Ukraine yaitaka Belarus kuondoa wanajeshi wake mpakani – DW – 26.08.2024

Wizara ya mambo ya nje ya Ukraine imeionya Belarus dhidi ya kufanya “makosa ya kusikitisha” wakati ikishinikizwa na Urusi.

Taarifa ya wizara hiyo imevihimiza vikosi vya jeshi la Belarus kuacha vitendo visivyo vya kirafiki na kuondoa wanajeshi wake mpakani.

Wizara hiyo imeendelea kueleza kuwa, vikosi maalum vya jeshi la Belarus pamoja na wapiganaji wa zamani wa kundi la mamluki la Urusi Wagner walikuwa miongoni mwa wanajeshi walioko mpakani.

Soma pia: Belarus, Urusi zakagua silaha za kimkakati za nyuklia

Miongoni mwa zana za vita za Belarus ni pamoja na vifaru, makombora, mifumo ya ulinzi wa anga na vifaa vya uhandisi vilivyopelekwa katika mkoa wa Gomel karibu na mpaka wa Ukraine upande wa kaskazini.

Taarifa hiyo imesema Ukraine haijawahi kuchukua na haina nia ya kuchukua hatua yoyote isiyo ya kirafiki dhidi ya watu wa Belarus.

Belarus Stationierung von russischen Atomwaffen
Rais wa Belarus Alexander Lukashenko(kushoto) na Rais wa Urusi Vladmir Putin wakikumbatiana wakati wa mkutano wao uliofanyika kwenye Ikulu ya Kremlin mjini Moscow.Picha: Pavel Byrkin/Sputnik/AP/picture alliance

Mnamo Agosti 18, Rais wa Belarus Alexander Lukashenko alisema kuwa Ukraine ilipeleka zaidi ya wanajeshi 120,000 kwenye mpaka wa nchi hizo mbili.

Mamlaka nchini humo imesema leo kuwa imetuma ndege, vikosi vya ulinzi wa anga na vifaru vya kivita kwenye mpaka wake na Ukraine.

Soma pia: Poland yaiomba Belarus kuwafukuza Wagner 

Belarus ambayo inashirikiana na Urusi, haijihusishi moja kwa moja na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Hata hivyo, Lukashenko aliruhusu wanajeshi wa Urusi kuingia Ukraine kupitia Belarus wakati wa uvamizi wake mnamo Februari 2022.

Baada ya kushindwa na kupata hasara kubwa wakati wa jaribio la kusonga mbele na kuelekea mjini Kyiv, vikosi vya Urusi hatimaye vililazimika kujiondoa.

 

Related Posts