Mwanzilishi wa Telegram akamatwa Ufaransa, maudhui ya ngono yatajwa

Paris. Mwanzilishi wa mtandao wa Telegram na mzaliwa wa Urusi, Pavel Durov anaendelea kushikiliwa na polisi baada ya kuzuiwa katika uwanja wa ndege Kaskazini mwa Paris nchini Ufaransa.

Durov (39) alikamatwa Jumapili Agosti 25, 2024 akituhumiwa kwa makosa 12 ikiwemo kushindwa kuchukua hatua za kuzuia uhalifu wa ulanguzi wa dawa za kulevya kupitia mtandao huo pamoja na maudhui ya ngono kwa watoto.

Tukio hilo inaelezwa kuwa huenda limechochewa na sababu za kisheria katika usalama wa data.

 Telegram imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kisheria katika nchi mbalimbali kutokana na sera zake za faragha na usalama wa mawasiliano.

Wizara ya Mambo ya Nje ilisema katika taarifa mapema Jumanne kwamba inafuatilia kwa karibu kesi ya Durov na kwamba imewasilisha ombi kwa Serikali ya Ufaransa kumpa huduma zote za kibalozi haraka.

“Kujali raia, kulinda maslahi yao, kufuatilia mambo yao na kuwapa matunzo ni kipaumbele kwa UAE,” wizara hiyo ilisema katika taarifa hiyo.

Licha ya kwamba Durov alizaliwa Urusi lakini alikulia nchini Italia, hivyo anatambulika kama raia wa UAE, Ufaransa, Urusi.

Hata hivyo Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron jana Jumatatu alisema kuwa kukamatwa kwa Durov haikuwa hatua ya kisiasa bali ni sehemu ya uchunguzi huru.

Akichapisha kwenye mitandao ya kijamii, Macron alisema kwamba “Ufaransa inazingatia uhuru wa kujieleza lakini uhuru unadumishwa ndani ya mfumo wa kisheria, kwenye mitandao ya kijamii na katika maisha halisi, kulinda raia na kuheshimu haki zao za kimsingi.”

Hata hivyo baadhi ya watumiaji wa mtandao huo Tanzania wamekuwa wakiulalamika muda mwingine kuwa mzito na kupata changamoto ya kupakua vitu kama picha.

Related Posts