Dar es Salaam. Katika kuongeza thamani ya soko la kahawa, Tanzania imepanga kuwa mwenyeji wa kongamano la maonyesho ya kahawa litakalofanyika Februari 2025 jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo linafanyia ikiwa imepita miaka minane tangu lilipofanyika mwaka 2016 kwa kushirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Imeelezwa kuwa, kongamano hilo litakaloambatana na maonyesho ya bidhaa za kahawa litakuwa na vibanda takribani 80 na linatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 2,000, na kuifanya kuwa mkutano mkubwa zaidi wa kahawa katika bara la Afrika.
Akizungumza katika uzinduzi wa kongamano hilo leo Agosti 22, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Kahawa Bora za Afrika (AFCA), Gilbert Gatali amesema maonyesho hayo yataendelea kuitangaza nchi kutokana na sifa walizonazo Watanzania za ukarimu wa kipekee na uzalishaji wa kahawa.
“Tanzania tunayo furaha kurudisha tukio hili muhimu katika nchi hii nzuri wahudhuriaji watapata fursa ya kushiriki katika safari ya kahawa, kuchunguza mashamba ya kahawa maarufu nchini Tanzania na mandhari ya asili ya kuvutia, ikiwa ni pamoja na Bonde la Ngorongoro na Ziwa Manyara,” amesema Gatali.
Amesema, dhamira ya AFCA ni kukuza maarifa na uhusiano wa kibiashara ndani ya sekta ya kahawa na mkutano ujao unaahidi kuwa jukwaa muhimu la mitandao, kujifunza na ukuaji wa biashara.
Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema kongamano hilo lina dhamira ya kuimarisha sekta ya kahawa kwa manufaa ya wadau wote, kuanzia wakulima hadi watumiaji.
“Wakulima nchini, wakisaidiwa na vyama vya ushirika na huduma za ugani, wamejitolea kudumisha na kuimarisha urithi huu,” amesema Kimaryo.
Amesema kongamano hilo limekuwa muhimu katika historia ya uzalishaji na uuzaji wa kahawa, hasa barani Afrika na Tanzania ambayo ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa kahawa barani Afrika, zikiwamo pia nchi za Ethiopia, Uganda, Ivory Coast, na Kenya.
Kimaryo amesema Tanzania inajivunia urithi mkubwa wa aina mbalimbali za kahawa za ubora wa juu, ikiwa ni pamoja na Arabica na Robusta.
Hata hivyo, tukio hilo linatoa fursa ya kipekee kwa wadau nchini kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa na kutumia mbinu bora za kuimarisha uwepo wao katika soko la kimataifa.
Amesisitiza mahitaji ya mbinu shirikishi na bunifu ili kushughulikia changamoto kubwa kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na soko.