RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi amewaonya viongozi wa vyama vya mikoa wasiowajibika na kusisitiza hawafai kuendelea kuongoza.
Isangi alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati wa ufunguzi wa mashindano ya riadha ya Taifa yaliyofanyika kwa siku mbili.
“Mashindano ya taifa yanafanyika mara moja kwa mwaka. Katika mikoa kuna mwenyekiti na katibu wa chama. Katika kipindi cha mwaka mzima kama wanashindwa kuwasafirisha wachezaji kushiriki mashindano ya taifa hawatufai na hawafai kuongoza riadha,” alisema.
Katika mashindano ya taifa, mikoa inapewa kota kulingana na historia na rekodi, huku idadi kubwa ni ya wanariadha 15 na ndogo ni wanne, mikoa ikigharamia usafiri na posho huku gharama nyingine zikibebwa na RT.
Msimu huu mikoa 17 ya Mwanza, Morogoro, Kilimanjaro, Singida, Arusha, Simiyu Mara, Shinyanga, Tanga, Dodoma, Dar es Salaam, Mjini Magharibi, Manyara, Mbeya, Kagera, Tabora na Pwani ndio iliyoshiriki.
Akifungua mashindano hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Msaidizi (Miundombinu), Arch Nghoma alisema riadha ina historia na heshima kwa taifa kimataifa.
Katika mashindano hayo Arusha, Pwani, Mbeya, Mjini Magharibi na Dodoma ilionyesha upinzani, huku mbio za mita 1500 ya wanawake, Neema Msuadi wa Arusha aliibuka kinara akitumia dakika 04:38:53, akifuatiwa na Justina John wa Dodoma aliyetumia dakika 04:39:19 na Sarah Masalu wa Pwani alikuwa wa tatu akitumia dakika 05:59:24.
Kwa wanaume, Daniel Sinda wa Arusha alibuka kinara akitumia dakika 3:54:79, Steward Mboya wa Mbeya aliyetumia dakika 3:55:22 alitwaa medali ya fedha huku Jamal Mohamed wa Arusha akimaliza wa tatu kwa dakika 3:56:78.
Mbio za Mita 100 wanawake, Emmy Hosea wa Arusha aliibuka kinara kwa sekunde 12:35, Tereza Bernard wa Mjini Magharibi alimaliza wa pili akitumia sekunde 12:36 na Leah Chadewa wa Mwanza alihimitisha tatu bora kwa sekunde 12:60.
Kwa wanaume, Ally Hamis Gulam wa Mjini Magharibi aliibuka kinara akitumia sekunde 10:51 akifuatiwa na Gasisi Gegasa wa Arusha (10:68) na Elias Silvester wa mjini Magharibi alihitimisha tatu bora kwa sekunde 10:86 na katika mbio za Mita 5000 wanawake, Transfora Mussa wa Arusha aliibuka kinara kwa dakika 17:13:27, Enestina Mng’olage wa Arusha wa pili kwa dakika 18:16:06 na Neema Nyaisawa wa Kilimanjaro wa tatu akitumia dakika 18:31:40
Katika mbio za mita 10000 wanaume Protas Gabriel wa Arusha aliibuka kinara akitumia dakika 31:53, Joshua Elisante wa Kilimanjaro aliyetumia dakika 32:08 na Nicodem Joseph wa Kilimanjaro aliyetumia dakika 32:11 walimaliza wa pili na tatu na mashindano hayo yalitarajiwa kufungwa jana Jumamosi.