Morogoro. Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa amewataka watetezi wa haki za binadamu hapa nchini kuongeza kasi ya kuibua na kushughulikia changamoto za ukatili na ndoa za utotoni kwenye maeneo yao, ikiwemo mitandaoni ambako nako ukatili huo unafanyika.
Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 29, 2024 kwenye mafunzo maalumu ya kuwanoa watetezi wa haki za binadamu takribani 40 kutoka kanda za kusini na kati mkoani Morogoro, amesema kwa kuwa kasi ya matendo ya uvunjivu wa haki za binadamu hufanyika mtandaoni, wameamua kuja na mafunzo maalumu ya namna ya kukabiliana na hali hiyo.
“Kwa sasa dunia imekuwa kijiji, vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinaadamu vimeshamiri na kukua kwa njia ya mtandao, hivyo ninyi watetezi mnayo haki ya kuhakikisha kwamba mnaongeza juhudi katika kuibua vitendo hivi ili jamii yetu iondokane navyo,”
“Katika kulifanikisha hilo, tumeandaa mafunzo haya maalumu ya kuwajengea uwezo wanachama wetu ili wapate mbinu mpya za ulinzi na utetezi wa haki za binaadamu, hasa kwenye suala la utoaji taarifa na maswala ya uwekaji kumbukumbu wa kazi za ulinzi na utetezi wa haki za binadamu,” amesema.
Olengurumwa amesema kwa siku za karibuni vitendo vya ubakaji kwa watoto wadogo mtaani vimekuwa vikifanyika kwa watu wakiwamo wasiotegemewa, hususan madereva na walimu, ambao hutumia mbinu za kisasa ambazo ni ngumu kugundulika.
Kwa upande wake, Edson Elias Mwakyembe, mtetezi wa haki za binadamu kutoka Mkoa wa Mbeya, amesema uwepo wa mafunzo hayo utawasaidia kuendana na kasi ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambao umeshamiri mtandaoni.
Rachel Siwiti ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu kutoka Morogoro, amesema wao kama watetezi wanakutana na changamoto ya kupata taarifa za uvunjifu wa haki za binadamu kutokana na jamii kuficha, hivyo mbinu walizojifunza zitawawezesha kupata taarifa.
“Hapa Morogoro vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu vimekuwa vingi vikihusisha makundi ya watoto wa kike kuozeshwa katika umri mdogo pamoja na wanawake kudhulumiwa mali zao pale wanapofiwa na waume zao, taarifa hizi zimekuwa zikifichwa lakini naamini kwa mafunzo haya, tunakwenda kuwa na mbinu mpya na za kisasa kukabiliana na changamoto hizi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mindu mjini Morogoro, Juma Ally amesema vitendo vya ukatili, ngazi ya familia vinafanyika lakini kwenye mtaa wake vimepungua.
“Kwenye mtaa wangu vitendo ukatili na unyanyasaji vimepungua kwa kiasi kikubwa lakini huko nyuma wanawake ndio walikuwa wakileta kesi zao kwa wingi kwamba wanapigwa na kunyanyaswa kwenye familia zao, tumejaribu kuzungumza na waume zao hali hiyo imetulia,” amesema.