Simiyu. Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amesema hawezi kuvuliwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa sababu tu ya kuwataja hadharani aliowaita mafisadi na wala rushwa kwa kuwa hata chama hicho kimekuwa kikikemea vitendo hivyo.
Mpina kwa sasa anatumikia adhabu ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge, baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumkuta na hatia ya kudharau mamlaka ya Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge.
Mbunge huyo aliyepata umaarufu kwa kuwakosoa mawaziri mbalimbali, alisimamishwa Juni 24, 2024 na anatakiwa kurudi katika Bunge la Novemba 2024.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwaukoli Kata ya Kisesa, Mpina amesema CCM sio pango la wanyang’anyi hivyo kitendo cha kuwasema hadharani mafisadi na kuwatibulia mipango ya kufanya rushwa, dhuluma na wizi, sio sababu ya kumfanya aondolewe katika chama hicho.
“Wengine wamekuwa wakifanya rushwa zao wanakimbilia katika ubavu wa CCM, nani aliyewaambia CCM ni pango la wanyang’anyi?” amehoji.
Amesema chama hicho kimekataa rushwa, dhuluma na wizi katika katiba yake.
“Wengine wanasema Mpina atafukuzwa CCM, hivi jembe kama Mpina lifukuzwe lipelekwe wapi, mimi nifukuzwe kwa kuwasema hadharani wezi?”amehoji.
Aidha, amesema hayupo tayari kunyamaza kimya huku akiona wananchi wanaumia na kudhulumiwa haki na mali zao, kwa uzembe wa viongozi wanaojali masilahi yao binafsi.
“Hatuwezi kuwa na watumishi wa umma ambao wanakiuka utawala bora… kiongozi mkuu kama hachukui hatua maana yake yeye anayaunga mkono hayo.”
Katika hatua nyingine, Mpina amewahimiza wananchi kujitokeza Septemba 4, 2024 jimboni humo katika maboresho ya uandikishaji wa daftari la mpiga kura, akiwataka kuchagua viongozi wenye uwezo wa kusimamia majukumu ya wananchi katika maendeleo.
“Tiketi ya kupiga kura ni kuwa na kadi ya mpiga kura, niwaombe nendeni mkatuchagulie viongozi wazuri, maendeleo yana gharama kubwa, maendeleo ni kujipanga kwa kuchagua viongozi wazuri na kiongozi mzuri anafanana na sisi chagueni kiongozi anayefanana na Mpina na Rais Samia ambao hawatabomoa misingi tuliyoiweka” amesema Mpina.
Akizungumzia kauli za Mpina, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Samweli John amesema anachokifanya mwanasiasa huyo ni kutekeleza majukumu yake kama mbunge.
“Uwepo wa Mpina ndani ya CCM ni kiongozi ambaye anatumia mrengo wa ukosoaji jengefu. Nafikiri anapaswa atumiwe zaidi katika kipindi hiki kwa sababu anasaidia kujenga taswira chanya ndani ya chama hicho na kuwaonesha kwamba wanaweza kukosoana,” amesema
Amesema kuwa jamii imejenga hofu kuwa mtu ambaye anafanya ukosoaji jengefu dhidi ya Serikali, anaonekana adui, kitendo ambacho si sahihi katika jamii inayohitaji maendeleo.