Miili mingine yafukuliwa kwa mganga, ulinzi waimarishwa

Singida. Baada ya kuzuka kwa taharuki ya miili mingine kufukuliwa katika nyumba ya mganga wa kienyeji mkoani Singida, Jeshi la Polisi mkoani humo limeimarisha ulinzi katika eneo hilo, huku miili hiyo ikifikia mitatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale alieleza hayo leo Jumapili Agosti 25, 2024 alipozungumza na wananchi, akisema eneo hilo litakuwa chini ya Jeshi la Polisi mpaka taratibu zote zitakapokamilika.

Amesema miili mingine iliyofukuliwa imeshindwa kutambulika, hivyo kitakachofanyika ni kuipima vinasaba, ili ndugu waliopotelewa na ndugu zao waweze kuitambua.

“Tukishachukua sampuli za miili hii na ndugu ambao walipotelewa, tutafanya uchunguzi wa vinasaba vinavyoweza kututambulisha jinsia ya mwili mmoja na mwingine. Kwa sasa si rahisi kutambua. Pia kuanzia sasa na kuendelea eneo hili litakuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi,” amesema Kamanda Kakwale.

Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha amesema katika maeneo yao wameingia waganga wa kienyeji maarufu kama lambalamba ambao hujitafutia fedha kwa njia zisizo halali.

Ameongeza kuwa kulingana na hali ilivyo, kuna uwezekano wa kuwapo miili zaidi ya iliyopatikana katika eneo hilo, hivyo ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kufanya uchunguzi zaidi.

“Huyu mganga si mzaliwa wa hapa Singida,  lakini amekuja kuchukua akili za wananchi hata walipoanza kupoteza ndugu zao hawakushtuka kwa sababu inaonekana kuna miili zaidi ya hawa, waendelee kutafutwa mpaka wapatikane,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuki Stephano, mkazi wa kijiji cha Makulo amesema wananchi wanaumizwa na yanayotokea katika eneo lao na kusema si mara ya kwanza kutokea, hivyo wanaiomba Serikali kuimarisha ulinzi kwa kujenga kituo cha polisi katika kata yao.

“Serikali ipo pamoja na wananchi, ila tunaomba tujengewe kituo, wananchi watakapoona kituo kimejengwa Kata ya Makuro na Serikali imeleta askari watakaosimamia amani, wapata faraka. Tunaumia sana kwa haya yanayoonekana katika kijiji chetu,” amesema.

Ndugu wa mganga huyo, Tabu Ramadhani amesema amechukizwa na kitendo kilichotokea kwa  sababu mganga huyo alipohamia katika kijiji chao alipokelewa na kaka yake na kwamba mara kadhaa amekuwa akimfanyia ubaya.

Kwa upande wake, Husna Moses amesema tukio hilo linamhuzunisha na linaogopesha kwa sababu tangu azaliwe hajawahi kushuhudia tukio la namna hiyo.

Mpaka sasa,  miili ya watu watatu imepatikana katika nyumba hiyo ikiwa imefukiwa na mganga huyo na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Makuro na maeneo jirani wakichukizwa.

Tukio hilo limeufanya Mkoa wa Singida kuingiwa na wasiwasi, huku likifananishwa na tukio la mchungaji Paul Makenzi wa Mombasa nchini Kenya ambaye alituhumiwa kwa mauaji, baada ya miili ya watu 429 kupatikana ikiwa imefukiwa katika msitu wa Shakahola.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts