Njombe. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeahidi kujenga kituo kidogo cha uwekezaji mkoani hapa ili kuwapunguzia safari wawekezaji na wafanyabiashara ya kufuata huduma hiyo ofisi za kanda zilizopo mkoani Mbeya.
Ahadi hiyo imetolewa leo Jumamosi Agosti 24, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuwa na wawekezaji wa ndani ambao wamewekeza mitaji mikubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Teri amesema kituo hicho kimefanikiwa kusajili miradi 61 mkoani Njombe na uwekezaji wake ni Sh12 trilioni huku ajira zilizozalishwa ikiwa ni zaidi ya 20,000.
Amesema kuwepo kwa uwekezaji huo ni matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ya kuweka mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji hapa nchini.
“Tumepokea maelekezo kutoka kwako juu ya kuwepo kwa kituo kidogo cha uwekezaji hapa kwa ajili ya kuhudumia Watanzania wawekezaji wa mfano wa ndani kutoka hapa Njombe na wale kutoka nje wanaokuja kuwekeza mkoani Njombe” amesema Teri.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kuweka kituo kidogo cha uwekezaji mkoani humo ili kuwapunguzia wawekezaji safari ya kufuata huduma katika kituo cha uwekezaji cha kanda kilichopo mkoani Mbeya.
Amesema Mkoa wa Njombe unakua kwa kasi na hata kipato cha mwananchi mmojammoja kimeongezeka na kila mmoja anaweza kumiliki kwa wastani zaidi ya Sh3 milioni kwa mwaka licha ya kuwa na idadi ndogo ya watu ambao ni 800,000.
Kasongwa amesema wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wanafika na kuwekeza katika maeneo, hivyo kuwepo kwa kituo hicho cha uwekezaji kitasaidia kurahisisha na kuinua shughuli za kiuchumi.
Amesema hivi karibuni serikali imesaini mkataba wa uchimbaji wa madini ya chuma huko wilayani Ludewa na kiwanda kinajengwa cha kuchenjua chuma na kutengeneza nondo huko halmashauri ya mji wa Makambako wilayani Njombe.
“Njombe tunayoiona sasa hivi ina mafanikio makubwa kwa hiyo kumuona mkurugenzi mkubwa wa kituo cha uwekezaji tuna matumaini makubwa pengine leo utasema neno sisi watu wa Njombe tukapona kwa kupata kituo kidogo cha uwekezaji ili wasihangaike sana kwenda Mbeya,” amesema Kasongwa.
Meneja Mkuu wa Misitu Kiwanda cha Tanwatt, Antery Kiwale amesema ujio wa mtendaji mkuu wa kituo cha uwekezaji mkoani Njombe ni fursa kwao na wamejifunza mambo mengi na wao kuangalia kazi ambazo wanafanya.
“Wametupa ushauri mkubwa tena mahususi wa faida ambazo sisi tutapata hasa tunapotaka kujitanua zaidi katika biashara ni wazo ambalo kampuni yetu imekuwa nalo,” amesema Kiwale.