Kuwasili polepole kwa chanjo – ambazo tayari zimepatikana katika zaidi ya nchi 70 nje ya Afrika – kumeonyesha kuwa mafunzo yaliyopatikana kutokana na janga la UVIKO-19 kuhusu ukosefu wa usawa wa huduma za afya duniani yamechelewa kuleta mabadiliko, maafisa wa afya ya umma na wanasayansi wamesema.
Miongoni mwa vikwazo: Ililichukua Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi mwezi Agosti kuanza rasmi mchakato unaohitajika kuzipa nchi maskini upatikanaji rahisi wa kiasi kikubwa cha chanjo kupitia mashirika ya kimataifa. Hilo lingeanza miaka iliyopita, maafisa kadhaa na wanasayansi waliliambia shirika la habari la Reuters.
Mpox ni maambukizi hatari yanayosababisha dalili kama za mafua na vidonda vilivyojaa usaha na huenea kwa mguso wa karibu wa kimwili. Ilitangazwa kuwa dharura ya afya ya umma duniani na WHO mnamo Agosti 14 baada ya aina hiyo mpya, inayojulikana kama clade Ib, kuanza kuenea kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi nchi jirani za Afrika.
Likijibu maswali ya Reuters kuhusu kucheleweshwa kwa kupelekwa kwa chanjo, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, lilisema siku ya Ijumaa kuwa litalegeza baadhi ya taratibu zake safari hii katika juhudi za sasa kuharakisha upatikanaji wa chanji cha mpox kwa mataifa maskini.
Soma pia: Bado kuna maswali muhimu yanahitaji majibu kuhusu Mpox
Kununua chanjo hizo ghali moja kwa moja ni jambo gumu kwa mataifa mengi maskini. Kuna chanji mbili muhimu za mpox, zilizotengenezwa na makapuni ya dawa ya Bavarian Nordic ya nchini Denmark na KM Biologics ya Japan. Dozi ya chanjo ya Bavarian Nordic inagharimu dola za Marekani 100, bei ya dozi ya KM Biologics haijulikani.
Subira ya muda mrefu ya idhini ya WHO kwa mashirika ya kimataifa kununua na kusambaza chanjo hiyo kumelazimisha serikali moja mmoja za Afrika na kituo cha kuzuwia na kupambana na magonjwa barani humo – Africa CDC – badala yake kuomba misaada ya chanjo kutoka mataifa tajiri. Mchakato huo mzito unaweza kuporomoka, kama ilivyokuwa hapo awali, ikiwa wafadhili wanahisi wanapaswa kuhifadhi chanjo ili kulinda watu wao.
Dozi 10,000 za kwanza ziko njiani kwenda Afrika – zikiwa zimetangenezwa na kampuni ya Bavarian Nordic – zimetolewa msaada na Marekani, na siyo mfumo wa Umoja wa Mataifa.
Helen Rees, mjumbe wa kamati ya dharura ya Afrika CDC kuhusu mpox, na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Wits RHI mjini Johannesburg, Afrika Kusini, alisema “inachukiza kweli” kwamba, baada ya Afrika kuhangaika kupata chanjo wakati wa janga la COVID, eneo hilo bado limeachwa tena nyuma.
Mnamo mwaka wa 2022, baada ya aina tofauti ya kirusi cha mpox kuenea nje ya Afrika, chanjo za mpox zilitumiwa tena na serikali ndani ya wiki chache, zilkiidhinishwa na wadhibiti na kutumika katika takriban nchi 70 za kipato cha juu na cha kati kulinda wale walio hatarini zaidi.
Chanjo hizo sasa zimewafikia watu milioni 1.2 nchini Merika pekee, kulingana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, CDC. Lakini hakuna chanjo zilizoifikia Afrika nje ya majaribio ya hospitali. Sababu kuu: Chanjo zilihitaji kuidhinishwa na WHO kabla ya kununuliwa na mashirika ya huduma ya afya ya umma, yakiwemo Gavi, ambao ni muungano wa Chanjo.
Soma pia: WHO: Homa ya Nyani ni dharura ya afya ya umma duniani
Gavi huyasaidia mataifa maskini kununua chanjo, kwa kutoa chanjo za utotoni kwa njia hii mara kwa mara. Ilisimamia mpango wa kimataifa wa chanjo zote wakati wa UVIKO-19 na ina hadi dola milioni 500 za kutumia kwa chanjo ya mpox na vifaa. CDC ya Afrika imesema dozi milioni 10 huenda zikahitajika katika bara zima.
