Morogoro. Shirika la Maendeleo ya Jamii la DDSCDD na shirika lisilo la kiserikali la Norwegian Church Aid (NCA) kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro wameanzishwa mradi wa kuzibadili taka kuwa bidhaa za thamani.
Mradi huo unaohusisha makumi ya vijana wa Manispaa ya Morogoro ulizinduliwa Alhamisi Agosti 22, 2024 kwa vijana kukabidhiwa kiwanda kidogo cha kuchakata taka tofauti zikiwamo chupa za plastiki kwa ajili ya ureshwaji.
Meneja mradi huo kutoka DDSCDD ambayo ipo chini ya Kanisa Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Pius Ngirwa amesema lengo ni kuunga mkono sera ya ulinzi wa mazingira inayotaka kuifanya Tanzania kuwa na mazingira endelevu, safi na yenye afya ubora.
“Ni mradi wa majaribio wa kuzibadili takataka kuwa mali, hii ni zaidi ya biashara, kwa inalinda mazingira na kutoa fursa kwa vijana na hiki ni kielelezo kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuleta matokeo chanya,” amesema Ngirwa.
Ngirwa amesema mradi huo wa miaka miwili utahusisha kata nne (Mjimkuu, Mafisa, Kichangani na Mwembesongo), huku Sh300 milioni zikitarajiwa kutumika kutengeneza miundombinu bora na wezeshi.
Vijana watakabidhiwa mradi huo waendeshe ili kupunguza ukosefu wa ajira.
“Taka kuwa mali si kazi ya watu wa hali ya chini, nchi nyingine hata waliomaliza chuo kikuu wanafanya kazi hizi. Nyumba 10,000 zitafundishwa namna ya kutenganisha taka za plastiki, kioo, chuma na za kikaboni watu 150,000 wanatarajia kunufaika,” amesema.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa NCA, Gwamaka Mwakyanjala amesema taka ni fursa za kiuchumi lakini kwa kushirikiana na wadau pamoja na jamii ya Morogoro wataboresha mazingira, hivyo manufaa ya mradi huo ni makubwa.
“Taka zimekuwa zikifanya watu tuwaweke kwenye kundi fulani, mfano waraibu wa dawa za kulevya (mateja) lakini sasa tunapaswa kubadili fikra na kujua kuwa ni fursa ya kiuchumi na kwetu sisi kulinda mazingira ni kipaumbele. Kukusanya na kurejesha na kutengeneza ajira ambazo upatikanaji wake umekuwa wa kusuasua ni jambo litakaloleta nafuu kubwa,” amesema.
Meya Morogoro, Pascal Kihanga amesema mradi huo utasaidia kuboresha hali ya usafi ya manispaa anayoiongoza na kutoa ajira.
“Tuna changamoto ya mabadiliko ya tabianchi lakini sisi binadamu ndiyo tumeifikisha hapa hali hii bila kujua na yote hayo tulikuwa tunatafuta maendeleo, na sasa dunia nzima imeshtuka juhudi kubwa ni kulinda mazingira na mradi huu pamoja na kulinda mazingira lakini mtakuwa mnatengeneza fedha,” amesema.
Amesema kabla ya mradi huo taka zote zilikuwa zinachoma lakini sasa ana imani kuwa baadhi zitakuwa zinachakatwa.
“Tumekuwa tukichoma mali kwa kuwa hatujui cha kufanya tukishajua hamna kuchoma tena,” amesema Kihanga.