Dar es Salaam. Wahandisi vijana takriban 500 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano lililoandaliwa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) likilenga kuwapiga msasa.
Kongamano hilo la siku mbili kuanzia Septemba 2-3 ni sehemu ya matukio yanayotarajiwa kufanyika kuelekea mkutano wa mwaka wa wahandisi nchini unaotarajiwa kufanyika Septemba 2-3 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Amesema kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wahandisi takribani 4000 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Agosti 26, 2024 jijini Dar es Salaam Msajili wa ERB, Benard Kavishe amesema wameona ili kuongeza ufanisi katika fani hiyo kuna haja ya kukutana na kujadili mambo mbalimbali na wahandisi vijana.
Kavishe amesema wahandisi vijana ndio kundi kubwa kwa idadi ya wahandisi waliosajiliwa na bodi hiyo.
Anasema wahandisi waliosajiliwa hadi sasa wanafikia 40,000 kati yao asilimia 70 ni vijana huku kila mwaka wamekuwa wakisajili takriban wahandisi vijana 4,000.
Ameongeza kuwa ongezeko hilo linasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ukuaji wa uchumi pamoja na kuendelea kuhamasishwa kwa vijana kusomea masomo ya sayansi.
“Tumeona kuna haja ya kukutana nao pamoja kuwapa uzoefu, maarifa na mbinu zitakazowakuza zaidi katika fani hiyo.”
“Pia namna wanavyoweza kuitumia fani hiyo kutengeneza fursa za kibishara, kuwasaidia kuunda kampuni pamoja na kuwaunganisha na kampuni kongwe ili waweze kupata uzoefu,” amesema.
Kavishe amesema katika jitihada za kuzalisha wahandisi wengi zaidi wameamua kuja na kampeni ya kuhamasisha masomo ya sayansi, hesabu na teknolojia (Steam Support Program) kwa wanafunzi hasa wa kike.
“Kama uhandisi ni mti, mbegu ni masomo ya sayansi, hisabati pamoja na teknolojia na ili kuzalisha wahandisi wazuri hamasa inatakiwa kuanzia katika ngazi za msingi za elimu,” amesema.
Amesema programu hiyo imelenga kuwawezesha walimu wanaojitolea kwa kuwawezesha kupata posho kila mwezi pamoja na bima ya afya, ili kusaidia kupunguza changamoto ya walimu hasa wa masomo ya sayansi na hisabati.
Amesema ili kufikia malengo hayo wameamua kuja na mbio maalumu (marathon) ambayo inatarajiwa kufanyika Septemba 7, 2024 jijini Dar es Salaam na inalenga kukusanya takriban Sh2 bilioni ili kuwezesha walimu wengi zaidi.
Ameongeza kuwa lengo lao ni inapofika 2030 kuwe na usawa wa kijinsia katika idadi ya wahandisi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania kitengo cha wanawake, Ester Christopher amesema bado idadi ya wahandisi wanawake waliosajiliwa hairidhishi.