Walinzi 50 wauawa Geita kwa nyakati tofauti

Geita. Walinzi 50 waliokuwa wakilinda maeneo mbalimbali mkoani Geita wamevamiwa na kuuawa wakiwa malindoni kati ya mwaka 2017-2024 hali iliyosababisha vijana wengi kuikimbia kazi ya ulinzi.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Kampuni Binafsi za Ulinzi Geita, Meshack Kasega, wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba kwenye uzinduzi wa Ofisi ya Kanda ya Ziwa ya Umoja wa Kampuni binafsi za Ulinzi Nchini (Ukuta).

Kasega amesema kati ya waliouawa 38 walitoka kwenye kampuni mbalimbali za ulinzi na 12 walikuwa walinzi binafsi.

Amesema kutokana na matukio hayo ya mauaji, vijana wamekuwa wakienda lindoni kwa shaka huku wengine wakiamua kuacha kazi kwa kuhofia kuuawa.

Katibu wa Ukuta Taifa, Rogers Raphael amesema changamoto nyingine ni kutopata vibali vya silaha kwa wakati hali inayofanya washindwe kuimarisha ulinzi na wakati mwingine kukimbiwa na wateja kwa kukosa silaha.

Akizindua ofisi hiyo, Komba amewataka wamiliki wa kampuni binafsi za ulinzi kuona umuhimu wa kuajiri watu waliopitia mafunzo ya awali ya kijeshi ili kuwa na wapiganaji imara na madhubuti watakaosaidia kuimarisha ulinzi na usalama.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mbali na kuimarisha ulinzi na kulinda raia na mali zao, kupitia mafunzo ya kijeshi waliyoyapata yatawawezesha kujilinda wenyewe na kuwataka wenye kampuni kuajiri  wanaopita kwenye mafunzo ya Jeshi la Akiba na JKT.

Komba amewatahadharisha pia kuacha kuajiri wazee wanaoshindwa kustahimili changamoto zinazotokea lindoni kutokana na umri.

“Jingine ni hili la umri wasaidieni wazee wetu, yapo malindo ambayo wanawekwa wazee ukiangalia huyu ndio anaenda kupambana na wahalifu unajiuliza utayari wake ukoje, mwili unamsaliti japo moyo unatamani kulinda niwaombe muone umuhimu wa kuzingatia umri mnapotoa askari wanaokwenda kulinda,” amesema Komba.

Aidha, amewataka kutumia umoja wao kuzisaidia kampuni zinazodhulumiwa na kuwataka waajiri wanaochukua walinzi kwenye kampuni kuhakikisha wanawalipa kwa wakati ili nao waweze kuwalipa vijana walio waajiri.

Related Posts