Gamondi ashtukia ishu nzito, atangaza vita mpya

KOCHA wa Yanga Miguel Gamondi  amesema matokeo ya ushindi wa jumla wa mabao 10-0 iliyopata timu hiyo kwake yameshapita na sasa akili zake ni kwenye mechi mbili za raundi ya pili dhidi ya CBE ya Ethiopita akiitangazia vita kwa lengo la kutaka kuvunja mwiko ulioitesa vijana wa Jangwani.

Yanga imekuwa na rekodi mbovu dhidi ya timu za Ethiopia katika mechi za Caf hasa zile za ugenini, lakini Gamondi alisema baada ya kuwanyoosha Vital’O ya Burundi kwa mabao 6-0 juzi waliporudiana nao na kuifanya ivuke raundi ya kwanza kwa mabao 10-0, awali ikiifunga 4-0 wanaelekeza nguvu kwa Waethiopia.

Timu kwa sasa imepangwa kukutana na Commercial Bank ya Ethiopia (CBE) iliyoing’oa SC Villa ya Uganda kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya mechi ya kwanza kushinda ugenini 2-1 na juzi ikiwa nyumbani kutoka sare ya bao 1-1 na michezo ya raundi ijayo zitachezwa kati Septemba 13-15 na Septemba 20-22.

Washindi wa mechi za hatua hiyo moja kwa moja hutinga makundi ambayo Yanga ilicheza msimu uliopita ikiwa ni baada ya miaka 25.

Kwa mara ya kwanza Yanga ilikutana na Waethiopia mwaka 1969 katika mechi ya Klabu Bingwa(sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) na kuitoa Saint-George kwa jumla ya mabao 5-0, iliyoshinda ikiwa nyumbani na ile ya ugenini ikiisha kwa suluhu na kusonga hadi robo fainali.

Mwaka 1998 michuano iliyobadilishwa mfumo, ikaitoa Coffee FC katika mechi za mtoano wa Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 8-3, ikitoka sare ya 2-2 ugenini na kushinda nyumbani mabao 6-1 na kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Yanga ilianza kukutana na timu kutoka Ethiopia mwaka 2011 na kutolewa na Dedebit kwa jumla ya mabao 6-4, baada ya kulazimishwa sare ya 4-4 nyumbani kisha kulala ugenini kwa mabao 2-0.

Mwaka 2018, Yanga ikakutana tena na Welaita Dicha ya Ethiopia katika Kombe la Shirikisho Afrika kusaka tiketi ya makundi ambapo ilishinda kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya mchezo wa kwanza kushinda 2-0 nyumbani kisha kuchapwa 1-0 ugenini.

Rekodi hizo zipo mezani mwa Gamondi na akizungumza na Mwanaspoti Gamondi alisema, kwa sasa anajivunia aina ya kikosi alichonacho ingawa hawezi kuacha kutoa pongezi kwa wapinzani, Commercial Bank kwa kiwango kizuri walichokionyesha baada ya kuwafuatilia michezo yao miwili dhidi ya SC Villa.

“Ni timu nzuri ambayo haijafika hatua hii kwa bahati mbaya, tunahitaji kujipanga vizuri kwa sababu hautokuwa mchezo mwepesi, kila mmoja wetu kwa sasa ana furaha na matokeo tuliyoyapata ingawa tuna kazi kubwa huko mbeleni,” alisema Gamondi aliyesema kiu yake ni kuona timu inafuzu makundi tena.

Kwa upande wa Rais wa Yanga Injinia Hersi Said alisema katika mchezo wao wa marudiano utakaopigwa kati ya Septemba 20 hadi 22, hapa nyumbani wamepanga kutumia Uwanja wa New Amaan Complex ili kuwapa fursa mashabiki wao waliopo Zanzibar.

“Malengo yetu ni kuendelea kuipeleka timu yetu karibu na wanachama na mashabiki wake kote nchini hivyo baada ya mechi hii ya awali kucheza hapa Dar es Salaam, kwa sasa raundi ya pili tunatarajia kuchezea kule visiwani Zanzibar,” alisema.

CBE ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchukua ubingwa wa kwao kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe 1982.

Timu hiyo imeshiriki mara mbili michuano ya Afrika ambapo mara mbili ilicheza Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa katika hatua ya mtoano miaka ya 2005 na 2010, kisha msimu huu kuandika historia mpya kwa kushiriki Ligi ya Mabingwa.

Related Posts