Kinara wa mabao aitega Ken Gold

BAADA ya kuandika rekodi mbili tamu Championship, winga wa Ken Gold, William Edgar amesema bado hajajua hatma yake kubaki au kuondoka kikosini humo msimu ujao.

Nyota huyo ameshinda tuzo ya mfungaji bora akitupia mabao 21 na pia hii ni mara ya pili kuipandisha timu Ligi Kuu baada ya msimu wa 2021/22 kuipandisha Mbeya Kwanza.

Kwa misimu minne nyuma, nyota huyo amekuwa katika kiwango bora akifunga mabao mengi na kuwa kwenye vita ya kuwania kiatu cha mfungaji bora japokuwa alizidiwa na wapinzani.

Katika msimu uliopita Edgar alitupia mabao 15 akiachwa na aliyekuwa kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyemaliza msimu kwa mabao 18 na kuipandisha timu hiyo Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Edgar amesema mpira ndio kazi yake hivyo hawezi kuweka wazi wapi atakuwa msimu ujao, licha ya kwamba anaipa nafasi zaidi Ken Gold.

Amesema kilichompa ufanisi katika ligi hiyo ni kutokana na ushirikiano ndani na nje ya uwanja na pia kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ndio ilikuwa silaha kwake.

“Hii ni kazi yangu, nitaangalia masilahi japokuwa naipa nafasi kubwa timu yangu niliyoipandisha, nilijituma na kushirikiana na wenzangu, lakini zaidi kufuata maelekezo ya kocha,” amesema Edgar.

Nyota huyo ameongeza kuwa haikuwa kazi rahisi kuweza kufikia malengo kutokana na upinzani wa ligi ulivyokuwa kutokana na timu zilivyojipanga haswa kwenye nafasi nne za juu.

Amesema wanapoenda Ligi Kuu lazima wajipange vizuri kuhimili mikiki ya wapinzani ili kuweza kubaki kwa muda mrefu akiwaomba wenzake kujiandaa kiushindani.

“Haikuwa kazi rahisi, timu zilijipanga haswa zile za nafasi nne juu, kwa ujumla tunajipongeza na kuwashukuru wadau kwa sapoti yao na tutajipanga katika Ligi Kuu tuweze kufanya vizuri,” amesema staa huyo.

Related Posts