Dar es Salaam. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo wanakutana kwa siku mbili kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwamo migogoro ya ardhi, matukio ya utekaji na matishio ya usalama yanayoendelea kuripotiwa katika maeneo tofauti nchini.
Mbali na hayo, kikao hicho ambacho kimeelezwa kuwa cha kawaida kikatiba, wajumbe pia watajadili mikakati endelevu ya ujenzi wa chama kama sehemu ya maandalizi ya kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho ambacho pia kimehudhuriwa na viongozi na wastaafu wa chama hicho, Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu amesema hoja hizo zinawasumbua wananchi, hivyo zitajadiliwa kwa kina kabla ya kutoka na msimamo wao.
“Tatizo la migogoro ya mipaka imekuwa na athari kubwa kwa wananchi, ikiwemo kunyang’anywa mifugo, mazao, vitisho, vipigo na vifo vya watu (wananchi na askari wa uhifadhi).
Akitolea mfano maeneo yenye migogoro ya ardhi, Semu ametaja ni pamoja na Mbarali, Ngorongoro, Kasulu, Uvinza, Loliondo, Kaliua na Kilwa.
“Mtakumbuka hali ilivyo sasa huko Ngorongoro. Takribani nusu karne wananchi jamii ya kimasai katika Tarafa ya Ngorongoro na Loliondo wamekuwa wakiishi katika mashaka kwenye ardhi yao,”amesema kiongozi huyo.
Amesema viongozi wao kupitia baraza kivuli la mawaziri wako mstari wa mbele kusimama na wananchi wa Ngorongoro na maeneo mengine kulinda haki yao ya ardhi.
“Tunaendelea kuitaka Serikali kuruhusu haki ya ardhi kwa wananchi wa Ngorongoro, tunaitaka ibatilishe tangazo haramu na 673 la 2024. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ivunjwe na iundwe kampuni yenye ushiriki na umiliki wa ubia kati ya Serikali na wananchi,”amesema.
Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta tena Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba azungumzie hoja hizo za ACT Wazalenda kuhusiana na migogoro ya ardhi, lakini muda mwingi simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Hata hivyo, kuhusiana na hili la Ngorongoro, itakumbukwa Agosti 23,2024 mawaziri watatu, akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Danstan Kitandula walipeleka ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wa Ngorongoro walioandamana kwa siku tano.
Waziri Lukuvi alisema Rais amepanga kukutana na wawakilishi wa wananchi hao, huku akibainisha utaratibu wa kufanya hivyo unaandaliwa ili wakawasilishe kero zao.
“Rais ametutuma tuje tuwasilishe kwamba, haki yenu kupiga kura katika uchaguzi huu iko pale pale, mkurugenzi ambaye ndiyo msimamizi wa uchaguzi vituo vyote vilivyopangwa kwa melekezo ya Rais vifunguliwe na vifanye kazi yake,”alisema Lukuvi.
Kwa upande wake, Profesa Kabudi alisema Watanzania wote wako sawa na aliwahakikishia kwamba watapata haki sawa na maeneo mengine.
Semu amesema hivi karibuni kumeibuka wimbi la matukio ya utekaji, kupotea na mauaji ya raia, hasa wananchi wanaonekana kuikosoa Serikali au wanaohoji matukio yasiyofaa kuhusu viongozi wa Serikali.
“Watanzania wameanza kuingiwa tena na hofu kukithiri kwa matukio haya. Inasikitisha zaidi kuona watu wa kwanza wanaohusishwa na matukio haya ni Jeshi la Polisi na baadhi ya matukio wananchi wanalalamikia Polisi kutochukua hatua za haraka kwa wanaohusika,” amesema.
Amesema chama hicho kinalaani na kutaka hatua madhubuti kuchukuliwa na kusukuma madai ya mageuzi ya Jeshi la Polisi hasa kutoruhusu kutumika kisiasa.
“Jeshi la Polisi linapaswa kuwa taasisi huru inayojiendesha kwa weledi bila kusukumwa na upande mwingine,” amesisitiza kiongozi huyo wa chama.
Agosti 24, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa kwa umma akitoa angalizo kwa baadhi ya watu wanaozungumzia matukio ya aina hiyo watumie majukwaa yao kwa uangalifu, kwani sababu wanazotoa ni kutaka kubadilisha ukweli wa yanayoendelea ndani ya jamii ili kuleta taharuki na uhasama.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Akizungumzia hoja ya uchaguzi, Semu amesema itaangaziwa kwa ukubwa, huku akieleza wanatakiwa kujipanga ili kushinda viti vingi kama dira ya kujipanga na uchaguzi mkuu.