Mwanza. Pamba Jiji imeshindwa kufurukuta tena katika uwanja wake wa nyumbani wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya kushindwa kuondoka na pointi tatu ikilazimishwa sare ya pili mfululizo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Timu hiyo ambayo ni mchezo wake wa pili ndani ya Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa takribani miaka 23, imelazimishwa suluhu na Dodoma Jiji, leo Agosti 24, 2024 mchezo ukichezwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Sare hiyo ni ya pili mfululizo kwa Pamba baada ya mechi ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons kulazimishwa suluhu katika Uwanja wa CCM Kirumba ambao ni Uwanja wake wa nyumbani msimu huu baada ya msimu uliopita kutumia Uwanja wa Nyamagana, hivyo, kuonekana bado Uwanja huo ni mgumu kwa TP Lindanda ikiwa haijafunga bao lolote.
Kwa matokeo ya leo Pamba Jiji inafikisha alama mbili, huku Dodoma Jiji ambayo mchezo uliopita ilichapwa bao 1-0 na Mashujaa FC ikivuna pointi ya kwanza Ligi Kuu.
Katika mchezo huo uliokuwa na mashambulizi ya kushtukiza kwa pande zote mbili, kipa wa Dodoma Jiji, Mohamed Mohamed alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo iliyoelekezwa langoni kwake.
Mshambuliaji mpya wa Pamba Jiji, George Mpole amerejea Ligi Kuu na kucheza mchezo wa kwanza baada ya kukosekana kwa takriban mwaka mmoja, ambapo amecheza dakika 45 na kuwakosha mashabiki waliokuwepo uwanjani wakimpigia makofi.
Mpole ambaye alikosekana katika mchezo uliopita, aliingia dakika ya 45 akichukua nafasi ya Costantine Gabriel na kuiongezea uhai safu ya ushbuliaji, dakika ya 71 shuti lake limegonga mwamba wa juu, na dakika ya 47 shuti lake likapanguliwa na kipa na kuwa kona.
Kiwango alichoonyesha George Mpole kilimfanya achaguliwe kuwa nyota wa mchezo huo na kukabidhiwa zawadi na wadhamini wa Ligi Kuu.
Makocha wa timu zote mbili, Goran Kopunovic wa Pamba Jiji na Mecky Maxime wa Dodoma Jiji, Kila mmoja kwa nafasi yake alionekana muda mwingi kutoa maelekezo na kufanya mabadiliko ya wachezaji ambayo mwisho wa siku hayakuleta pointi tatu, wakijikuta wakigawana alama mojamoja.
Kocha wa Pamba Jiji, Goran Kopunovic, amesema licha ya kutopata ushindi lakini wachezaji wake wamecheza vizuri na kufuata maelekezo ya kiufundi, hivyo anapata imani kwamba mbeleni watapata matokeo mazuri na kuinuka kutoka hapo walipo.
Naye Mecky Maxime wa Dodoma Jiji, amesema kikosi chake kinaimarika kutoka mchezo mmoja hadi mwingine, huku akitoa wito kwa Bodi ya Ligi Kuu kutotoa tuzo za mchezo bora wa mechi kwa kuangalia timu mwenyeji pekee bila kuzingatia ubora wa wachezaji uwanjani.