Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Tanzania, Mhe. Jean Pierre Massala amekutana na Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kufanya mazungumzo yenye lengo la kuboresha huduma za afya nchini humo.
Mazungumzo hayo yameangazia ushirikiano katika matibabu ya magonjwa ya damu, upasuaji wa watoto wenye jinsia tofauti, utafiti wa kisayansi na mifupa.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema ushirikiano huu ni muendelezo wa hatua ya awali ambapo wataalam wa afya kutoka MNH, JKCI na MOI walipata nafasi ya kutembelea nchini humo ili kujifunza na kuona mazingira ya utoaji huduma za afya.
“Ziara ya sasa ya Balozi inalenga kujifunza kutoka MNH na kutathimini namna ya kuleta wataalam kwa ajili ya kubadilishana ujuzi ambapo ushirikiano huu utaleta matokeo chanya katika kuboresha huduma za afya kwa nchi zote mbili na kuongeza kasi ya utalii tiba,” amesisitiza Prof. Janabi