Pacha ya Makambo, Yacouba ngoja tuone!

MSHAMBULIAJI wa Tabora United, Heritier Makambo amesema kitu pekee kinachoweza kubadilisha staili ya ushangiliaji wake wa kuwajaza ni supastaa wa  Al Nassr ya  Saudi Arabia, Cristiano Ronaldo

Makambo alisema kama Ronaldo amedumu na staili yake ya suuu na imekuwa maarufu dunia nzima, huku wachezaji wengine wakiiga, yeye ni nani hadi abadili ya kwake, hivyo alisisitiza mabadiliko yatatokana na staa huyo.

Alipoulizwa kama ni shabiki wa Ronaldo? Alijibu “Hapa namshabikia Lionel Messi uwanjani ambaye hana mambo mengi ya kushangilia, ila kuhusu ushangiliaji ni Ronaldo.”

Ukiachana na hilo, kazungumzia mipango yake katika msimu huu, anataka raundi ya kwanza anahakikisha anafunga mabao mengi yatakayomuweka kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ufungaji bora, ameanza hivyo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Namungo, ambapo alifunga na kutoa asisti.

“Siwezi kutaja idadi ya mabao, lakini nitahakikisha nafanya kazi kubwa mzunguko wa kwanza, utakaoniweka katika mstari wa malengo yangu,”alisema.

Je, unajua Makambo alihusika kushauri mchezaji mwenzake Yacouba Songne, hivi ndivyo alivyofichua hilo” Ni miongoni mwa niliomshauri Yacouba asaini Tabora United, naamini tutakuwa na pacha kali ya mabao, hasa kocha akituanzisha wote wawili tutawanyanyasa sana mabeki.”

Mbali na hilo, alimtaja Erasto Nyoni wa Namungo FC, kuwa ni kati ya wachezaji wenye maarifa makubwa na vipaji nchini, ambao wanastahili kuigwa na wengine.

“Msimu wangu wa kwanza 2018/19 niliofunga mabao 17, niliwahi kusema Nyoni kwangu mimi ni mchezaji anayenipa changamoto ya kujituma kwa bidii, kila nikikutana naye katika mechi, imekuwa hivyo tulivyocheza dhidi ya Namungo FC, wachezaji wa aina yake wanafanya ligi iwe bora,” alisema.

Related Posts