Lakini WHO mwezi huu pekee iliwataka watengenezaji chanjo kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa chanjo za mpox kupokea leseni za dharura – ambazo ni idhini iliyoharakishwa ya WHO kwa bidhaa za matibabu. Ilizitaka nchi kuchangia chanjo hadi mchakato huo ukamilike, mnamo Septemba.
WHO ilisema inashirikiana na mamlaka nchini Kongo kuweka pamoja mpango wa chanjo, na Ijumaa ilisema Gavi anaweza kuanza mazungumzo huku ikikamilisha kibali chake cha dharura.
Sania Nishtar, afisa mtendaji mkuu wa Gavi, alisema lengo la WHO sasa kuchukua hatua haraka juu ya idhini na uboreshaji wa ufadhili inaonyesha “upande mzuri zaidi wa mahali tulipo tukilinganishwa na UVIKO.” Alipoulizwa kutoa maoni juu ya ucheleweshaji wa idhini, alisema, “natumai huu ni wakati mwingine wa kujifunza kwetu.”
WHO yakosolewa kwa kujikongoja
Jukumu la WHO katika kuidhinisha bidhaa za matibabu limeleta mapinduzi makubwa ya ugavi katika nchimaskini, ambazo mara nyingi hazina vifaa vya kukagua bidhaa mpya zenyewe, lakini pia limekabiliwa na ukosoaji kwa kasi yake ndogo na ugumu.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa lenye makao yake mjini Geneva, lilisema siku ya Ijumaa halikuwa na data za kutosha wakati wa dharura ya mwisho ya mpox mwaka 2022, ili kuanza mchakato wa kuidhinisha chanjo hiyo, na limekuwa likifanya kazi na watengenezaji tangu wakati huo ili kuona ikiwa data zinazopatikana zinawezesha kutolewa idhini.
Mpox, ambayo inajumuisha aina kadhaa tofauti, imesababisha visa 99,000 vilivyothibitishwa na vifo 208 ulimwenguni tangu 2022, kulingana na WHO. Huenda hesabu hiyo ni ya kukadiria kwani visa vingi haviripotiwi. Maambukizi yamedhibitiwa katika maeneo tajiri kwa mchanganyiko wa chanjo na mabadiliko ya tabia miongoni mwa makundi yaliohatarini zaidi.
Pamoja na aina kuu ya awali ya kirusi cha mpox, wanaume wanaojamiiana na wanaume walikuwa hatarini zaidi, lakini aina mpya ya clade Ib inaonekana kuenea kwa urahisi kupitia mawasiliano mengine ya karibu, ikiwa ni pamoja na miongoni mwa watoto, na pia kupitia kujamiiana kati ya watu wa jinsia tofauti.
Nchi ambayo kwa sasa imeathirika zaidi na mpox ni Kongo. Tangu Januari 2023, kumekuwa na zaidi ya visa 27,000 vinavyoshukiwa na vifo 1,100 nchini humo, kulingana na takwimu za serikali, hasa miongoni mwa watoto.
Soma pia: Ulaya kuzalisha chanjo zaidi za ugonjwa wa homa ya nyani
Lakini chanjo 10,000 za kwanza zilizotolewa na Marekani hazikupelekwa Kongo bali Nigeria, kutokana na mazungumzo ya miaka kadhaa kati ya serikali zote mbili, kulingana na chanzo kilichohusika katika mchakato huo ambacho hakikuidhinishwa kuzungumza na vyombo vya habari. Nigeria imekuwa na visa 786 vinavyoshukiwa mwaka huu, na hakuna vifo.
Wizara ya afya ya Nigeria haikujibu ombi la maoni; Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani, USAID, limesema pia limetoa dozi 50,000 kwa Kongo lakini tarehe ya kuwasili bado haijakamilika.
Watoto wako hatarini
Nchini Kongo, utawala wa nchi hiyo ni sehemu nyingine ya tatizo. Ikikabiliana na mizozo na milipuko mingi ya magonjwa, serikali yake bado haijaiomba rasmi Gavi kuipatia chanji, na ilichukua miezi kuzungumza na serikali wafadhili. Mamlaka yake ya uidhibiti wa dawa iliidhinisha chanjo mbili kuu mwezi Juni tu.
Si wizara ya afya ya Kongo wala ya Japani, ambayo inashughulikia kiasi kikubwa cha chanjo za KM Biologics, iliyojibu maombi ya maoni kwa ajili ya makal hii. Bavarian Nordic ilisema wiki hii inahitaji uagizaji sasa ili kutoa chanjo kwa kiasi kikubwa mwaka huu.
