Geita. Hukumu ya kesi ya mauaji ya Milembe Suleman iliyotarajiwa kutolewa leo, Agosti 26, 2024, imeahirishwa na sasa itasomwa kesho, Agosti 27, 2024, saa tatu asubuhi.
Sababu zilizotajwa za kuahirishwa kwa hukumu hiyo ni urefu wa kesi, wingi wa mashahidi, pamoja na mchakato wa utafutaji wa haki kwa pande zote mbili.
Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita anayesikiliza shauri hilo, Kelvin Mhina akitangaza ahirisho la shauri hilo, amesema sababu za kutotoa hukumu hiyo leo kama ilivyotangazwa awali ni kutokana na kesi hiyo kuwa ndefu yenye mashahidi 29.
Kesi hiyo pia ina kurasa 371 za kusoma ili aweze kuandika hukumu, hivyo kueleza kuwa sio jambo dogo licha ya kuwa wengi wanaisubiri kwa hamu kusikia hukumu itakayotolewa.
“Sio jambo dogo wakati nyie mnasubiri kwa hamu hukumu kutolewa, sisi tunaichakata ili tuweze kutoa haki, pia tunaangalia ili kutomuonea mtu, kuna uhai wa mtu umetoka lakini adhabu ya kosa la mauaji pia adhabu yake sio ndogo,”amesema Jaji Mhina na kuongeza;
“Najua kuna presha tunaona mnavyoandika, lakini kingine hukumu haijachelewa iko ndani ya muda wa siku 90 za kutoa hukumu, Mahakama bado ina muda wa kutafakari ili kutoa hukumu. Tarehe ya mwisho ya kutoa hukumu ni Septemba 29,2024, bado tuna muda lakini tulisema tutaharakisha, ingawa mambo yalikuwa mengi, kesho saa tatu asubuhi hukumu itasomwa wale wa mbivu na mbichi kujulikana leo, basi kesho saa tatu asubuhi mbivu na mbichi zitajulikana,” amesema jaji.
Tofauti na siku nyingine, leo wananchi wakiwemo ndugu wa Milembe na wale wa washtakiwa walikuja kwa wingi mahakamani kutaka kujua kitakachojiri.
Hili ni ahirisho la tatu katika kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023, awali hukumu ilikuwa itolewe Julai 19, 2024 lakini ilishindikana na kuahirishwa hadi Agosti 23,2024 ambayo nayo haikusomwa na kutangazwa kusomwa leo Agosti 26, 2024 na sasa itasomwa kesho.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastory na Musa Pastory (33) ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shitaka moja la kumuua Milembe Suleman.
Awali washitakiwa hao walikua watano na walipandishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza Mei 24,2023 na kuanza kusikilizwa Mahakama Kuu kanda ya Geita Aprili 8,2024 kwa vipindi tofauti hadi Juni 28,2024 pande zote mbili zilipomaliza kutoa ushahidi wake.
Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 29 na vielelezo 19 na baada ya ushahidi wa Jamhuri Mahakama ilimwachia huru mshitakiwa wa tano Cecilia Macheni baada ya Mahakama kuona hana kesi ya kujibu.
Washitakiwa wanne waliobaki walijitetea wenyewe na wote kwa nyakati tofauti walidai kutohusika na mauaji hayo na kuiomba Mahakama iwaachie huru.