Nkuba ataja sababu kuondoa rufaa kupinga matokeo uchaguzi TLS

Dar es Salaam. Licha ya kushindwa katika uchaguzi wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na baadaye kukata rufaa dhidi ya matokeo ya uchaguzi huo, Wakili Sweetbert Nkuba hatimaye ameiondoa rufaa hiyo.

Uamuzi wake wa kuiondoa rufaa hiyo kwa mujibu wa Nkuba, umekuja baada ya mazungumzo yake na mshindi wa kiti cha urais wa TLS, Boniface Mwabukusi na wagombea wengine, wakilenga kuwaunganisha mawakili.

Nkuba alitangaza kukata rufaa Agosti 3, mwaka huu baada ya Kamati ya Uchaguzi ya TLS kumtangaza Mwabukusi kuwa rais wa chama hicho kwa kupata kura 1,274 dhidi ya kura 807 alizozipata Nkuba.

Alitangaza rufaa hiyo kwa kile alichodai kulikuwa na kasoro katika uchaguzi huo, ikiwemo kuishiwa karatasi za kupigia kura na watu kuruhusiwa kupiga kura hata baada ya muda wa ukomo uliotangazwa kuisha.

Nkuba ameieleza hatua yake hiyo jana, alipokuwa akifanyiwa mahojiano maalumu katika kipindi cha Medani za Siasa kinachorushwa na Kituo cha luninga cha Star TV.

Amesema baada ya ushindi wa Mwabukusi baadaye walizungumza juu ya kasoro alizozilalamikia kwa lengo la kuhakikisha hazijitokezi tena katika uchaguzi ujao.

Baada ya mazungumzo hayo na kwa kuwa msingi wa wagombea wote ulikuwa ni kuwaunganisha mawakili, ameamua kuiondoa rufaa yake hiyo na kwamba anakubaliana na ushindi wa Mwabukusi.

“Nilikata rufaa na baadaye tukazungumza juu ya umuhimu wa kutengeneza umoja wa mawakili na kwa sababu hiyo, tulikubaliana kuhusu mapungufu na kuona namna gani tutakavyoyatatua wakati mwingine,” amesema.

Hata hivyo, amesema kushindwa kwake katika uchaguzi huo, hakuondoi ukaribu wake na Mwabukusi, akisisitiza ni kama kaka yake waliojuana muda mrefu.

“Boniface ni kaka yangu, ni rafiki yangu na bahati nzuri wakati anahama kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kufanya kazi zake huko mimi ni mmoja wa watu alioniomba ushauri.

“Boniface alikuwa meneja kampeni wangu katika uchaguzi wa TLS uliopita. Kwa hiyo ni kaka yangu kabisa na tunaongea vizuri,” ameeleza.

Hata hivyo, ameeleza kinachopaswa kupewa kipaumbele katika utendaji wa urais wa TLS ni kusimamia kifungu cha nne cha sheria ya kuanzishwa kwa chama hicho, kama inavyofanywa na Mwabukusi.

Amesema kifungu hicho kinaeleza wajibu wa chama hicho kwa Serikali, wananchi, Bunge, kutoa elimu ya kisheria, kutetea haki za wananchi na mambo mengine.

Katika mahojiano hayo, Nkuba amesema anaamini katika siasa zitakazoruhusu mgombea binafsi na ndiyo sababu iliyomfanya awe na mapenzi na mwanasiasa wa upinzani hayati Christopher Mtikila.

Mtikila ndiye mwanasiasa aliyepeleka kesi mahakamani akipinga mabadiliko ya katiba mwaka 1993, yaliyokuwa yanazuia mgombea binafsi na mwaka 1994 alishinda.

Lakini alipeleka tena kesi hiyo mahakamani na kushinda, ingawa hadi sasa hilo halijawahi kutekelezwa.

Kwa mujibu wa Nkuba, mgombea huru ingetoa nafasi ya kupata wasiopenda kujihusisha na vyama vya siasa, lakini ni viongozi wazuri.

“Sijui woga uko wapi lakini natamani siku moja ndani ya Taifa letu, waruhusu mgombea binafsi au mgombea huru,” amesema.

Amesisitiza umefika wakati kama ilivyo mambo mengine kuangalia uwezekano wa kuwa na mgombea huru, hata kama sio kwa ngazi ya urais angalau ngazi nyingine.

Wakati wanaharakati wakishinikiza kuundwa kwa chombo huru kitakachochunguza mwenendo wa Jeshi la Polisi, Nkuba naye ana msimamo kama huo, akifafanua kisiishie kwa polisi kichunguze vyombo vyote vya ulinzi na usalama.

