Wakazi wa Kigamboni kunufaika mradi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam wanatarajia kunufaika na mradi mpya wa kimataifa unaolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku ukitoa fursa za kiuchumi kwa jamii.

Mradi huo, unaojulikana kama ‘Kukuza Maarifa kwa Manufaa ya Muda Mrefu na Ustahimilivu wa Tabianchi Kupitia Huduma za Tabianchi Holistiki na Suluhisho za Msingi wa Asili (ALBATROSS), unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga ya asili yanayoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia, mradi huo utaunda zana na maarifa bunifu ili kusaidia kupitishwa kwa mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo ni ya kutekelezeka, yenye ufanisi na endelevu katika sera na mipango ya Afrika. Utatekelezwa katika nchi nne za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Tanzania, Madagascar, Afrika Kusini, Ghana, na Kenya.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Agosti 27, 2024, Mratibu wa mradi huo, Profesa Wilbard Kombe amesema utalenga maeneo yanayokabiliwa na changamoto za mazingira kama vile kupungua kwa mvua, kuongezeka kwa joto na kuenea kwa mafuriko na dhoruba.

“Mradi wa utafiti utaangazia Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, eneo la pwani linalokabiliwa na hatari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa, kuongezeka kwa viwango vya bahari na hali mbaya ya hewa. Mradi huu utaanza kwa kulenga eneo moja ndani ya Kigamboni,” amesema Profesa Kombe.

Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, mradi wa ALBATROSS utahusisha wakazi wa Kigamboni katika shughuli za hifadhi ya mazingira ikiwamo urejeshaji wa mikoko, uhifadhi wa bayoanuwai ya majini na ufugaji wa nyuki.

Shughuli hizi siyo tu zitasaidia kulinda mazingira bali amesema zitatoa fursa za ajira na kipato kwa wakazi wa Kigamboni, hususan wanawake na vijana.

Profesa Kombe amesema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano na jamii za Kigamboni, ambapo vikundi vya kijamii kama vile vya ufugaji nyuki, ulinzi wa jamii na vikundi vya wanawake na vijana.

Wengine ambao watashirikishwa ni viongozi wa mitaa na halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni katika kuhakikisha utekelezaji wa mafanikio wa mradi.

Kwa upande wake, Mtafiti wa mradi huo, Profesa Alphonce Kyessi amesema mbali na kuhifadhi mazingira pia unalenga kutoa fursa za kiuchumi kwa jamii.

Amesema kwa kushirikiana na taasisi za serikali kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Idara ya Uvuvi, mradi huu utawezesha wakazi wa Kigamboni kupata maarifa na mbinu bora za kuhifadhi mazingira na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi kwa njia endelevu.

Mmoja wa wakazi wa Kigamboni, Fatuma Juma, ambaye ni mama wa watoto watatu amesema  amefurahia kusikia kuhusu mradi huo, kwani kwa kiasi fulani mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri maisha yao hasa kipindi cha mvua za El-Nino.

Related Posts