndani na nje ya Kreta na maeneo mengine;
(g) Sheria ya Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro na sheria nyingine zinazohusika zifanyiwe marekebisho makubwa ili kuhakikisha ulinzi wa haki za ardhi na rasilmali za wananchi wa Ngorongoro. - Tunahitaji kuwa na ufahamu wa kila kinachoendelea na kujipanga ku-deal nacho. Kitu muhimu kuliko vyote ni kutambua kwamba mass action, maandamano ya wananchi wa Ngorongoro, ndiyo silaha wanayoiogopa zaidi.
Maandamano hayawezi kufichwa kirahisi kwa wageni wanaokwenda Ngorongoro na kwa jumuiya ya kimataifa. Maandamano yanavuruga mipango yote ya huyu mwanamke kudalalia rasilmali za wananchi wa Ngorongoro.
Kwa sababu ya umuhimu huu wa maandamano, ni muhimu yahamasishwe hadi hapo madai yote ya wananchi yatakapopatiwa usuluhishi wa kudumu.