Uwepo wa chombo hicho kwa mujibu wa Nkuba, utaongeza hali ya usimamizi wa vyombo vya dola.

“Hii inasababisha hata kama bila kuingilia majukumu, angalau na wao wanaweza kuwa na woga kwamba, sisi tusipofanya kwa kadri sheria inavyotaka kuna chombo kitatuchunguza na ikaanika maovu tutakayoyafanya,” amesema.

Ameeleza kwa maendeleo yaliyofikiwa sasa, ni muhimu kuwa na aina kama hiyo ya chombo.

Msingi wa majibu yake hayo ni swali aliloulizwa kuhusu hatua ya Jeshi la Polisi kujichunguza lenyewe linapokosea.

Aliambatanisha majibu yake hayo na msisitizo kuwa hafurahishwi na kuongezeka kwa matukio ya utekaji kama inavyoripotiwa, kadhalika anachukizwa na aina nyingine zote za uhalifu unaofanyika nchini.

Ili kudhibiti vitendo hivyo, ametaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini zaidi, hasa kuhakikisha vinawekeza kwenye kuzuia, badala ya kusubiri matukio yatokee ili kuyakabili.

Katika hilo, amesema wananchi wana wajibu wa kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mapema pale wanapoona kuna tukio linakaribia.

Kwa upande wa jamii, amesema ni wadau wa kwanza kuhakikisha usalama wa watu na mali zao kwa sababu idadi ya askari haikidhi mahitaji ya ulinzi wa watu wote.

Alipoulizwa msimamo wake kuhusu yanayoendelea Ngorongoro, wakili huyo amesema kwa kuwa mgogoro kati ya wananchi na mamlaka hiyo ya hifadhi umedumu tangu miaka ya 1990, kuna haja ya pande mbili kufanya mazungumzo.

“Natamani kuona pande mbili zinakaa kujadili kuona kwa nini jambo hili halifiki mwisho na angalau kuwepo na maelewano,” amesema.

Amesema baraza la uongozi la TLS limetoa tamko na kwamba anaunga mkono kuwa yafanyike mazungumzo, angalau wananchi wapate taarifa na kupatikana maelewano ya pande zote.

Maadhimisho ya Bavicha kuzuiwa

Alipoulizwa kuhusu kuzuiwa kwa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Nkuba amesema kama waliomba kibali na kuruhusiwa, walipaswa waachwe wafanye maadhimisho hayo.

Nkuba ambaye ni kada wa CCM aliyewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho mwaka 2015 hadi 2020, amesema kama kuna sababu zinazoitwa za kiintelejensia, jeshi hilo linapaswa kuzitaja.

“Chombo kama Polisi kuzuia, inapaswa sababu zisiwe za jumla kunapaswa kuelezwe wazi sababu ya kina. Watu wanapoandaa mkutano wanakuwa wametumia gharama kubwa.”

“Nadhani msingi wa kisheria ni hawa kukaa pamoja na kuzungumza kwamba katika hiki mnachotaka kukifanya kuna tishio moja au mbili, sasa tushirikiane namna ya kuzuia,” amesema.

Ameeleza haki hiyo ipo kikatiba na sheria zinatungwa kwa ajili ya kuhakikisha inalindwa.

Hata hivyo, Nkuba haoni sababu ya wakurugenzi wa halmashauri kutiliwa shaka juu ya kuusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa, ingawa vyama vya upinzani vina haki ya kulalamika.

Hoja yake hiyo inatokana na kile alichofafanua, Mkurugenzi anapokwenda kusimamia uchaguzi anaapa na kiapo hicho kinaondoa unasaba wake na Serikali na nafasi yake ya uteuzi.

Hata hivyo, ameelezea mabadiliko ya jina la tume na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), akisema yataongeza ufanisi katika utendaji ndani ya watumishi wake.

“Mabadiliko ya jina la tume yatamfanya hata anayefanya kazi ndani ya tume kuhakikisha anasimamia jambo bila kuingiliwa,” amesema.

Sambamba na hayo, Nkuba aliulizwa iwapo ana nia ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwakani kama ilivyokuwa mwaka 2015, amesema ni mapema kutangaza nia.

Amesema kwa kuwa utaratibu wa chama chake CCM unataka mbunge aliyepo kwenye nafasi aachwe afanye kazi kipindi chake chote, naye analifuata hilo.

“Bunge litakapovunjwa, ukiniuliza Nkuba unakwenda kugombea na wapi hapo nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kueleza. Lakini sio sasa,” amesema.

Related Posts