COASTAL Union iko katika mazungumzo ya mwisho ya kuachana na kocha mkuu, David Ouma kwa kile kinachoelezwa viongozi hawaridhishwi na mwenendo wa matokeo inayoyapata.
Taarifa za ndani zilizonazwa na Mwanaspoti zinaeleza kwamba, Coastal baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Bravos do Maquis ya Angola katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Afrika, ilimtaka Ouma kueleza sababu za kipigo.
“Wakati tumetoka Angola kuja Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa marudiano, Ouma alitakiwa kuleta ripoti kutokana na matokeo tuliyopata, japo ni njia tu ya kumuondoa kwa sababu hawana imani naye,” kilisema chanzo.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Coastal Union, Abbas Elsabri alisema kwa sasa viongozi wameweka nguvu katika mchezo wa leo wa marudiano ili wafanye vizuri, kisha baada ya hapo watazunguza.
Ouma alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia hilo alisema kuna changamoto kidogo ambazo zimejitokeza ingawa bado yupo na timu.
Licha ya kauli hizo, lakini Mwanaspoti linatambua kwamba hayupo na timu kwa sasa kwani tayari ameitwa Tanga na viongozi wa kikosi hicho ili kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuhusu suala la kuvunja mkataba.
Wakati viongozi wakiwa katika mazungumzo hayo, Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba, timu hiyo itakuwa chini ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Lazaro aliyerejeshwa akisaidiana na kocha msaidizi, Ngawina Ngawina.
Ouma alijiunga na Coastal Novemba 9, 2023 akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho na mkurugenzi wa Programu za Vijana, Mwinyi Zahera aliyejiunga na Namungo huku akizifundisha timu za Sofapaka, Mathare United na Posta Rangers.
Kocha huyo aliyetawala soka la Kenya kwa zaidi ya miaka 21 akiwa na leseni ya UEFA, CAF A na uzoefu kutoka kituo cha michezo cha Ajax Amsterdam cha Uholanzi, amewahi pia kufundisha timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ chini ya Bobby Williams.
Uzoefu wake umeiwezesha Coastal Union kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu iliposhiriki mara ya mwisho na kuishia raundi ya kwanza mwaka 1989.