Aliyeomba Sh50 milioni za kupandikiza figo, bado ahitaji Sh41 milioni

Moshi. Dickson Sambo (37), anayeugua ugonjwa wa figo na anahitaji Sh50 milioni kwa ajili ya kupandikiza figo mpya, amefanikiwa kupata Sh9 milioni hadi sasa.

Hata hivyo, bado anahitaji Sh41 milioni ili kufanikisha matibabu hayo.

Sambo, mkazi wa Mbokomu Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, figo zake mbili zilifeli miaka minane iliyopita, baada ya kupatwa na shinikizo la damu na dada yake, Jackline amejitolea kumpa figo moja, lakini ameshindwa kupandikiza kutokana na kukosa fedha hizo.

Akizungumza na Mwananchi Digital nyumbani kwake leo Jumatatu Agosti 26, 2024, amesema licha ya kujitokeza hadharani kuomba msaada kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki bado hajafanikiwa.

Hivyo, anawaomba Watanzania wasichoke kumsaidia kwa kuwa bado anapambania uhai wake.

“Ndugu zangu Watanzania nimekuja tena kwenu, nawashukuru kwa wale wote walionichangia mara ya kwanza nilipojitokeza hadharani kuomba msaada wenu kutokana na changamoto niliyonayo ya figo, figo zangu zote mbili zimefaili, naombeni msaada wenu msichoke kunisaidia.

“Mpaka sasa nimepata Sh9 milioni kati ya Sh50 milioni ninazohitaji kwa ajili ya kupandikizwa figo nyingine,” amesema Sambo.

Anasema baada ya kupata Sh9 milioni ameanza kufanya vipimo yeye na dada yake ambaye amejitolea kumsaidia figo moja kwa hatua za awali.

“Hii Sh9 milioni niliyopata kwa Watanzania wenzangu nimeanza nayo vipimo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini bado sijafikia lengo, zinahitajika Sh50 milioni ili nifanikishe matibabu haya,” amesema.

Amewaomba Watanzania kuguswa na tatizo lake linalomsumbua na kwamba mpaka hapo alipofika ameuza mali zake zote na bado familia inamtegemea kama baba wa familia.

“Nawaomba Watanzania wenzangu mnisaidie katika hili niweze kurejea katika afya yangu ya awali, kuwekewa figo ndio tiba kamili ambayo itanirejeshea afya yang,” amesema Sambo.

Jackline Sambo, dada yake Dickson amesema kaka yake ameteseka kwa miaka mingi, naye anawaomba Watanzania kumsaidia kwa kuwa tayari ameuza mali zake zote akipambania uhai wake kwa ajili ya kusafisha figo.

“Nimejitolea kumpa kaka yangu figo yangu moja, kwa sababu namwona anateseka sana, tangu mwaka 2017 ni mtu anayepitia changamoto ya afya, nawaomba ndugu zangu mtusaidie ili afanyiwe huu upasuaji na awekewe figo nyingine,” amesema Sambo.

Amesema upandikizaji wa figo ni gharama kubwa na familia wamechangishana na wamefikia hatua ya mwisho.

“Tunamwomba pia Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) utusaidie familia hii, tumejitahidi kwa kila namna lakini tumeshindwa,” amesema mdogo mtu.

Dickson alianza kusumbuliwa na tatizo la figo mwaka 2017 na mpaka sasa anaendelea kusafisha figo (dialysis) katika hospitali mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro.

Related Posts