MAKOSA ya safu ya ulinzi ya Simba Queens jana yalichangia kwa kiasi kikubwa ipoteze mchezo wa nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kwa wanawake dhidi ya Police Bullets ya Kenya na kushindwa kufuzu Klabu Bingwa Afrika mwaka huu.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Abebe Bikira huko Ethiopia, Simba Queens ilipoteza kwa mabao 3-2.
Bao la kwanza la Police Bullets lilitokana na kosa la kipa Rufa Carolyne kuponyokwa na mpira wa krosi mkononi na kuuangushia kwa Lucy Jira ambaye aliukwamisha kimiani katika dakika ya 29.
Licha ya Simba Queens kujitutumua na kusawazisha bao katika dakika ya 38 na kupata bao la pili katika dakika ya 56 yote yakifungwa na Vivian Aquino, safu yake ya ulinzi ilifanya tena kosa la kutoruka kuokoa mpira wa kona na kumruhusu Diana Wacera kufunga bao la kusawazisha la Police Bullets katika dakika ya 61.
Kukosa mawasiliano baina ya mabeki na kipa wa Simba Queens, kuliipa faida Police Bullets kupata bao la tatu na la ushindi katika dakika 82 kupitia kwa Rebecca Akinyi ambaye alitumia vyema udhaifu kuwatoka walinzi wawili wa Simba Queens na kuujaza mpira kimiani.
Ni kama ilikuwa ni mwendelezo wa udhaifu wa safu ya ulinzi ya Simba Queens kuruhusu mabao kizembe baada ya kufanya hivyo katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya PVP Buyenzi ya Burundi ilipofungwa mabao mawili na mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kwa matokeo ya jana, Simba Queens imeshindwa kufuzu Klabu Bingwa Afrika kwa wanawake kwani ni timu moja ambayo inapata fursa hiyo kwa kila kanda ya soka Afrika ambayo ni ile inayotwaa ubingwa wa kanda. Simba Queens iliwahi kushiriki klabu bingwa Afrika mwaka 2022 na kumaliza katika nafasi ya nne.