Siku ya nne mgomo Soko Kuu Mafinga, wafanyabiashara wapaza sauti

Mufindi. Wakati mgomo wa wafanyabiashara katika soko kuu Mafinga mkoani Iringa ukiinga siku ya nne nne leo, wafanyabiashara wa matunda, nafaka pamoja na samaki wamelalamikia wakisema mgomo huo unawaathiri kibiashara.

Mgomo huo umesababisha adha kwa wananchi na wafanyabiashara wasio na maduka, wakisema wanayategemea maduka hayo kupata bidhaa za kuuza.

Mwenyekiti wa soko hilo, Philinus Mgaya amefafanua kuwa wafanyabiashara hao wamefunga maduka kutokana na kupanda kwa kodi ya pango ya vibanda hivyo Sh 80,000 jambo ambalo wamedai bei hiyo ni kubwa kwao.

“Kupanda kwa kodi ya pango kutoka Sh8, 000 hadi kufikia 80,000 kumewafanya wafanyabiashara wameshindwe kuvumilia.

Muonekano wa maduka katika Soko Kuu la Mafinga yakiwa yamefungwa kutokana na mgomo unaoendelea ambapo leo Agosti 26, 2024 umeingia siku ya nne tangu kuanza kwake. Picha na Mary Sanyiwa

“Tumefanya jitihada mbalimbali kwenda halmashauri na ofisi ya mkuu wa wilaya hadi kwa mkuu wa mkoa, lakini kwa bahati mbaya juhudi hizo hazikuzaa matunda yoyote katika jambo hili,” ameeleza Mgaya.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba alipoulizwa kuhusu mgomo huo, leo Jumatatu Agosti 26, 2024 amemtaka mwandishi kuwauliza wafanyabiashara wenyewe.

“Mimi sina majibu, wafanyabiashara ndio wanaweza kuwa na majibu ya mgomo huo kwa sababu wao ndio wameutengeneza,” amesema Serukamba.

Mjasiriamali wa matunda, Sophia kihombo akionyesha parachichi yaliyoharibika baada ya kukosa wateja kutokana na mgomo unaoendelea katika Soko la Mafinga. Picha na Mary Sanyiwa

Akizungumzia mgomo huo, mjasiriamali wa matunda, Alice Mwagala amesema changamoto ya kufunga maduka hayo imeleta athari kubwa kwao kwa kuwa wanauza bidhaa za vyakula zinazoharibika haraka.

“Tunaomba Serikali isikilize kilio cha wafanyabishara kwa sababu tunapoteza mitaji na hatuelewi tutapata wapi, ukizingatia wengi wetu tuna marejesho ya Vicoba,” amesema Mwagala.

Naye muuza matunda, Sophia Kihombo amesema wajasiriamali hao wamekuwa wakipata adha kubwa kutokana na mwingiliano wa wateja kuingia katika soko kupunguza kutokana na mgomo huo.

Muonekano wa maduka katika Soko Kuu la Mafinga yakiwa yamefungwa kutokana na mgomo unaoendelea ambapo leo Agosti 26, 2024 umeingia siku ya nne tangu kuanza kwake. Picha na Mary Sanyiwa

“Tunaomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie sisi wajasiriamali wa Mafinga kwa sababu maduka yamefungwa leo siku ya nne, wafanyabiashara wa matunda na maduka tunategemea watu kutoka vijiji kununua bidhaa, lakini wanakuja na kukuta soko hilo likiwa  limefungwa.

“Wafanyabishara wa matunda na maduka tunategemea watu vijiji kununua bidhaa pamoja na matunda hayo kwa sababu wakifika soko kuu lazima watakuja kununua matunda katika soko letu, lakini kwa sasa tunashindwa kuuza kutoka na mgomo huu, hali inayosababisha matunda yetu kuharibika,” amesema Kihombo.

Muonekano wa maduka katika Soko Kuu la Mafinga yakiwa yamefungwa kutokana na mgomo unaoendelea ambapo leo Agosti 26, 2024 umeingia siku ya nne tangu kuanza kwake. Picha na Mary Sanyiwa

Mamalishe Happy Richard, amesema biashara imekuwa ngumu kutokana kukosa vitu vingi walivyokuwa wakinunua katika maduka ya jumla, hivyo sasa wanalazima kununua katika maduka ya rejareja, hali inayochangia biashara kuwa ngumu.

“Wafanyabishara hawa wakiendelea hivi kufunga maduka hata sisi mamalishe tutafunga bishara zetu kwa sababu maduka ya nje wanapandisha bei za bidhaa, hivyo sisi itakuwa ni vigumu kupata faida,” amefafanua Richard.

Related Posts