Kwa mzazi inaweza isikuingie akilini kwamba watoto wako unaoishi nao nyumba moja wanaweza kuwa na uhusiano wa kimapenzi, ila ukweli uko hivyo, yapo matukio mengi ya aina hiyo ambayo yanaendelea kushika kasi kwenye jamii.
Hii inahusisha ndugu wa damu, ndugu wa familia au ukoo na hata baba na mtoto ambayo kwa tamaduni zetu wanaitwa maharimu.
Kwa sheria za Tanzania, ni kosa maharimu kujamiiana au kuwa na uhusiano wa kimapenzi, lakini huenda utandawazi umefanya jambo hili kuanza kuonekana kawaida na matukio ya ndugu kuwa na uhusiano wa kimapenzi yameanza kuingia kwenye jamii yetu.
Mfano wa hili ni kile kilichotokea Agosti 14, 2024, Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ilitoa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa Mussa Shija (32) na miaka 30 jela kwa Hollo Shija baada ya kukutwa na kosa la kujamiiana na maharimu.
Mahakama ilithibitisha wawili hawa kuwa ni ndugu wa damu waliokuwa na uhusiano wa kimapenzi, wakiishi pamoja kama mume na mke kwa zaidi ya miaka mitano na kufanikiwa kupata mtoto mmoja.
Kesi hii iliibua mjadala kwa wengi, wakihoji inawezekanaje kwa ndugu wa damu kuwa na uhusiano wa kimapenzi hadi kufikia hatua ya kuishi pamoja kama mke na mume?
Matukio ya aina hii huenda yakachukua sura mpya kwenye jamii kufuatia kuwepo ongezeko kubwa la kesi za ndugu wa damu kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Ripoti ya Hali ya Uhalifu nchini iliyotolewa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonesha kwa mwaka 2023 jumla ya matukio 233 yaliyohusisha maharimu kuzini yaliripotiwa, huku mkoa wa Arusha ukiongoza kuwa na kesi nyingi za aina hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto 68 walikutana na ukatili huo ambapo mkoa wa Tanga uliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliozini na maharimu, kukiwa na jumla ya watoto 35 kati yao 34 wa kike na mmoja wa kiume.
Wakati ripoti ikionesha hivyo, mtaani zipo shuhuda mbalimbali za ndugu kuwa na uhusiano wa kimapenzi, kama inavyoelezwa na baadhi ya watu waliozungumza na jarida hili ambao waliomba majina yao kuhifadhiwa.
“Kwenye familia yetu kuna hii changamoto, tulibaini mtoto wa baba mkubwa na baba mdogo wana uhusiano wa kimapenzi, tena walianza mmoja akiwa shule ya msingi mwingine sekondari. Tulipogundua walitenganishwa mmoja akapelekewa nje ya nchi, lakini haikusaidia, wenyewe wanasisitiza wanapendana,” kilieleza chanzo hicho.
Chanzo kingine kilieleza; “Mtoto wa kike wa dada yangu alipata ujauzito wa mtoto wa kiume wa baba yake wa kambo. Dada yangu ndiye aliyegundua hili, hakutaka watu wengi wafahamu, kwa haraka akamtoa ujauzito yule binti”.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka anasema hayo ni matokeo ya wazazi kuacha jukumu la kulea na kuruhusu utandawazi uendelee kuathiri maadili.
“Wazazi wa sasa hawalei bali wanafuga. Wanaishi na watoto wao kama mifugo, wanachohakikisha wao wanawapatia chakula, malazi, makazi na elimu. Tunatakiwa kutoa mafunzo ya malezi kwa wazazi, hawana hiyo elimu, wanatumia muda mwingi kutafuta kipato na kusahau kabisa kuhusu kulea, matokeo yake ndiyo haya.
“Utandawazi unawafanya watoto wawe huru kujifunza vitu vilivyo juu ya umri wao na kwa akili ya watoto, wanachokiona wanafikiria kukijaribu, hapo kwenye kujaribu ndiyo anajikuta akijaribu na ndugu yake,” anasema na kuongeza;
“Ndiyo maana Uislamu unasisitiza watoto wakishafikia umri wa kubalehe watenganishwe, wa kike walale kwao na wa kiume kivyao, changamoto iliyopo sasa hata hao wa kiume wakilala peke yao bado kuna hatari.”
Sheikh Mataka anasema matukio ya aina hiyo yapo kwenye jamii na yameanza kukomaa, huku mengine yakihusisha wazazi wa kiume.
“Hivi vitu vipo kwenye jamii na siyo kwa watoto tu, wakati mwingine tunakutana na kesi za baba anatembea na mtoto wake, mara nyingi hata ikigundulika haiwekwi hadharani kwa kuficha aibu kwenye familia na wakati mwingine kumlinda binti asije kukosa mume,” anasema.
Anasema kukabiliana na hayo, ni muhimu kwa wazazi wakajikita kwenye misingi bora ya malezi na kuwajengea watoto wao hofu ya Mungu ili wenyewe wajiweke mbali na mambo yasiyofaa.
Mwanasaikolojia Jacob Kilimba anasema zipo sababu za kisaikolojia ambazo zinaweza kuwafanya ndugu wa damu wakaangukia kwenye uhusiano wa mapenzi na mara nyingi hutokea pale wanapokosa mwongozo tangu wakiwa wadogo.
