Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Peter Msofe amedokeza kuanza kutumikia kwa mtalaa mmoja kwa wanafunzi wa masomo ya udaktari na uuguzi, lengo likiwa kupata wahitimu wenye sifa moja na washindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Pia kuanza kutumika kwa mtalaa huo kutawaongezea wakufunzi wa fani hizo ujuzi pamoja na kuwezesha mgonjwa kupata huduma bora na inayofanana kwa kila mtaalamu.
Mtalaa huo tayari umeanza kutekelezwa na Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Chuo Kikuu cha Afya Bugando na Chuo Kikuu cha Afya Bugando (Cuhas) pamoja na Chuo cha Afya Kilimanjaro (KCMUCo) chini ya mradi wa mabadiliko ya ufundishaji wa wataalamu wa afya ukifadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates.
“Mradi huu umetumika kutengeneza mitalaa ya mfano katika mafunzo ya udaktari na uuguzi. Mitalaa hii imeshapitishwa na taasisi ya urekebu pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na tunatarajia mtalaa huu utumike kwa vyuo vyote vya afya nchini,” amesema.
Msofe amesema mtalaa huo unalenga kutengeneza namna tofauti ya ufundishaji katika masomo ya tiba katika fani ya afya.
Amesema mtalaa huo umetokana na mahitaji kuongezeka, hivyo ufundishaji lazima ubadilike kwani miaka ya nyuma mgonjwa anapokwenda kwa daktari husubiri maelezo yote kwa daktari, lakini sasa anakwenda hospitali akifahamu ugonjwa unaomsumbua.
Mkurugenzi huyo amesema ni lazima madaktari wafundishwe namna ya kuhudumia watu wa namna hiyo, pamoja na kuzalishwa wahitimu wenye maarifa na uwezo wa kutumia ujuzi wao katika mazingira halisi ya kazi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema mtalaa huo walioutengeneza kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Duke na Chuo Kikuu cha California San Francisco Francisco za nchini Marekani, utabadilisha ubora wa mafunzo ya afya nchini.
Profesa Kamuhabwa amesema mradi huo umepitia mitalaa ya afya nchini na kuangalia namna wataalamu wa sekta hiyo wanavyofundishwa na kuainisha mambo wanayopaswa kujifunza kwa mazingira ya Tanzania na duniani.
“Mbali na mitalaa, tumewatengeneza wataalamu wa kuwafundisha walimu, mwalimu akiajiriwa tayari tuna wataalamu wetu wa kuwafundisha mitalaa hii,” amesema.
Profesa huyo amesema utekelezaji wa mtalaa huo utaanzia vyuo vya kati hadi vyuo vikuu, ili kupata wataalamu wenye ujuzi usiotofautiana sokoni, akisisitiza hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Serikali kuboresha elimu kuanzia ngazi za chini hadi vyuo vikuu.
Mratibu wa mradi huo, Profesa Gideon Kwesigabo amesema walichobaini wakati wa uandaaji wa mtalaa mpya ni kuwa mitalaa iliyopo kutowawezesha wataalamu kufanya kazi kwa vitendo, hivyo kupitia maboresho yaliyofanyika matumizi ya Tehama yamezingatiwa, ili ufanisi uwepo kwenye utekelezaji wake.
“Kupitia mradi huu tumewaongezea uwezo walimu kufundishwa wengine na kuhamasisha utafiti wakati wa ufundishaji,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Mafunzo Wizara ya Afya, Dk Saitore Laizer amesema kuanza utekelezaji wa mtalaa kwa vyuo vya afya, ni hatua muhimu itakayotoa fursa kwa nchi za Afrika Mashariki kujifunza kwa Tanzania namna ilivyofanikiwa kwenye utekelezaji wake na wizara hiyo ipo tayari kwa utekelezaji.