Moshi. Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro, linamshikilia mkazi wa Kibosho Kirima, Wilaya ya Moshi, mkoani humo, Rose Apolinary Kimaro, (57) kwa tuhuma za mauaji ya mama yake mzazi, Anastazia Shiyo (87) huku chanzo kikitajwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.
Inadaiwa kuwa, baada ya kutekeleza mauaji hayo, aliandaa taratibu zote za maziko ikiwa ni pamoja na kutafuta watu wa kuchimba kaburi, kununua mashada pamoja na mambo mengine yanayohusiana na mazishi hayo ambayo yalikuwa yafanyike wiki iliyopita.
Hata hivyo taarifa zinadai kuwa, baada ya kuandaa shughuli hiyo ya mazishi, baadhi ya ndugu waliingiwa na wasiwasi kutokana na kifo cha bibi huyo, na hivyo kwenda Polisi kuomba kibali cha kuzuia maziko hayo mpaka hapo mwili utakapofanyiwa uchunguzi wa kidaktari.

Mashada yaliyoandaliwa na mtoto anayedaiwa kumuua mama yake mzazi nyumbani kwako Kibosho Kirima, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa polisi Mkoani hapa, Simon Maigwa amesema, limetokea Agosti 17 na kwamba uchunguzi wa awali umebaini kulikuwa na mgogoro wa ardhi baina ya marehemu na binti yake huyo.
Kamanda Maigwa amesema kabla ya mauti kumfika bibi huyo, binti huyo alikwenda nyumbani kwake anakoishi na kumchukua mama yake bila ridhaa ya wanafamilia akiwa na afya njema hadi alipofariki akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi.
Akielezea tukio hilo, mwenyekiti wa ukoo, Thadei Shiyo amesema bibi huyo alichukuliwa nyumbani kwake Agosti 13 baada ya binti yake huyo kumvizia ndugu aliyekuwa akiishi naye akiwa hayupo, ndipo alipofika nyumbani hapo na kuondoka na mama yake huyo.
“Baada ya bibi kuchukuliwa katika mazingira ya kutatanisha, Agosti 13, saa 1:30 asubuhi, tuliitana ndugu kuona ni nini cha kufanya, tulikubaliana kwenda polisi kutoa taarifa na baadaye tulitoa pia taarifa kwa mtendaji na mwenyekiti wa kijiji,” ameeleza mwenyekiti huyo.
Amesema baada ya kutoa taarifa hizo kwenye mamlaka husika, siku ya tatu alipigiwa simu na mtu mmoja akimweleza kuwa mama huyo amefariki.

Kaburi lililoandaliwa na anayetuhumiwa kumuua mama yake mzazi
“Baada ya siku tatu alinipigia simu mtu mmoja, akaniambia yule mama yenu Anastazia Patrick amefariki, nikamwambia amefariki kwani alikuwa anaumwa nini wakati sisi tunajua haumwi?,” amesimulia mwenyekiti huyo.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo tata kuhusu kifo cha mama huyo, walikwenda kuomba kibali polisi cha kuzuia mazishi ambayo yalikuwa yafanyike wiki iliyopita ambapo hayakufanyika.
“Baadaye tulikaa kikao cha familia na ukoo mzima, tukaomba Jeshi la Polisi litusaidie, tukaandika barua tukatuma kwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) kuomba mazishi ambayo yalikuwa yafanyike Jumatano iliyopita yazuiliwe ili tujiridhishe na kifo cha mama yetu, maana tangu nikabidhiwe huyu bibi sikuwahi kumsikia akisema anaumwa, siku zote naenda nyumbani kwake tunaongea bila shida yoyote,” amesema.
Amesema baada ya mwili kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu, ilibainika kuwa mama huyo alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo baadhi ya mbavu zilikuwa zimevunjwa na pafu lake moja la kulia lilikuwa limeharibika.
Getruda Shiyo, ambaye ni mtoto wa bibi huyo amesema dada yake huyo amekuwa na ugomvi na mama yao kwa muda mrefu wakigombania kipande cha ardhi katika eneo la familia.
“Chanzo cha tukio hili la kumuua mama yangu ni ugomvi wa shamba alilokuwa akigombania na ilifikia mahali dada yangu akawa ananiambia lazima amuue mama,” amesema na kuongeza:
“Nilishirikisha ukoo, nikawaeleza hali halisi ya dada anachotaka kukifanya kuhusu shamba na tangu wakati huo dada alinichukia na hakutaka kuwa karibu na mimi kwa kumkemea alichokuwa anadhamiria kukifanya kwa mama yangu, alifuta hadi namba zangu za simu.”