Serikali ya Kongo imewaambia waandishi wa habari kuwa inatarajia kupokea msaada wa chanjo wiki ijayo, lakini vyanzo vitatu vya wafadhili vimeiambia Reuters kuwa haijabainika iwapo hilo litafanyika. Mamlaka ya utayarifu kwa ajili ya majanga ya Ulaya ilisema kwa barua pepe kwamba dozi zake 215,000 hazitawasili Kongo kabla ya Septemba.
Bavaria Nordic na Kongo bado zinajadiliana kuhusu masharti ya kabla ya usafirishaji wa chanjo, ambayo ni muhimu kuhakikisha uhifadhi na ushughulikia sahihi, alisema msemaji wa shirika la USAID. Kwa mfano, chanjo hizo zinapaswa kuhifadhiwa kwa kiwango cha baridi cha nyuzi -20C.
Mashariki mwa Kongo, karibu watu 750,000 wanaishi katika kambi baada ya kukimbia vita, akiwemo Sagesse Hakizimana mwenye umri wa miaka saba na mama yake Elisabeth Furaha. Yeye ni mmoja wa zaidi ya watoto 100 walioambukizwa mpox katika eneo moja karibu na mji wa Goma, Kivu kaskazini, kulingana na madaktari.
Soma pia: Tanzania yaimarisha hatua za kuzuia maambukizi ya Mpox
“Hebu fikiria unakimbia vita kisha umpoteze mtoto wako kutokana na ugonjwa huu,” alisema Furaha, 30, wakati akimpaka mafuta kwenye vipele mwanawe na kuongeza kuwa dalili zake zinapungua. Alikuwa akitibiwa wiki iliyopita katika kituo cha Ebola kilichobadilishwa matumizi. “Tunahitaji chanjo kwa ugonjwa huu. Ni ugonjwa mbaya unaowadhoofisha watoto wetu.”
Hata chanjo zikifika, maswali yanasalia kuhusu jinsi ya kuzitumia: Chanjo ya Bavarian Nordic – inayotumika sana duniani kote – inapatikana kwa watu wazima pekee. Chanjo ya KM Biologics inaweza kutolewa kwa watoto lakini ni ngumu zaidi kutumiwa.
Zaidi ya hayo, wanasayansi bado hawajakubaliana ni vikundi gani vinapaswa kupewa chanjo kwanza, ingawa mkakati unaowezekana ni chanjo ya pete, ambapo watu waliotangamana na visa vinavyojuliana hupewa kipaumbele.
“Tuliona wakati wa UVIKO-19, kwamba chanjo hiyo inapatikana lakini watu hawakuitaka,” anasema Jean Jacques Muyembe, mgunduzi mwenza wa virusi vya Ebola na mkurugenzi wa Institut National de Recherche Biomédicale, INRB, mjini Kinshasa.
Yeye na wanasayansi wengine walisema hatua nyingine za afya ya umma kama vile kuongeza uelewa barani Afrika na utambuzi bora pia ni muhimu katika kukomesha kuenea kwa mpox; Chanjo sio suluhisho pekee.
Vipaumbele
Baadhi ya wataalam wa afya duniani wanasema WHO na wengine walipaswa kujikita mapema katika kuboresha upatikanaji wa chanjo ya mpox pamoja na vipimo vya ugonjwa huo na matibabu.
“Michakato [ya WHO kwa ajili chanjo] na ufadhili wa uchunguzi wa mpox unapaswa kuwa umeanza miaka michache iliyopita,” alisema Ayoade Alakija, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa ushirikiano wa afya duniani unaolenga kufanya mwitikio wa mpox kuwa wa usawa zaidi.
Soma pia:Ugonjwa wa Mpox sio janga kama COVID-19
Alisema maoni yake hayakuwa ukosoaji wa WHO, ambayo inaweza tu kuweka kipaumbele kile ambacho nchi wanachama wake wanataka. “Ni suala la ambacho ulimwengu unachukulia kuwa kipaumbele, na [hilo si] magonjwa ambayo kimsingi yanaathiri watu weusi na wa kahawia.”
Katika taarifa yake, WHO ilisema “inawahimiza washirika wote ikiwa ni pamoja na nchi, wazalishaji na jamii kuhamasisha juhudi, kuongeza michango ya chanjo, kupunguza bei na kutoa msaada mwingine muhimu ili kulinda watu walio katika hatari wakati wa mlipuko huu”.
Jean Kaseya, mkuu wa CDC ya Afrika, alisema anafanya kazi kuwashirikisha watengenezaji chanjo barani Afrika ili kuongeza usambazaji na kushusha bei, lakini hilo litachukua muda.