SIMBA ndio mabingwa wapya wa michuano ya Kombe la Muungano, iliyoshirikisha timu nne zikiwamo Azam, KMKM na KVZ.
Michuano hiyo ilifikia tamati rasmi juzi visiwani Zanzibar, kwa Simba kuifunga Azam kwa bao 1-0 katika pambano la fainali lililopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan kwa bao la dakika ya 77 kutoka kwa kiungo mkabaji, Babacar Sarr.
Simba imetwaa taji la michuano hiyo iliyorejea tena mwaka huu baada ya kutofanyika kwa takribani miaka 22 tangu mara ya mwisho ilipoacha kuchezwa mwaka 2002 na kuzawadiwa Sh50 milioni huku Azam iliyomaliza ya pili ikizoa Sh30 milioni.
Ligi hiyo ilianza rasmi mwaka 1982 kwa lengo la kudumisha Muungano wetu ambao mwaka huu umefikisha miaka 60 tangu ulipoasisiwa Aprili 26, 1964 ili kutoa usawa wa kiuwakilishi katika michuano ya kimataifa ya klabu za Tanzania Bara na za Zanzibar.
Michuano hii ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo na ikishuhudia timu tisa tu zikiibuka na kombe hilo katika miaka tofauti.
Mwanaspoti linakuletea mambo mbalimbali yaliyojitokeza katika mashindano ya mwaka huu yaliyoteka hisia za mashabiki hapa nchini, lakini kubwa ni namna Simba ilivyostahili kubeba ndoo kutoka na Azam kucheza kichovu fainali na pia michuano kucheza katika mfumo tofauti na ule wa awali wa ligi na kuanzia nusu fainali.
Msimu huu zimeshiriki timu nne katika michuano hii, mbili kutoka Tanzania Bara ambazo ni Simba na Azam FC huku kwa upande wa visiwani Zanzibar zikiwakilishwa na KVZ na KMKM tofauti na miaka ya nyuma na zilikuwa zikishiriki sita.
Kabla ya kurudi msimu huu michuano hii ilikuwa ikihusisha timu sita bora, tatu bora kutoka Ligi ya Bara na tatu bora kutoka Ligi ya Zanzibar.
Bingwa wa Ligi ya Muungano ndio alihesabiwa na CAF na FIFA ndiye bingwa wa Tanzania na atakayepata nafasi ya kushiriki Klabu Bingwa ambayo kwa sasa ni Ligi ya Mabingwa Afrika huku mshindi wa pili akishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Ushindi wa juzi umeifanya Simba kufikia rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya sita na kuwafikia watani zao Yanga.
Yanga ndiyo ilikuwa ikiongoza kwa kutwaa taji hilo mara nyingi ikilichukua kuanzia 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000 kisha Simba kujibu mapigo hayo baada ya wao nao pia kulichukua wakianzia mwaka 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na 2024.
Licha ya Simba kufikia rekodi hiyo kwa wapinzani wao Yanga ila ndio timu pekee iliyochukua Kombe la Muungano mara tatu mfululizo baada ya kuhangaika kwa zaidi ya miaka 10 bila mafanikio yoyote hadi ilipofika 1993 walipokuwa na kikosi bora.
Katika mataji matano iliyochukua kati ya sita iliyonayo sasa, mara tatu Simba ilichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara yaani mwaka 1994, 1995 na 2001 kasoro 1993 na 2002 na bingwa wa Bara alikuwa ni mpinzani na mshindani wake mkubwa Yanga.
Azam imeshiriki kwa mara ya kwanza michuano hii tangu kurejea kwake na kushindwa kuandika rekodi mpya ya timu ya kwanza kuchukua ubingwa huo kwa sababu mabingwa wote tisa waliochukua ni walewale walioshiriki kuanzia mwaka 1982.
Mbali na Yanga na Simba, timu nyingine zilizotwaa ubingwa huo ni Majimaji iliyotwaa mara tatu (1985, 1986, 1998), Malindi (1989, 1992), Pan Africans (1982), KMKM (1984), African Sports (1988), Pamba (1990) na Tanzania Prisons (1999).
Katika michuano hii, tuzo ya mchezaji bora ilienda kwa Fabrice Ngoma wa Simba kutokana na kuonyesha kiwango bora katika michezo yote miwili huku kipa bora akichukua, Ayoub Lakred wa Simba pia baada ya kutoruhusu bao lolote katika mechi zote alizocheza.
Kwa upande wa tuzo ya mfungaji bora wa mashindano hayo ilienda kwa Abdul Suleiman ‘Sopu’ wa Azam FC aliyefunga mabao mawili wakati kikosi hicho kikiibuka na ushindi mnono wa 5-2, dhidi ya KVZ katika mchezo wao wa kwanza wa nusu fainali. Katika pambano hilo la fainali, Nyota wa Mchezo alikuwa ni Saido Ntibazonkiza.
Nyota na nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ baada ya mchezo alisemahaikuwa rahisi kutwaa ubingwa huo kutokana na ubora wa Azam FC, huku akiwataka mashabiki kuendelea kuisapoti timu.
“Tumecheza na timu bora lakini kosa walilolifanya tumelitumia na kuwaadhibu, kikubwa mashabiki zetu wasitukatie tamaa, ubingwa huu utaamsha morali ya michezo ya Ligi Kuu.