Somji azamisha dume Uganda Open

MCHEZA gofu kutoka Arusha, Aalaa Somji amekuwa  kipimo cha ubora wa mikwaju katika mashindano ya ubingwa kwa wanawake ya Uganda baada ya kupiga hole-in one katika shimo namba sita la Viwanja vya Gofu Entebbe, jana Ijumaa.

Hole-in-one ni alama bora na adimu katika gofu na hupatikana kwa mcheza gofu kuingiza mpira shimoni moja kwa moja kwa pigo moja kutoka sehemu ya kuanzia. Ni pigo ambalo ni nadra kulipata na hiyo inampa Somji hadhi ya kuwa mmoja wa waweka alama adimu katika viwanja vya mchezo huo.

Lilikuwa shimo la wastani wa mapigo matatu (par 3) ya mpira, lakini nyota huyu kinda kutoka Arusha aliujaza mpira shimoni kwa pigo moja na hivyo kujiweka katika orodha ya wacheza gofu wachache duniani wenye bahati ya kushinda hole-in-one.

“Kusema kweli sikutegemea kuwa nitalamba dume (ace). Nililenga mpira karibu na shimo na ukaingia,” Somji alikaririwa akisema.

“Ilikuwa ni kiasi cha yadi 125 katika shimo namba sita. Kwangu nilitumia fimbo ya chuma 9 na ikanipa matokeo adhimu.

“Sikuona kilichoendelea mbele baada ya kuupiga mpira kwa chuma 9, ila muda mfupi baadaye nikasikia watu wakishangilia kwa nguvu na kupiga makofi kwa wingi. Nilikuja kutambua nimelamba dume yaani hole-in one, na sintaisahau siku hii na uwanja huu namba sita. Nikautoa mpira shimoni na kuandika mkwaju mmoja katika kadi ya alama. Nilifurahi mno na siwezi kuilezea zaidi furaha yangu.”

Licha ya kulamba dume siku ya pili yenye jumla ya mashimo 36, Somji alimaliza wa tisa katika siku ya pili baada ya kurudisha mikwaju 83.

Alianza vizuri mashindano kwa kupiga mikwaju 79, lakini kinachoonekana ni kuzidiwa na furaha alirudi chini siku ya pili kwa mikwaju minne.

Kabla ya kwenda  Uganda, Somji pia alishiriki mashindano ya wazi ya wanawake ya Zambia ambapo  alimaliza katika nafasi ya tisa nyuma ya mshindi wa jumla Madina Iddi kutoka Tanzania.

Somji pia alimaliza katika nafasi ya saba katika mashindano mengine ya wazi ya wanawake nchini Uganda wiki moja nyuma ambapo mshindi wake wa kwanza pia alikuwa Mtanzania Madina Iddy.

Related Posts