Na Mwandishi wetu
KATIKA kuendeleza kampeni ya kumtua mama mzigo wa kuni kichwani Kampuni ya Taifa Gas imewapatia vijana 50 wajasiriamali mjini Morogoro vifaa vya gesi kupitia mkopo vikiwemo majiko, mtungi wa gesi .
Lengo ni kuwawezesha kuanza matumizi ya nishati safi katika biashara zao
Hatua hiyo ni muendelezo wa jitihada za kampuni hiyo katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kufanikisha upatikanaji wa nishati safi hapa nchini kwa kuiwezesha jamii kuachana na matumizi ya nishati chafu za kupikia na kugeukia nishati safi na endelevu.
“Hii ni sehemu ya jitihada pana zaidi ya Taifa Gas za kupunguza utegemezi wa nishati za jadi kama mkaa na kuni, ambayo ni hatari kwa afya na mazingira. Kwa kurahisisha mpango wa kutumia gesi ya mitungi, Taifa Gas inalenga kuweka kipaumbele cha namna ambavyo vijana wanaweza kushiriki kwa vitendo jitihada za nishati safi na endelevu wakiwa wanafanya biashara zao,” alieleza Angellah Bhoke, Mkuu wa Idara ya Mahusiano ya Umma katika kampuni ya Taifa Gas.
Alisema jitihada za kampuni hiyo hazilengi tu kupunguza athari za mazingira, bali pia kuboresha maisha ya wajasiriamali hao, wanaofanya shughuli za uuzaji wa vyakula kwa kuwaondolea gharama kubwa zitokanazo na nishati zisizo rafiki kibiashara ikiwemo kuni na mkaa ili kuboresha ufanisi wa shughuli zao.
Alisema wnalenga wasafiri katika njia kuu ya Morogoro-Dodoma pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu kilicho maeneo karibu, wajasiriamali hao walipokea vifaa kamili vya mitungi ya gesi ya kupikia yenye uzito wa kg 38kg na majiko ya kisasa tangu mwezi Julai 2023, chini ya mpango wa malipo ya awamu kutoka Taifa Gas.
“Baada ya mwaka mmoja, wanufaika wanakamilisha malipo yao huku wakionyesha mabadiliko makubwa kutokana na uelewa mpya kuhusu matumizi ya nishati safi. Mabadiliko hayo yanatoa mwanga katika utekelezaji mkubwa wa mpango huo, hivi karibuni,” alisema.
Issa Sudi (31), ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mikopo hiyo katika Soko la Msamvu Morogoro alisema “Siwezi kufikiri kuwa kuna mtu yeyote kati yetu ambaye angependa kurudi kutumia kuni au mkaa kwa sababu haya yamekuwa ni mabadiliko halisi. Kwangu mimi, imekuwa mwaka mmoja wa mabadiliko makubwa. Nilikuwa natumia kati ya Sh70,000 na Sh75,000 kununua mkaa, lakini sasa hali si hivyo tena kwa sababu karibu asilimia 90 ya kupika kwangu sasa hufanyika kwa kutumia gesi.”
Issa, ambaye amekuwa muuzaji wa chakula katika Soko la Msamvu kwa takribani miaka 9, anaakiri kuwa juhudi hizi za hivi karibuni za kuwapa wauzaji wa chakula nishati safi ni hatua sahihi.
Yeye ameungana na wanamabadiliko wengine vijana katika juhudi hii, ikiwemo Neema Mnokela, Shadrack Michael, Mawazo Cosmas, na Sharia Mpishi, ambao wamekuwa mfano katika jamii yao, wakionyesha jinsi vijana wanavyoweza kuongoza katika kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.
“Matumizi ya gesi ya kupikia yamenifanya nipike vyakula kwa ufanisi zaidi, kupunguza muda wa kupika na gharama za uendeshaji. Zaidi ya hayo, mabadiliko haya yamesaidia kupunguza idadi ya wafanyakazi wangu na kuwasaidia waliobaki dhidi ya athari za moshi na hewa hatarishi, hivyo kuchangia afya bora kwetu,” alisema Neema Mnokela.
Taifa Gas imekuwa ikisaidia ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia tangu ilipozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mnamo mwaka 2022. Kwa mujibu wa kampuni hiyo Shilingi bilioni 2 zimekuwa zikitumika kupitia Uwekezaji wake wa Kijamii wa Kampuni hiyo ili kusaidia uendelezaji wa kampeni hiyo.
Mipango mingine iliyotekelezwa na kampuni hiyo ni pamoja na kusambaza mtandao wake wa vituo katika kila mkoa pamoja na kuwa na mfumo imara wa usafirishaji ili kuhakikisha gesi ya majumbani inawafikia watu katika kila kona ya nchi.
“Kupitia programu hii ya mikopo, Taifa Gas haiwezeshi tu vijana wa Morogoro, bali pia inaweka mfano wa jinsi biashara zinavyoweza kuchangia maendeleo endelevu na hifadhi ya mazingira, huku ikiboresha maisha ya jamii za wenyeji kwa wakati mmoja,” aliongeza..
Mmoja wa wafanyabiashara wadogo wa vyakula kwenye soko la Msamvu, Morogoro, Halima Kimairo ambae ni mmoja wa wanufaika wa mpango wa ukopeshwaji wa nishati safi ya kupikia kutoka kampuni ya Taifa Gas akiendelea na shughuli zake kwenye soko hilo mwishoni mwa wiki. Mkopo huo ni sehemu ya majaribio kuelekea utekelezaji wa mpango mkubwa wa kampuni hiyo unaolenga kutoa mikopo ya nishati hiyo kwa wajasiriamali 1000 kwenye kila mkoa hapa nchini.