Walimu, wanafunzi Pugu wanolewa elimu ya fedha

Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa elimu ya fedha na umuhimu wa kuweka akiba kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Pugu, iliyopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam.

Hatua hii inalenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa kifedha, kuwawezesha kujiwekea akiba, kubuni mawazo ya biashara na kufahamu jinsi ya kutumia taasisi za kifedha kama NBC kwa manufaa yao ya kiuchumi.

Akizungumza katika semina hiyo leo Jumatatu Agosti 26, 2024 shuleni hapo, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji Sheria wa Benki ya  NBC, Sarah Laiser amesema elimu ya fedha kwa wanafunzi ni muhimu kwa sababu inawawezesha kuelewa jinsi ya kusimamia fedha zao, kubuni na kufuata bajeti.

“Pia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, ndiyo lengo la mafunzo haya, tunataka kuwasaidia  wanafunzi kutambua umuhimu wa akiba, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo,” amesema ofisa huyo.

Naye Mkuu wa Shule ya Pugu, Boniface Orenda ameishukuru Benki ya NBC kwa hatua hiyo na kueleza kuwa elimu hiyo ya kifedha itawasaidia wanafunzi, hasa wale wanaohitimu kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kujiendeleza kijasiriamali.

Amesema elimu hiyo imewanufaisha wanafunzi 930, wakiwemo 139 wenye mahitaji maalumu kwa sababu yalikuwa shirikishi na yenye tija kubwa kwa wote.

Wakati wa semina hiyo, maofisa wa benki hiyo wametoa mafunzo na kuwasilisha mada mbalimbali kuhusu fedha na ujasiriamali, sambamba na kutoa fursa kwa wanafunzi kujadili na kuuliza maswali kuhusu mada hizo. Pia, huduma maalumu za benki kwa wanafunzi na walimu zilitambulishwa ikiwamo ya akaunti za Mwanafunzi na akaunti ya Mwalimu.

Mbali ya darasa la fedha, maofisa wa NBC wameshiriki katika kupanda miti ya matunda na vivuli kwenye viunga vya shule hiyo, kama njia ya kuunga mkono jitihada za utunzaji mazingira.

Related Posts