“Siku zote mtoto anazaliwa akiwa hana kitu kichwani, kadiri anavyokua, kila kitu kinapozalishwa kwenye mwili kinatakiwa kielekezwe namna ya kufanyika. Kuna mtoto hadi anakua hajui kwamba suala la uume kusimama ni la kibailojia na sio lazima afanye mapenzi.
“Sasa kama mtoto anapopitia mabadililiko ya kimwili hajui chochote, halafu anaona kwenye filamu watu wanafanya mapenzi au kubusiana, yeye hajui kama wale wanaigiza, anachoona pale ni mwanamke na mwanamume, hiyo kitu inaingia kichwani mwake na anapopata nafasi, lazima afanye majaribio,” anasema Kilimba.
“Changamoto iliyokuwepo watoto hawana mwongozo na inawezekana kabisa wala asijue tofauti yake na ndugu yake, ndiyo maana unasikia watoto wameanza michezo hiyo. Kwa kifupi watoto wanatakiwa kutengenezwa mwongozo ili wasikiingize kichwani kila wanachokiona kwa kuwa inaweza kutengeneza hisia ambazo hawezi kuzidhibiti kisaikolojia,” anasema.
Anasema ni muhimu wazazi kuwa na utamaduni wa kuzungumza na watoto kuhusu mabadiliko ya kimwili, hasa kihisia na kuwafundisha namna ya kuishi na hisia za kimwili na mipaka yake katika kuzitoa.
“Kisaikolojia iko hivi, zinapoibuka hisia kwa mtoto udhibiti wake unategemea mtu aliye karibu naye mara kwa mara, inawezekana wewe ukawagundua ukubwani, kumbe wenyewe walianza tangu utotoni, wakiangalia movie wanaona walio kitandani ni mwanamke na mwanamume na wao ni wa kike na wa kiume, kwa nini wasifanye.”
Mwanasaikolojia huyo anafafanua kuwa kwa wale ambao wanaendeleza michezo hiyo katika ujana ni matokeo ya kuotesha mizizi ambayo kuing’oa kwake inahitaji nguvu.
“Kuna wale ambao wanatengeneza bond kabisa, halafu wapo ambao wanashuhudia wazazi wao wakigombana, hivyo wanaona hakuna haja ya kuanzisha uhusiano na watu wa nje, bora wabaki wenyewe, kitu ambacho ni hatari.
Kwa mujibu wa kifungu cha 158 (1) (b) na kifungu 160 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16, ni kosa kwa mwanamume na mwanamke kujamiiana na ndugu yake wa damu.
Kifungu cha 158 (1) kinaeleza mwanamume yeyote ambaye amekatazwa kufanya ngono na mwanamke yeyote ambaye anamjua kuwa ni mjukuu wake, binti yake, dada yake au mama yake na akifanya hivyo atakuwa ametenda kosa.
Wakati kwa wanaume ikiwa hivyo, kifungu cha 160 kinaeleza mwanamke yeyote mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 ambaye anaridhia na kuruhusu kuzini na babu, baba, kaka au mtoto wake wa kiume atakuwa ametenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka 30.
Mbali na vitendo hivi kuzuiwa kisheria na mila na desturi za Kitanzania, inaelezwa pia vinaweza kuwa na madhara ya kiafya, hasa kwa watoto wa kike pale wanapolazimika kuitunza siri hiyo.
Akizungumzia hilo, Dk Eliya Kwiyamba anasema kuna kesi nyingi za ndugu wa familia moja kuwa na uhusiano wa kimapenzi ambao huangukia kwenye mimba zisizotarajiwa.
Anasema wakati mwingine kumekuwa na utoaji mimba usio salama kwa sababu ya kuficha aibu kwa familia kwa binti kupata mimba ya mwanafamilia, jambo ambalo linahatarisha maisha ya wasichana wengi.
“Ni jambo ambalo halizungumzwi, ila haya matukio ni mengi na tunayashuhudia huko kwenye hospitali, watu wakija kupata matibabu baada ya majaribio ya kutoa mimba. Tanzania ni kosa kisheria kutoa mimba, watu wanatoa mimba na wanakuja hospitali kutibiwa wakipata madhara yatokanayo na utoaji mimba.
“Anapokuja sasa ukisikiliza historia ya mgonjwa utabaini amejaribu kuharibu ujauzito, kazi yetu ni kuokoa maisha ya mgonjwa, lakini unapomfuatilia kwa kina sababu za kufanya hivyo ndiyo unabaini ni matokeo ya uhusiano wa kimapenzi au amebakwa na ndugu wa karibu,” anasema Dk Kwiyamba na kuongeza:
“Wakati mwingine familia inashiriki kumtoa mimba binti ili kuficha aibu ya kwamba amebeba ujauzito wa mwanafamilia mwingine, iwe kwa kuwa na uhusiano au labda alibakwa,”
Dk Kwiyamba, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya wanawake, anasema ni muhimu kwa wazazi kuwa makini na kuzungumza na watoto wao juu ya athari na hatari inayoweza kujitokeza kwa ndugu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na siyo kusubiri hadi majanga yatokee.
Anasema, “Ni muhimu wakati mwingine wazazi kuvunja ukimya, tuzungumze na watoto wetu hata yale tunayoyaona kuwa magumu, unaweza kuona fahari unawafungia ndani ukiamini hakuna kinachoweza kutokea kwao kaka na dada, kumbe wao wameshapiga hatua moja mbele”.