Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametaja sababu tatu za kuanzisha Kampeni ya ‘Dawasa mtaa kwa mtaa, njoo tukuhudumie’ ikiwemo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuondoa lawama na manung’uniko na kuwapatia huduma ya maji safi na salama.
Kampeni hiyo itakayosambaa nchi nzima inalenga kuwa karibu na wananchi, ili wawe huru kutoa maoni yao kuhusu huduma zinazotolewa pamoja na kupima utendaji wa viongozi wa mamlaka zinazotoa huduma ya maji, ikiwemo Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa).
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 26, 2024 jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo iliyofanyika Kunduchi, Tegeta Wilaya Kinondoni, Waziri Aweso amesema msingi wa kampeni hiyo ni utekelezaji wa maazimio ya ziara ya siku tano aliyoifanya Julai 2024 katika Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya kubaini upungufu uliopo.
“Tumekuja na kampeni hii kama mnakumbuka nilifanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam, kulikuwa na changamoto mbalimbali baada ya kuziona kulikuwa na maelekezo, baadhi yamefanyiwa kazi ndiyo maana mnaona mabadiliko.
“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji kwa kutambua wanaotaabika na huduma hii ni kinamama na Rais Samia Suluhu Hassan hataki kusikia hilo na maji hayana mbadala. Tumekuja na kampeni hii kuona watu wanapata huduma kwa wakati,” amesema Aweso.
Waziri Aweso amesema kampeni hiyo itakuwa shirikishi kuanzia kwa wananchi hadi viongozi wa mitaa, madiwani na wabunge na mameneja wanapaswa kuwasikiliza wananchi kero zao.
“Katika kila kazi kuna faida, lakini maneno matupu ni hasara. Nataka iwe kampeni ya faida na kutatua changamoto na kuondoa maneno ambayo si ya msingi.
“Tukishirikisha tutafanikiwa na tusiposhirikisha tutakwama, mnapaswa kwenda sehemu zote zenye huduma na hata maeneo yasiyokuwa na huduma mnapaswa kwenda kuwasikiliza na kuwaeleza mipango yenu,” amesema.
Pamoja na kampeni hiyo, amemtaka Mkurugenzi Dawasa kuacha kutesa watu kwa kutoa huduma ya maji usiku.
“Kupata hitilafu si udhaifu, lakini toeni taarifa kuwaeleza wananchi na ukifika muda mliosema wapeni watu maji, ni muhimu kitengo cha mawasiliano ya umma kuwapa taarifa wananchi kama mnaboresha huduma,” ameagiza.
Awali, Katibu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema watendaji wa mamlaka hizo watakuwa wanatoa elimu kwa wananchi jinsi ya kusoma mita.
“Kumekuwa na malalamiko ya watu kubambikiwa bili, tunachotaka kwanza kuwaelimisha wananchi wajue kusoma bili, ili iwe rahisi kujua lakini pia kupitia kampeni hiyo tutawanganishia maji,” amesema.
Nye Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo Chama cha Mapinduzi CCM, Mkoa wa Dar es Salaam Ally Bananga amesema watendaji wa Serikali wamewakabidhi duka na wanachopaswa ni kutatua changamoto zinazowasumbua wananchi.
“Kero zipo ila malengo yetu katika sekta ya maji ni kumtua mama ndoo kichwani, kama kuna kero ni muhimu zikatatuliwa haraka na muda wote mnapaswa kuwa tayari kuwasikiliza,” amesema.
Amesema siasa za Dar es Salaam ni maji na barabara na chama hicho kimejipanga kushinda na ili wafikie azma hiyo ni lazima wawe karibu na wananchi.
Sababu kampeni kuzinduliwa Tegeta
Baada ya waziri kufanya ziara Mkoa wa Dar es Salaam, siku ya mwisho katika kikao cha majumuisho, mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima alimuomba kutembelea maeneo yake kuangalia namna miundombinu ya taasisi hiyo inavyotoa maji.
Akizungumza Julai 4, 2024 akiwa Magomeni, Gwajima aliwasilisha kero ya kumwagika ovyo maji katika maeneo yake, huku akieleza imekuwa chanzo cha uharibifu wa barabara na kila wananchi wake wakitoa taarifa watendaji hawaendi kudhibiti.
“Mabomba yamepasuka mengi maji yanatoka kila kona, ni muhimu kutengeneza mfumo wa kugundua mabomba yaliyopasuka maana yanatoka kila kona na inawezekana bili hizo zinahamishiwa kwa watu wengine,” alisema.
Katika maelezo yake, alisema kusifiana mara kwa mara hawawezi kupata maendeleo yanayohitajika, hivyo alipendekeza hatua zichukuliwe.
“Nakuomba waziri kutenga muda uje katika jimbo langu ujionee uhalisia na ikiwezekana uje na mfumo utakaosaidia kusukuma watendaji ili changamoto hizi zitatuliwe,” alisema.