Mke, mtalaka wanusurika kifo, mauaji ya mume mpya

Arusha. Mahakama ya Rufani iliyoketi Tabora, imewaachia huru Akizimana Buchengeza na Perajia Mawenayo (watalaka) waliohukumiwa adhabu ya kifo, kwa kumuua Augustino Ndisabila (mume mpya wa Perajia) na kumkata uume wake.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa warufani hao walikuwa mke na mume zamani, ila walitengana.

Pia ilielezwa kuwa Perajia na Augustino (marehemu) kabla ya kutengana, walikuwa na mgogoro wa kutaka kutengana kisa marehemu anadaiwa alikula chakula kwa mke wa pili.

Katika rufaa hiyo ya jinai namba 43 ya mwaka 2022, watalaka hao walikuwa wakipinga hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Desemba 17, 2021.

Uamuzi wa rufaa hiyo ulitolewa Agosti 22, 2024 na jopo la majaji watatu, Patricia Fikirini, Shaban Lila na Panterine Kente.

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili za rufaa, majaji hao waliondoa kwenye kumbukumbu za rufaa maelezo ya onyo ya Akizimana na Perajia, kuruhusu rufaa, kufuta hukumu na adhabu ya kunyongwa hadi kufa iliyokuwa imetolewa dhidi yao.

Jaji Lila alisema baada ya kufutwa kwa vielelezo hivyo, ushahidi unaobaki kwenye kesi hiyo unaonekana kuwa ulifikiriwa kuwahusisha warufani hao na mauaji hayo, lakini haikufuatiliwa zaidi ili kuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika pasipo kuacha shaka.

Akizimana na Perajia, walidaiwa Juni 25, 2017, saa moja asubuhi katika Kijiji cha Ulyankulu Wilaya ya Urambo Mkoa wa Tabora, walimuua Augustino na kushitakiwa chini ya kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Siku ya tukio, Perajia anadaiwa kusikika akilia kuomba msaada na mashahidi walipofika eneo la tukio, walikuta amekaa nje ya nyumba hiyo na kudai walivamiwa na watu wasiojulikana ambao walimshambulia na kumuua mumewe.

Mashuhuda hao walidai kwamba waliuona  mwili wa marehemu umelala kwenye dimbwi la damu ndani ya chumba hicho huku ukiwa na majeraha ya kukatwa mkononi, shingoni, kifuani na sehemu zake za siri zikiwa zimekatwa na kuondolewa.

Shahidi wa nne na tano (Mikas Kabula na Turundiko Salvatory), katika ushahidi wao, walidai kufahamu kuwa Perajia na marehemu walikuwa na uhusiano wenye mgogoro na shahidi wa nne alidai marehemu alitaka kutengana na Perajia.

Mikas alidai kwa kuwa marehemu alikuwa na wake wawili, kulikuwa na ugomvi baina yake na Perajia baada ya marehemu kwenda kula chakula kwa mke wake mwingine.

Ushahidi mwingine ulitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ulyankulu, Chilemba Chikawe ambaye aliandika maelezo ya ziada ya warufani walipopelekwa kwake na polisi wawili,

yalipingwa na mawakili wa utetezi na kufanikiwa, yalishindwa kutaja tarehe na saa ya kukamatwa Perajia na Akizimana.

Akizimana alidai kuwa alikamatwa nyumbani kwake na Polisi jamii huku akikana kumjua Perajia.

Perajia alidai kuishi na marehemu kama mume na mke kwa kipindi cha miaka mitano na kudai walikuwa na migogoro kwa sababu marehemu alikuwa akimpiga kila mara akimkosa nyumbani, ingawa  mzozo huo haukumfanya amuue mumewe.

Alidai siku ya tukio, walivamiwa na watu wawili wakiwa na panga lakini alikana kumfahamu Akizimana na kupanga naye mauaji hayo na kuhusu maelezo ya onyo, alikana na kudai aliteswa hadi akazirai ili akiri.

Katika rufaa yao, washitakiwa hao  waliwakilishwa na Wakili Saikon Justin huku wakiwa na hoja nne ikiwemo ya jaji kukosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu, kwa kuzingatia vielelezo vya tatu na nne ambavyo havikuorodheshwa wala kusomwa katika mwenendo wa shauri la kesi hiyo.

Hoja nyingine walidai jaji alikosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu kulingana na kielelezo cha nne ambacho kilikubaliwa kimakosa kuwa ushahidi.

Upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali mwandamizi, Upendo Malulu ambaye aliunga mkono rufaa hiyo.

Mawakili wa pande zote mbili hawakuwa na maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashitaka yanayowahusisha warufani na kutenda kosa na kuwa, hukumu ya warufani ilitokana na maelezo yao wenyewe ya onyo.

Wakili wa warufani aliitaka Mahakama ikubaliane naye kwamba vielelezo hivyo viwili vilitolewa kimakosa na kukubaliwa kuwa ushahidi wakati havikuorodheshwa kuwa miongoni mwa vielelezo.

Wakili huyo alisema endapo vielelezo hivyo vitafutwa kwenye kumbukumbu ya rufaa hiyo upande wa mashitaka unabaki bila ushahidi mwingine unaowahusisha warufani na mauaji ya Agustino, hivyo aliomba rufaa ikubaliwe.

Wakili Upendo alikubali upungufu ulioelezwa na wakili wa warufani na kueleza kufutwa kwa vielelezo hivyo kwenye kumbukumbu kunasababisha kesi ya mashitaka kushindwa kuthibitika na kuwatia hatiani.

Jaji Lila alisema utaratibu wa mashauri yaliopo Mahakama Kuu ni kwamba, ushahidi wote ikiwemo nyaraka au maelezo ya mashahidi watarajiwa lazima yaelezwe kwa mshitakiwa na orodha ya vielelezo ili mshitakiwa afahamu anayokabiliana nayo, wakati wa usikilizwaji wa kesi na kumpa nafasi ya kuandaa utetezi wake.

Alisema kifungu cha 289(1) na (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinakataza ushahidi ambao haujaorodheshwa na kiini chake ambacho hakijasomwa kwa mshitakiwa wakati wa shauri kuingizwa kwenye ushahidi.

Jaji Lila alisema wamejiridhisha hakuna taarifa iliyoandikwa na mwendesha mashitaka ya kumtaka aitwe shahidi wa ziada, na kuwa ushahidi wa shahidi aliyewasilisha vielelezo hivyo ulichukuliwa kinyume na sheria hivyo kuufuta ushahidi huo.

Mbali na kufuta ushahidi huo, majaji hao walifuta vielelezo vya tatu na nne kwenye kumbukumbu za rufaa ambavyo vilikuwa ni maelezo ya onyo ya warufani hao.

Jaji Lila alisema baada ya kufutwa kwa vielelezo hivyo ushahidi unaobaki kwenye kesi hiyo unaonekana kuwa ulifikiriwa kuwahusisha warufani hao na kifo cha marehemu, lakini haikufuatiliwa zaidi ili kuthibitisha kwa kiwango kinachohitajika pasipo shaka.

Related Posts