VIDEO: Ilichobaini polisi matukio matatu ya utekaji, watu kupotea

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetoa taarifa kwa umma kuhusu matukio matatu ya watu kutekwa au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na kukutwa wakiwa wameuawa.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo Jumamosi Agosti 24, 2024, imetolewa kukiwa na matamko kadhaa kutoka kwa umma, ukilitaka kutoka hadharani kuzungumzia matukio hayo, baadhi yakidaiwa kuwahusisha askari.

Agosti 10, 2024 Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kiliweka hadharani orodha ya watu 83, kikidai walitekwa na wengine kupotea na hawajulikani walipo mpaka sasa.

TLS ilipendekeza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda chombo maalumu kulichunguza Jeshi la Polisi sambamba na matukio hayo.

TLS ilimshauri Rais Samia kuunda tume maalumu kuchunguza matukio yote ya kupotea kwa watu, kutekwa na kuteswa ikisema tangu mwaka 2016 hadi 2024 watu 83 wamepotea, kutekwa na wapo waliopatikana wakiwa na majeraha, kufariki huku wengine hawakupatikana hadi sasa.

Mbali ya TLS, Agosti 22, 2024 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ilitangaza kufanya uchunguzi maalumu wa matukio hayo katika mikoa 15, ikiwemo Dar es Salaam na Arusha yaliyotokea kati ya mwaka 2020 hadi 2024 ili kubaini chanzo na wahusika wake.

Siku hiyohiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokradia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akieleza matukio ya utekaji na watu kupotea nchini, akilituhumu Jeshi la Polisi kuhusuika na kupotea kwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na wenzake wawili.

Alishauri kuundwa tume ya Rais ya majaji ili kufanya uchunguzi wa kina na wahusika kuchukuliwa hatua.

Misime katika taarifa kwa umma ametaja tukio la kijana Samwaja Said (22) mkazi wa Kijiji cha Chalunyangu mkoani Singida aliyetoweka tangu Agosti 8, 2024 na Agosti 23, 2024 mwili wake kukutwa umefukiwa kwenye shimo, huku sehemu zake za siri zikiwa zimekatwa.

“Tukio la kutoweka kwake liliripotiwa katika Kituo cha Polisi Makuro na lilifunguliwa jalada na uchunguzi kuanza.

“Baada ya ufuatiliaji wa kina wa Polisi zilipatikana taarifa kwa kijana ambaye walikwenda kutazama mpira na Said (marehemu) na baada ya mpira kumalizika walipokuwa wakirejea nyumbani walikutana na vijana wawili waliomwambia waende wakanywe pombe,” inaeleza taarifa.


Ilichobaini polisi matukio matatu ya utekaji, watu kupotea

Walipoondoka pamoja naye hakurejea nyumbani ndipo ndugu zake wakafika Polisi kutoa taarifa,” amesema.

Misime amesema Polisi waliwakamata vijana hao wawili na baada ya mahojiano walieleza ni kweli walikwenda kunywa pombe na Said na walipokuwa wanarejea, walimuua kwa kumnyonga kisha kukata sehemu zake za siri na kuufukia mwili wake kwenye shimo.

“Watuhumiwa hao pia walieleza walifanya hivyo baada ya kuelezwa na mganga wa kienyeji kuwa, wakipata sehemu za siri za binadamu watakuwa matajiri. Polisi walifanikiwa kumkamata mganga huyo. Walieleza wapo tayari kwenda kuonyesha walipoufukia mwili wa marehemu,” amesema.

Katika taarifa hiyo, amesema Agosti 23, 2024 watuhumiwa walikwenda kuonyesha walipofukia mwili wa marehemu, ufukuaji ulifanyika na mwili ulitambuliwa kuwa wa Said aliyetoweka Agosti 8, 2024.

“Hata hivyo, baada ya wananchi kushuhudia mwili wa marehemu na kubaini watuhumiwa waliohusika waliamua kwenda nyumbani kwa mganga huyo kwa nia ya kuchoma nyumbani yake moto,” amesema.

Amewataja waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo, ambao wanaendelea kushikiliwa ni Selemani Nyandalu maarufu Hango (24), mkazi wa Chalunyangu, Saidi Msanghaa ‘Mangu’ (24), mkazi wa Kijiji cha Migungu na Kamba Kasubi (34), ambaye ni mganga wa kienyeji mkazi wa Kijiji cha Migungu Mtinko.

Misime amesema Agosti 19, 2024 iliripotiwa kuwa, mwanamke Ezenia Kamana (36) mkazi wa Tandika Maghorofani wilayani Temeke ametoweka.

