Mgomo wa wafanyabiashara Mafinga waingia siku ya pili

Mufindi. Mgomo wa wafanyabiashara  katika  Soko Kuu la Mafinga lililopo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wa kufunga maduka, umeingia siku ya pili leo Agosti 24, 2024 ukisababisha adha kwa wananchi kukosa huduma.

Mwananchi limefika sokoni hapo na kushuhudia milango ya maduka hayo imefungwa huku baadhi ya wananchi waliofika kwa ajili ya kupata huduma wakiduwaa wasijue cha kufanya.

Wafanyabiashara wamedai kuwa hawatafungua maduka hadi malalamiko yao ya kupunguziwa kodi ya Sh80,000  yatakaposikilizwa.

Mwananchi ilimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa kuzungumzia hali hiyo lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda baada ya kutafutwa bila mafanikio.

Hata hivyo, Diwani wa Boma, Julias Kisoma lilipo soko hilo, amethibitisha wafanyabiashara hao kufunga maduka kwa madai kodi wanayolipa ni kubwa.

Muonekano wa maduka yakiwa yamefungwa katika Soko Kuu la Mji Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa leo Jumamosi Agosti 24, 2024. Picha na Mary Sanyiwa

“Wafanyabiashara wanalalamikia kodi wanayolipa ni kubwa ambayo ni ya zaidi ya asilimia 200, lakini mimi kama diwani nitaendelea kuwasemea wafanyabiashara hawa hadi pale nafasi yangu ya uongozi itakapokoma,” amesema diwani huyo.

Wakizungumzia adha hiyo, baadhi ya wananchi wamesema hali hiyo imewasababishia adha kubwa ya kufika sokoni bila kupata mahitaji kutokana na mgomo huo.

“Nimetoka kijijini kwa ajili ya kununua mahitaji ya duka langu lakini nimefika hapa nimekuta maduka yamefungwa, hivyo nimepoteza nauli muda katika suala hilo,” amesema mkazi wa Mtili, Prisca Mlelwa.

Mlelwa ametoa ombi kwa Serikali kukaa meza moja na wafanyabiashara hao ili wafikie mwafaka na kuendelea na biashara zao.

“Wananchi wengi wanapoteza muda kwa sababu hawakujua kama wafanyabiashara wamegoma na wengi wao wametoka maeneo ya mbali kwa ajili ya kupata mahitaji bila mafanikio,” amesema Mlelwa.

Muonekano wa maduka yakiwa yamefungwa katika Soko Kuu la Mji Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa leo Jumamosi Agosti 24, 2024. Picha na Mary Sanyiwa

Kwa upande wake, mkazi wa Nyololo, John Mgaya amesema Serikali inapaswa kushughulikia suala hilo  haraka ili kuwapunguzia wananchi adha ya kukosa huduma.

“Serikali ishughulie suala hili kwa sababu ni mambo yanayozungumzika ili wafanyabiashara hao waendelee kufanya biashara kuliko hali kama hii, mtu anatoka kijijini akijua anakuja kupata mahitaji lakini ikifika anakuta maduka yamefungwa,” amesema.

 Godson Sadaka, mfanyabiashara katika soko hilo, amesema wafanyabiashara walijenga vibanda na kumekuwa na mvutano na Halmashauri ya Mji Mafinga kwa muda mrefu kuhusu vibanda hivyo.

“Jambo hili hutakiwi kumuonea mtu kwa sababu unaweza kuua duka, akija kiongozi mkubwa madiwani ndiyo wanatakiwa kujibu kwa sababu wao ndio wanajua hali zetu,” amesema Sadaka.

Muonekano wa maduka yakiwa yamefungwa katika Soko Kuu la Mji Mafinga Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa leo Jumamosi Agosti 24, 2024. Picha na Mary Sanyiwa

Awali, akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa Soko Kuu la Mafinga, Philinus Mgaya amesema wafanyabiashara hao waliomba kupunguziwa kodi ya Sh80,000 ili kulipa Sh50,000.

“Tunaomba Serikali isikilize kilio chetu sisi kama wafanyabiashara watupunguzie kiwango hicho cha Sh80,000 ili tuweze kulipa Sh50,000 kwa sababu tuliambiwa tulipe madeni yetu yote ya nyuma Sh9,000 kwa kila kibanda (331), lakini tumelipa madeni hayo na hadi sasa hawazidi hata 10 ambao wamebakia,”amesema Mgaya.

Mgaya amesema baada ya wafanyabiashara hao kutii agizo la kulipa madeni hayo, wamedai kuwa mkuu huyo aliwaambia waanze kuonyesha jitihada ya kulipa Sh80,000 kisha watafikiliwa maombi hayo kwa kupunguziwa kiasi hicho.

Related Posts