Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kesho kutoa uamuzi kuhusu maombi ya dhamana au kufikishwa mahakamani viongozi wawili wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), wanaodaiwa kushikiliwa kizuizini.
Viongozi hao, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na Katibu wake, Jacob Mlay na dereva wa pikipiki, Frank Mbise wanadaiwa kushikiliwa kizuizini na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, jijini Dar es Salaam kwa siku 10 mpaka leo Agosti 27, 2024.
Kutokana na hilo, mawakili wao wamefungua shauri la maombi wakiomba amri ya Mahakama iamuru waachiwe huru kutoka kizuizini au wajibu maombi wawafikishe mahakamani na kuendelea na taratibu nyingine za kisheria.
Katika shauri hilo la maombi namba 23998, wajibu maombi ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZPC) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO).
Wengine ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Temeke (OC- CID), Mkuu wa Kituo cha Polisi Chang’ombe (OCS), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Wilfred Dyansobera limetajwa mahakamani leo Jumanne, Agosti 27, 2024
Kiongozi wa jopo la mawakili wa waleta maombi, Peter Madeleka anayeshirikiana na mawakili Deogratius Mahinyila na Paul Kisabo, amedai kwa asili ya maombi hayo, Mahakama inapaswa kuyapa upekee kwa kuwa yanazungumzia binadamu ambao wako kizuizini.
“Kwa hiyo wakati taratibu nyingine za kisheria zitakazopendekezwa na Mahakama yako kundelea, tunaomba itoe amri waleta maombi waletwe mahakamani kwanza kwa mujibu wa kifungu cha 390 (1) (a) na (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai –CPA,” ameomba Madeleka.
Wakili Kisabo amedai shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura na kwamba, waombaji walikamatwa Agosti 18, 2024 na hawakuruhusiwa kuwaona si mawakili tu, bali hata ndugu zao.
Amedai kwa mujibu wa Kanuni ya 7 ya shauri la maombi ya aina hiyo (Habeas Corpus) Mahakama ina mamlaka ya kutoa dhamana wakati wakisubiri usikilizwaji wa shauri lao.
Akirejea Katiba, amesema ibara ya 15(1) inaeleza wazi kuwa kila mtu anayo haki ya kuwa huru na (2) inapiga marufuku mtu yeyote kukamatwa kufungiwa, kuweka kizuizini au kunyang’anywa uhuru wake isipokuwa tu kwa mujibu wa sheria.
“Ni hoja yetu kwamba waleta maombi wameporwa haki yao ya kuishi kama watu huru. Kwamba wajibu maombi hawajaleta kiapo kinzani hiyo haizuii Mahakama kutoa amri tulizoomba, kuachiwa kwa dhamana au kuletwa mahakamani ili shauri hili linapokuwa linasikilizwa nao waweze kusikiliza,” amesema.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Ndakidemi amepinga kutolewa amri zilizoombwa na mawakili hao akidai hawana uhakika kama waombaji wako Polisi.
Amedai mawakili wanahisi kuwa waombaji hao wako Kituo cha Polisi Chang’ombe, akidai wameuliza kituoni hapo wakaambiwa hawapo, akiahidi mahakamani kuwa wataendelea kufuatilia kama taarifa hizo zina ukweli.
Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilinyi ameirejesha Mahakama katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika moja ya mashauri ya aina hiyo akidai imeelekeza mtu anayefungua maombi kama hayo lazima kwanza awe na uthibitisho wajibu maombi wanawashikilia waombaji.
“Kwa uamuzi huo mawakili wa waleta maombi walipaswa waithibitishie mahakama kuwa watu hao wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, lakini mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi,” amedai.
Amedai kwa kuwa walipewa nyaraka za shauri hilo jana Agosti 26, 2024 wanaomba muda wafuatilie madai hayo.
Wakili Madeleka akijibu hoja hizo amedai ni suala la kisheria kwamba kiapo ni sehemu ya ushahidi, hivyo mawakili wa Serikali wanaposema hawajawasilisha ushahidi wowote kwamba waombaji wanashikiliwa na wajibu maombi anadhani hawajui huo msimamo wa kisheria.
Amedai namna pekee ambayo Mahakama inaweza ikafikia hitimisho kuwa waombaji hawako Polisi ni kupitia kiapo chao kinachounga mkono maombi hayo na kiapo kinzani kitakacholetwa na wajibu maombi.
Amedai wanajua wajibu maombi wana haki ya kusikilizwa lakini maombi yao ni waombaji wapelekwe mahakamani.
Amedai uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi iliyorejewa na mawakili wa Serikali haizungumzii maombi kama walioyatoa mahakamani hapo.
Wakili Mahinyila amedai hoja kwamba wamehisi waombaji wako Chang’ombe, wao hawakutamka kwa mdomo bali ni taarifa zilizoko kwenye kiapo ambacho kinapaswa kujibiwa kwa kiapo kinzani.
Jaji Dyansobera baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema zilizotolewa zinagusa vifungu vya sheria na uamuzi wa Mahakama ya Rufani ambao ni maelekezo kwa mahakama za chini.
“Kwa hiyo Mahakama hii inaamuru kwamba uamuzi wa dhamana au kuletwa mahakamani yatayolewa Agosti 28, 2024 saa 4.30 asubuhi na wajibu maombi walete kiapo kinzani kufikia saa 4.00 kamili,” amesema.
Kwa mujibu wa kiapo kinachounga shauri hilo la maombi, kilichotolewa na rafiki wa waombaji hao, Mohamed Mzindu, Agosti 18, Soka alipigiwa simu kutoka Kituo cha Polisi Chang’ombe aende kuchukua pikipiki yake iliyokuwa ikishikiliwa kituoni hapo.
Anadai alipompigia simu Soka na Mlay hawakupatikana na hata alipowauliza ndugu zao walieleza hawafahamu waliko.
Mohamed na ndugu wa Soka na Mlay walikwenda Polisi Chang’ombe kuulizia wakajibiwa hawakuwa na taarifa zao na hata walipozunguka vituo vingine vya polisi walielezwa hawajui waliko.
Anadai mara ya mwisho walionekana eneo la kituo cha polisi Chang’ombe alikokwenda Soka kuchukua pikipiki yake, hivyo ana kila sababu ya kuamini wanashikiliwa kizuizini kwa ufahamu au amri ya wajibu maombi ambao ni maofisa wa polisi.