“Katika uchunguzi zilipatikana taarifa kuwa mwanamke huyo alikuwa na rafiki yake wa kiume Abdallah Miraji maarufu Mussa (42), mkazi wa Sinza kwa Remmy na walikuwa na mgogoro.

Amesema alikamatwa na alipohojiwa alikataa kuwa hafahamu alipo rafiki yake huyo.

Misime amesema Agosti 22, 2024 zilipokewa taarifa kuwa eneo la Silversand barabara ya Mtaa wa Freedom, Kunduchi kumeonekana mifuko ambayo ina viungo ambavyo vinadhaniwa ni vya binadamu.

Amesema polisi walipofika eneo hilo walikuta viroba vinne, walipochunguza walikuta viungo vya binadamu ambavyo ni paja moja, vipande vya mikono miwili, eneo la kifua, kalio, matumbo na nguo.

Amesema baada ya viungo hivyo kupatikana, mtuhumiwa alielezwa akaamua kusema ukweli kuwa alimuua mpenzi wake kwa kutenganisha mwili katika vipande na kwenda kuvitupa maeneo tofauti.

Agosti 23, 2024 amesema aliwaongoza askari hadi eneo la Tegeta Block D alikoonyesha alipotupa miguu na baadaye aliwaonyesha eneo ambalo alitupa kichwa.

Misime amesema mkoani  Tanga mtoto Elia Elifaza kwa jina lingine Raymond Mchome mwenye miaka mitatu, mkazi wa kitongoji cha Kwedijava wilayani Handeni alitoweka katika mazingira yasiyoeleweka Agosti 19, 2024 alipokuwa anacheza nje ya nyumba yao.

Amesema taarifa ilitolewa polisi na uchunguzi uliwezesha kukamatwa Jackson Elisante ‘Maeda’ (23), mkazi wa Kwedijava eneo linalochimbwa madini ya dhahabu.

Taarifa inaeleza alipohojiwa alikubali kumchukuwa mtoto huyo na kwamba, alimkabidhi mama yake mkubwa ambaye alienda naye Babati mkoani Manyara.

“Askari waliambatana naye hadi Babati lakini alibadili kauli na kueleza mtoto yupo Kwedijava, Handeni amemfukia ndani ya chumba anachoishi,” amesema.

Misime amesema walirejea Handeni akaonyesha chini ya kitanda kwenye chumba anachoishi alikokuwa amemfukia mtoto huyo baada ya kumuua.

Amesema wengine wanaoshikiliwa katika tukio hilo kwa ajili ya uchunguzi ni Sadick Lugendo, Mahiza Gumbo, Maligo Juma, Ally Mashaka, Juma Bakari, Abdulrahman Selemani na Bahati Daudi.

Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa watu kuacha tabia ambazo zinasababisha watu kudaiwa kupotea au kutekwa ambazo ni pamoja na wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, tamaa za mali au fedha na kulipiza kisasi.

“Tunatoa angalizo kwa baadhi ya watu wanaozungumzia matukio ya aina hii watumie majukwaa yao kwa ungalifu kwani sababu wanazotoa ni kutaka kubadilisha ukweli ya yanayoendelea ndani ya jamii ili kuleta taharuki na kujenga uhasama,” amesema.

Ametoa rai kwa viongozi wa dini, wazee wa kimila, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuona matatizo hayo yanayotokea ndani ya jamii, hivyo waendelee kujenga misingi bora ya kuyazuia kuanzia ngazi ya familia.

Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kujichukulia sheria mikononi badala ya kufuata taratibu zilizopo za kuwasilisha malalamiko ili yapatiwe ufumbuzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

“Wakumbuke malalamiko au kero hata siku moja hayatatuliwi kwa njia ya kujichukulia sheria mikononi kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, husababisha madhara kwa maisha ya watu na mali zao,” amesema.

Misime ametoa mfano wa tukio la baadhi ya wananchi  kujichukulia sheria mikononi huko Lamadi, mkoani Simiyu Agosti 22, 2024 na kwenda kuvamia kituo cha Polisi na kuharibu mali.

“Wakumbuke ni kosa la jinai na limesababisha madhara kwa binadamu, mali na kuzuia shughuli za maendeleo kuendelea.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa wenye tabia kama hizo na yeyote mwenye mawazo ya kuendelea kufanya uhalifu kama huo, Jeshi la Polisi lipo imara kwani litachukua hatua kwa nguvu ileile ambayo watu wa aina hiyo wanatumia katika kutekeleza uhalifu wa kujichukulia sheria mikononi,” amesema.

Related Posts