Rais Samia akoshwa usimamizi na makusanyo ya kodi ZRA

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema amefurahishwa na kazi inayofanywa na  Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali.

Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Agosti 24, 2024 katika maonyesho ya Tamasha la Kizimkazi alipomtembelea banda la mamlaka hiyo Mkoa wa Kusini Unguja.

Kwa mwaka wa fedha 2023/24,  ZRA imekusanya Sh718.7 bilioni kati ya malengo ya kukusanya Sh675.6 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 106.

Rais Samia amesema hali hiyo inaisaidia Serikali kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo na kuendesha mipango yake kwa wakati.

“Ninafurahishwa na kazi mnayoifanya ya kukusanya na kusimamia Mapato ya Serikali,” amesema .

Hata hivyo, ameitaka mamlaka hiyo iendelee kufanya kazi zaidi kuwafikia walipa kodi ili ifanikiwe kukusanya kodi zaidi kwa ufanisi.

Amesema Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), zina matumaini na mamlaka za kodi, hivyo hakuna budi kwa taasisi hizo kuhakikisha zinafanya kazi zao kwa weledi ili kutimiza malengo.

Amesema Serikali zinategemea zaidi ukusanyaji wa mapato ya kodi ili ziweze kuhudumia miradi mbalimbali ya kimaendeleo pamoja na kutoa huduma za kijamii zikiwamo za afya, majisafi na salama, huduma za elimu na nyinginezo.

Tamasha la Kizimkazi limekuwa jukwaa linaloendelea kukua na kuvutia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara mbalimbali kwa kutoa fursa ya kuonesha bidhaa au huduma zinazotolewa na kampuni au taasisi tofauti na hatimaye kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa ZRA, Makame Khamis amesema mamlaka hiyo imeendelea kuwa taasisi muhimu katika udhamini na ushiriki wa Tamasha la Kizimkazi kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Amesema inayatumia maonyesho hayo kwa kutoa huduma mbalimbali ikiwamo elimu ya kodi, usajili wa walipakodi pamoja na kutoa leseni za udereva.

Related Posts