Wanaharakati 21 wanaopinga mradi wa mafuta wakamatwa Uganda – DW – 27.08.2024

Mmoja wa mawakili wa wanaharakati hao wa mazingira Samuel Wanda amesema watu 21 waliokatwa, ni wanaume 19 na wanawake wawili.

Wanaharakati hao walijaribu kuandamana kuelekea bungeni na ofisi ya ubalozi wa China.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki EACOP, unaoongozwa na kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa ya TotalEnergies, unahusisha uchimbaji wa mafuta nchini Uganda na kusafarisha mafuta ghafi hadi Tanzania kwa ajili ya mauzo ya nje.

Soma pia: Mbunge wa Ujerumani aukosoa mradi wa EACOP 

Wanaharakati wa kutetea mazingira wameeleza kuwa mradi huo una athari mbaya kwa jamii na mazingira kwani shughuli ya uchimbaji inafanyika katika hifadhi ya kitaifa ya Murchison Falls, eneo kubwa lililohifadhiwa nchini Uganda.

Kampuni ya TotalEnergies hata hivyo imejitetea kwa kusema, watu waliopoteza makaazi yao au kuathirika kutokana na mradi huo wamelipwa fidia na kwamba hatua zimechukuliwa pia ili kulinda mazingira.

Mradi wa EACOP una uwezo wa kuvuna hadi mapipa bilioni 1.7 

Uganda Unterschrift EACOP in Kampala
Rais wa Tanzania Samia Suluhu na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni wakati wa hafla ya utiaji saini wa mradi wa EACOP mjini Kampala, Uganda.Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Wanda ameeleza kuwa, wanaharakati wanane kati ya waliokamatwa wangeathirika moja kwa moja na mradi huo wa TotalEnergies.

Amesema wanaharakati hao walikuwa wanashikiliwa katika kituo cha polisi cha Kampala lakini maafisa wa polisi bado hawajafafanua mashtaka dhidi yao.

Katika shauri lililoonekana na shirika la habari la AFP, waandamanaji hao walitoa ombi la dharura dhidi ya kile walichokiita ukiukaji unaoendelea wa haki za binadamu na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na mradi wa EACOP.

Soma pia: Museveni aapa kuendeleza mradi wa mafuta licha ya upinzani wa Bunge la Ulaya

Shauri hilo limeeleza kuwa, mradi huo wa mafuta ni “tishio kwa uchumi wa ndani ya Uganda” na kwamba una athari hasi za kijamii na kitamaduni.

Gharama za kukamilisha ujenzi wa mradi wa bomba zinatarajiwa kufikia takribani shilingi trilioni nane za Tanzania. Bomba hilo litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TotalEnergies, CNOOC ya China kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda UNOC na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC.

Mafuta ya kwanza yanatarajiwa kutiririka mwaka wa 2025 — karibu miongo miwili baada ya visima hivyo vya mafuta kugunduliwa — na mradi huo umepongezwa na Rais Yoweri Museveni kama faida ya kiuchumi kwa nchi hiyo isiyo na bandari na ambayo watu wengi wanaishi katika umaskini. 

Related Posts