TAASISI, MASHIRIKA YA UMMA YATAKIWA KUJIKITA UWEKEZAJI NJE YA NCHI 

 

Na: Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Taasisi na Mashirika ya Umma nchini yametakiwa kujikita katika kufikiria njia mbalimbali zitakazowawezesha kuwekeza nje ya nchi ili kusaidia nchi iendelee kujitawala kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 27, 2024 jijini Arusha wakati Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea ufunguzi wa kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kitakachofanyika kuanzia Agosti 27 – 30, 2024 katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho Agosti 28, 2024.

Mchechu amesema kuwa ili taasisi na mashirika ya umma yaweze kufanikiwa kuwekeza nje ya nchi, lazima kwanza yawe imara ndani ya nchi kwani haiwezekani kuwekeza nje ya nchi kama ndani ya nchi taasisi haiko imara.

“Tunapowataka watu wawekeze nje ya nchi tunataka wadhamirie malengo yaliyo juu zaidi, hatuna sababu ya taasisi zetu kushindwa kuwekeza nje ya nchi kwani huduma zingine zinagusa wateja walio nje ya mipaka, hivyo kutoa huduma sio lazima kuweka ofisi nje ya nchi”, amesema Mchechu.

Ameongeza kuwa, utendaji wa kazi wa taasisi za umma unatakiwa kubadilika ili kuwa na mawazo mapana yatakayowawezesha kuwekeza nje ya nchi.

Aidha, amefafanua kuwa taasisi zina wajibu wa kuwa na mipango ya muda mrefu ili ziweze kuchangia kwenye mpango mkakati wa nchi wa mwaka 2025 na sio kusubiri Tume ya Mipango ifanye yenyewe.

Kwa upande mwingine, Mchechu ameeleza kuwa hii ni mara ya pili kufanyika kwa kikao hicho na anatarajia ndani ya miaka mitatu kitakuwa cha mafanikio zaidi ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025, taasisi na mashirika ya umma kati ya 30 hadi 40 yatapunguza utegemezi kwa kuanza kujitegemea, vilevile yataweza kutoa gawio kwa serikali.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia uwekezaji wa umma ambao kwa sasa umefikia trilioni 76 ikiwa na jumla ya mashirika ya umma 248 na mashirika yasiyo ya umma 58.

Related Posts